TTCL

EQUITY

Tuesday, April 26, 2016

Matokeo ya awali ya uchaguzi SERBIA yaonesha VUCIC anaongoza

 
ALEKSANDAR VUCIC
Matokeo ya awali ya uchaguzi uliofanyika jana nchini SERBIA yanaonesha kuwa Waziri mkuu  ALEKSANDAR VUCIC ameshinda  baada Chama chake cha  Progressive Party kuongoza kwa kupata asilimia 57 ya kura zilizopigwa.
VUCIC ambaye amekuwa waziri mkuu wa SERBIA tangu mwaka 2014 aliitisha uchaguzi wa mapema akisema anataka kuwa na mamlaka ya kumuwezesha kufanya mageuzi yanayohitajika ili nchi hiyo iweze kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.
Kamishna wa Umoja wa Ulaya JOHANNES HAHN alikuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza kumpongeza VUCIC kwa ushindi wake. SERBIA, taifa lenye idadi ya watu Milioni Saba lilianzisha mchakato wa kujiunga na Umoja wa Ulaya mwezi Desemba mwaka jana.

Chama cha FREEDOM PARTY chashinda duru ya kwanza ya urais


Matokeo ya awali yanaonyesha kiongozi wa chama hicho NOBERT HOFER ameshinda kwa asilimia 36.7 ya kura.
Matokeo hayo yana maana kuwa kwa  mara ya kwanza tangu mwaka 1945, AUSTRIA haitakuwa na Rais anayetokea chama cha Social Democrats wala chama cha People's Party.
Wagombea wawili walioteuliwa na vyama tawala walishindwa kufuzu katika duru ya pili ya uchaguzi inayotarajiwa kufanyika tarehe 22 mwezi ujao.
Ushindi huo wa chama cha FPO unadhihirisha kutoridhishwa kwa wapiga kura na hali ilivyo katika kuendeshwa kwa masuala ya AUSTRIA.

Watanzania waadhimisha miaka 52 ya Muungano

Watanzania hii leo wanaadhimisha miaka 52 ya Muungano wa TANGANYIKA na ZANZIBAR ambapo nchi hizi mbili ziliingia kwenye Mkataba wa Muungano mnamo tarehe 22 Aprili, 1964

Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume tarehe 22 Aprili, 1964 huko Zanzibar. 
Mkataba huo ulithibitishwa tarehe 26 Aprili, 1964 na mnamo tarehe 27 Aprili, 1964, viongozi wa nchi zote mbili walikutana katika ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam na kubadilishana hati za Muungano.
Hata hivyo hakutakuwa na sherehe za maadhimisho ya MUUNGANO kufuatia Rais Dokta JOHN MAGUFULI kuagiza fedha zilizopangwa kutumika kwa ajili ya kugharimia vinywaji, vyakula, gwaride, halaiki, burudani mbalimbali na hafla ya usiku ambazo ni zaidi ya shilingi BILIONI MBILI zitumike kupanua barabara ya MWANZA Airport katika eneo linaloanzia GHANA QUARTERS hadi uwanja wa ndege wa MWANZA.
Barabara hiyo inafanyiwa upanuzi kutatua msongamano mkubwa wa magari ambao umekuwa ukiathiri shughuli mbalimbali katika eneo hilo.
Wananchi wametakiwa kuadhimisha sherehe hii wakiwa majumbani au wakiwa katika shughuli zao binafsi.

Mtanzania Anaswa na Unga wa Bil. 10

madawa 
Herry Mussa aliyenaswa na ‘unga’

Stori:  Makongoro Oging’ UWAZI
DAR ES SALAAM: Hii ni funga kazi sasa! Kuna habari kwamba, Mtanzania anayejulikana kwa jina la Herry Mussa Yange (42), amenaswa na polisi nchini Botswana akiwa na madawa ya kulevya ‘unga’ yenye thamani ya shilingi bilioni 10.5, Uwazi limefukunyua.

madawa sauzi (2)Polisi wakikagua mzigo huo.
  • ILIVYOKUWA
  • Alikuwa akiusafirisha kwa lori (semitrela).
  • Alitokea DRC na wenzake wawili.
  • Avuka mipaka ya nchi kadhaa, akamatiwa Sauzi.
madawa sauzi (3)Shehena ya unga aliyokamatwa nayo.
  • Polisi wa Sauzi wamstukia, watumia mbinu za Kiintelijensia kumnasa.
  • Akutwa na mifuko 141 ya Unga aina ya mandrax, paketi 1,000 ndani yake.
  • Wafunguliwa mashtaka hukohuko.
madawa sauzi (1)
  • Uwazi lanena na Kamanda wa Polisi wa Kitengo cha Kupambana na Kuzuia Madawa ya Kulevya Tanzania, ACP Mihayo Msikhela, alikiri kupokea taarifa hizo.
  • Kamanda wa Viwanja vya Ndege Tanzania, ACP Martin Otieno yeye anasemaje kuhusu Mtanzania huyo kama alipitia katika viwanja vya nchini kuelekea DRC?

Mbunge Nusura… Akamatwe na ‘unga’ Da

PTKamanda wa Kitengo cha Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya, ACP Mihayo Msikhela
Na Makongoro Oging’ UWAZI
 
Dar es Salaam: Jeshi la Polisi Kitengo cha Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya, wiki iliyopita nusura limnase mbunge mmoja kutoka jimbo moja lililopo katika moja ya mikoa ya pwani (jina linahifadhiwa) baada ya kumuwekea mtego kutokana na madai kwamba alikuwa akisafirisha madawa ya kulevya ‘unga’ kutoka kwenye ufukwe mmoja wilayani Bagamoyo kuelekea jijini Dar.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa vyanzo vyetu ndani ya jeshi hilo zinadai kuwa, msamaria mwema mmoja alivujisha siri kwa jeshi hilo kwamba, mbunge huyo amebeba unga kwenye gari lake dogo akielekea Dar ambapo bila kupoteza muda, polisi walimuwekea mtego kabambe kwenye njia ambazo alitarajiwa kupita ambapo hata hivyo, aliukwepa baada ya kubadilisha njia.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, mbunge huyo alikuwa akipita usiku wa saa mbili na mzigo huo lakini inadaiwa kuwa alishtukia kwamba amewekewa mtego hivyo akabadilisha njia na kusababisha asikamatwe.
Habari zinasema kuwa, mbunge huyo amekuwa akihusishwa na biashara hiyo lakini hajawahi kukamatwa kutokana na njia anazozitumia kuendesha biashara hiyo kuwa za ujanja wa hali ya juu huku akiwatumia watu.
“Baada ya kumkosa, ilibidi polisi watawanyike lakini kwa sasa wanaendelea kumfuatilia kwa karibu, naamini akiendelea siku si nyingi atanaswa,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya jeshi hilo.
Kamanda wa Kitengo cha Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya, ACP Mihayo Msikhela (pichani) alipoulizwa na Uwazi juzi, alisema tetesi hizo amezisikia lakini hajui kinachoendelea kwa sababu ameripoti kazini hivi karibuni na kukabidhiwa ofisi na mtangulizi wake, Kamanda Kamishna Robert Boaz.

Habari za hivi punde; Lucy Kibaki afariki dunia




Mke wa Rais wa Zamani wa Kenya, Mama Lucy Kibaki (pichani) amefariki dunia nchini Uingereza katika hospitali ya Bupa Cromwell alipokuwa akipatiwa matibabu, taarifa hizo zimethibitshwa na Rais Uhuru Kenyatta ambapo amesema aliugua kwa zaidi ya mwezi mmoja na alikuwa akipatiwa matibabu Kenya kabla ya nchini Uingereza kwa tiba zaidi.
Rais Uhuru Kenyatta amesema katika taarifa yake hiyo Mama Kibaki, atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa kwenye maendeleo ya nchi na hasa alivyosaidia katika mapambano dhidi ya Ukimwi
Unboundaries News: Inatoa pole kwa ndugu, familia ya marehemu na Wakenya wote kufuatia msiba huu mkubwa na Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema Ameen.!

Serikali kuendelea kufanya tathmini ya Viwanda

Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina, inafanya ufutaliaji na tathmini katika viwanda na mashirika ya Umma yaliyobinafsishwa ili kubaini kama mikataba waliyoingia inafuatwa au la ili kuchukua hatua stahiki.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage
Akizungumza jana bungeni katika kipindi cha maswali na majibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, amesema mikataba yote ya mauzo inapitiwa endapo itabainika kuwa imekiuka mashariti hatua za kisheria zitakuchukuliwa ikiwemo serikali kuvirejesha viwanda hivyo.

Mhe. Mwijage, amesema kuwa viwanda ambavyo vitaonekana wamiliki wanauwezo wa kuvifufua makubaliano mapya yatafikiwa huku akiongeza kuwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza nchini watatafutwa.

Aidha Waziri huyo wa Viwanda amesema kuhusu viwanda ambayo vimebainika kuwa havifanyi kazi wanavifatilia kwa kuangalia ubinfsishaji wa kisheiria ili kuvirejesha mikoni mwa serikali kisheria ili kuepuka migangano ambayo inaweza kujitokeza.

Mhe. Mwijage ameongeza kuwa kwa viwanda ambavyo vilibinafsishwa kwa wawekezaji wazawa watawafata ili wasaidiane nao kujua changamoto zinazowakabili kufanya uzalishaji na kuwasaidia waweze kuvifufua viwanda vyao.

Pia ameongeza kuwa serikali inaendelea kufanya jitihada za kudhibiti uingizwaji wa bidhaa za nje zisizo na ubora ili bidhaa zinazozalishwa katika viwanda vya ndani viweze kupata masoko bora ya bidhaa zao.

Afrika inaweza kuwa haina malaria ifikapo 2020

Mataifa sita ya Afrika yanaweza kuwa salama na Malaria hadi ifikapo mwaka 2020, kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la afya duniani iliyotolewa jana mjini Geneva kuadhimisha siku ya Malaria ulimwenguni .
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani -WHO - Dokta Margaret Chan.
Mojawapo ya malengo ya shirika la WHO kwa mradi wa kupambana na Malaria kati ya mwaka 2016 hadi 2030 ni kuteketeza homa ya Malaria katika nchi angalao 10 hadi mwishoni mwa mwaka 2020.
"Shirika la WHO linakadiria mataifa 21 yanaweza kulifikia lengo hilo,ikiwa ni pamoja na mataifa sita ya eneo ambako mzigo wa maradhi hayo ni mzito zaidi-limesema shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Geneva.

Nchi hizo sita ni pamoja na Algeria,Botswana,Cape Verde,Comoros,Afrika Kusini na Swaziland. Mataifa mengine yanayoaminiwa yanaweza kuangamiza Malaria hadi mwisho wa mwaka 2020 ni pamoja na China Malaysia,Korea ya kusini,Saud Arabia,Oman,Srilanka,Timor Mashariki ,Nepal,Bhutan na mataifa manane ya Latin Amerika. Kwa mujibu wa ripoti ya WHO,watu 214 milioni wanaugua homa ya Malaria iliyoangamiza maisha ya watu 438.000.
Asili mia 90 ya waliokufa ni kutoka eneo la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara.

Monday, April 25, 2016

Semina ya ajira yavutia wanafunzi vyuo vikuu

TBL Group yawapiga msasa kuhusiana na changamoto za ajira

Taasisi na makampuni mbalimbali mwishoni mwa wiki  yalishiriki katika semina ya kuwaandaa wanafunzi  wanaosoma vyuo vikuu kuingia kwenye ajira watakapomalizika masomo yao  ambayo ilifanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kushirikisha wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali vya elimu ya juu.
Kampuni ya TBL Group ilishiriki katika semina hiyo ambapo Meneja wake wa kuendeleza vipaji  Lilian Makau,alitoa mada kuhusiana na jinsi ya kuhimili kufanya kazi kwenye kampuni  kubwa na zenye mifumo thabiti ya kiutendaji  na changamoto za kupata ajira.
Wanafunzi wengi pia walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali kuhusu taratibu za ajira katika kampuni ya TBL ambapo aliwaeleza kuwa kampuni inatoa fursa za ajira kwa watanzania wote na taratibu zake za ajira ziko wazi na pia kuwa imekuwa na utaratibu wa kuajiri wasomi waliohitimu mafunzo vyuoni na kuwapatia mafunzo ya ndani na wengi wao wametokea kuwa na utaalamu wa kiwango cha juu baada ya muda mfupi kwenye ajira zao.

Lilian Makau
Meneja wa kuendeleza vipaji wa TBL Group, Lilian Makau akitoa mada wakati wa semina ya kuwaandaa wanafunzi wanaosoma vyuo vikuu (hawapo pichani) kuingia kwenye ajira watakapomalizika masomo yao iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Aisec 2
Pichani juu na chini ni  baadhi ya wanafunzi wakisikiliza mada na kuuliza maswali.

Aisec 12
Aisec 7
Baadhi ya wanafunzi wakipata maelekezo kutoka kwa Meneja wa kuendeleza vipaji wa TBL Group, Lilian Makau muda mfupi baada ya kumalizika semina.

Fuatilia mijadala ya Bungeni leo Aprili 25 hapa

Bunge (1)

SIMU.TV: Mbunge wa Kiteto Mhe. Papian aihoji serikali juu ya upelekaji wa gari la wagonjwa pamoja na mafuta ili kurahisisha huduma za kliniki; https://youtu.be/cjcg-A_ZExM
SIMU.TV: Mhe.Ester Midimu aihoji serikali juu ya hatua za haraka za ujenzi wa nyumba za watumishi katika wilaya mpya ya Ikirima;https://youtu.be/VTbOQNvetT8
SIMU.TV : Je ni vigezo gani hutumika kuanzisha wilaya mpya? Naibu waziri wizara ya tamisemi, utumishi na utawala bora Mhe.Jafo anajibu swali hilo; https://youtu.be/n7voN7wZowU
SIMU.TV: Serikali yatenga dolla za Kimarekani laki 540 kwaajili ya upembuzi yakinifu na ujenzi wa miundombinu ya barabara na mitaro Mtwara; https://youtu.be/lW-tPDKT2l4
SIMU.TV: Mhe. Peter Selukamba mbunge wa Kigoma aikalia koo serikali juu ya upatikanaji wa maji Kigoma kaskazini;https://youtu.be/F54Cexl2zso
SIMU.TV: Mbunge wa Moshi Mhe.Raphael ahoji viwanda vilivyobinafsishwa kutumika kama maghala badala ya kuendelezwa na kutumika kukuza ajira; https://youtu.be/cw_Yf3OEBCE
SIMU.TV: Ukistaajabu ya Musa utayaona ya firauni, huko mjini Moshi kiwanda kilichokosa muwekezaji chapangishwa kwa Sh.elfu 20;https://youtu.be/soa8mIfW_OI
SIMU.TV: Naibu waziri wa fedha na mipango Dr. Ashatu Kijaji  atanabaisha juu ya hatma ya baadhi ya wastaafu kutolipwa mafao yao baada ya kustaafu; https://youtu.be/uKhbIM-S2NA
SIMU.TV: Je ni utaratibu gani unatumika kukokotoa kodi katika forodha zinazopokea bidha za nje ya nchi ambazo pia zinazalishwa nchini?https://youtu.be/ig2YZASnsd4
SIMU.TV: Fahamu mpango wa serikali katika kuwasaidia wakulima wa korosho waliopata hasara kufuatia mikorosho kukumbwa na magonjwa; https://youtu.be/E4gnNOE27aU
SIMU.TV: Waziri Husein Mwinyi akitoa majibu ya serikali juu ya uboreshaji wa makazi  kwa askari wa majeshi ya ulinzi nchini;https://youtu.be/bWfu6caJJuc

CAG akabidhi ripoti ya ukaguzi wa mwaka wa fedha Juni. 2015 bungeni leo

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Juma Assad amekabidhi ripoti ya ukaguzi ya mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2015 bungeni leo ili iweze kujadiliwa na wabunge katika Bunge la bajeti ya mwaka 2016/2017.
Katika ripoti yake, CAG ametoa mapendekezo kadhaa ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi ili kuboresha matumizi ya fedha za Serikali kwa malengo yanayokusudiwa.
Miongoni mwa maeneo ambayo CAG ametoa mapendeklezo ni Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ifuatilie suala la uwasilishaji wa taarifa za fedha kwa wakati kulingana na matakwa ya sheria.
Hatua hiyo ya CAG inafuatia ukaguzi uliofanywa kwenye vyama vya siasa nchini vyenye usajili wa kudumu ambavyo jumla yao ni vyama 22.

Juma Assad 1
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Juma Assad akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo mjini Dodoma juu ya ripoti ya ukaguzi ya mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2015 ili iweze kujadiliwa na wabunge katika Bunge la bajeti ya mwaka 2016/2017.

Prof. Assad alisema kuwa kati ya vyama hivyo vyenye usajili wa kudumu, ni chama kimoja ndicho kilichowasilisha hesabu zake kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Januari hadi Juni 2015 ambacho ni Chama cha Wananchi (CUF).
Vyama vingine 21 havikuwasilisha vitabu vya hesabu kwa ajili ya ukaguzi kinyume cha kifungu Na. 14 cha Sheria ya vyama vya siasa Na. 5 ya mwaka 1992.

Juma Assad
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Juma Assad akiongea na waandishi wa habari leo mjini Dodoma juu ya ripoti ya ukaguzi ya mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2015 ili iweze kujadiliwa na wabunge katika Bunge la bajeti ya mwaka 2016/2017.

04
Waandishi wa habari wakipokea ripoti ya ukaguzi ya mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2015 ili iweze kujadiliwa na wabunge katika Bunge la bajeti ya mwaka 2016/2017.(Picha na Eleuteri Mangi-MAELEZO).

Habari Picha; Yaliyojili Bungeni Dodoma Leo

IMGS2819
 Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akiteta na Mbunge wa Mwibara, Kange Lugola, bungeni mjini Dodoma mapema leo Aprili 25, 2016.

IMGS2749 
Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akiteta na Waziri wa maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.

IMGS2690
IMGS2729
 Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akiteta na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sere, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama (katikati na Mwanansheria Mkuu wa Serikali, George Masaju.

IMGS2553
Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akiteta na   Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sere, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama.

IMGS2574
Waziri Mkuu, Majaliwa akiteta na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Phillip Mpango

IMGS2782
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe (kulia) akiteta na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi.

IMGS2838
Mwenyekiti wa Bunge Dkt. Mary Mwanjelwa  (kushoto) akiteta na Mbunge wa Viti Maalum Grace Kiwelu.

IMGS2875Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu

IMGS2950
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Mbunge wa Busanda, Lolesia Bukwimba kwenye viwanja vya bunge mjini Dodoma mapema leo Aprili 25, 2016. Katikati ni Mbunge wa Urambo, Margaret Sitta.

UKOLONI ,UJAMAA , SHULE ZA KATA NA UJANJA WA KISASA

Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Elimu, Clifford Tandari akishiriki kwenye kongamano la kujadili Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu (ESDP)
Imekuwa fasheni katika miaka ya karibuni watu kukosoana kwa asili zao, hali zao za maisha, rangi , maumbile yao na hata aina ya elimu waliyonayo ama waipatayo.
Si tatizo watu kukosoana , bali wakosoane kwa hoja na hoja haziji kwa hulka, mihemko ama mahaba na jambo jadiliwa bali hoja huja kwa ujuzi na maarifa ambavyo ni zao la elimu.
Elimu ni nini?
Ukitaka kujua maana ya neno elimu unaweza ukaja na majimbu mbalimbali kichwani mwako ama kwenye vichwa vya watakao kupa hiyo maana.
Kwa uelewa wangu elimu ni ujuzi ama stadi ambazo mtu ama kiumbe hujifunza (kwa hiari ama lazima) ama hufunzwa ili kukabiliana na mazingira.
Viumbe hukabiliana na mazingira ili kuweza kuishi na kutengeneza maisha bora ya vizazi tarajiwa.
Kwa binadamu elimu hutolewa /hupatikana kwa njia kuu mbili ile iliyorasmi na isiyo rasmi.Mifumo isiyorasmi ilianza tangu zama za ujima ambapo kupitia elimu moto ukapatikana, watu wakafuga, wakawinda na kufanya mengi ambayo yamekuja kusaidia vizazi vilivyofuata na mifumo rasmi kwa barani Afrika ililetwa kipindi bara hili lilipoanza kushirikiana na jamii za mabara mengine kama Asia na Ulaya huku mashirika ya dini ya kiisalam na kikristo.
Elimu hii ya mfumo rasmi ambako kuna mitaala iliyoandikwa ndiyo iliyoleta mbadiliko makubwa katika jamii nyingi za kiafrika.Hapo ndipo mgawanyo wa kazi na matabaka yakatengenezwa na kuimarishwa badala ya matabaka kuwa katika nyanja za uchumi na kisiasa pekee elimu hii iliongeza matabaka ya waliosoma na wasiosoma kisha hata uchumi na siasa ukaanza kuingiliwa na matabaka ya elimu.
Kwa Tanganyika, elimu ya mfumo rasmi iliyoletwa na watangulizi wa wakoloni ikatumika kipindi cha ukoloni hadi wakati wa azimio la Arusha.Elimu ile iliyolenga kutoa ujuzi kidogo na kuandaa watumishi wa kuwatumikiwa wakoloni na kuimarisha dola yao ,ilifanyiwa mageuzi kadhaa ambayo bado madoa yake ni ngumu kufutika.
Baada ya azimio la Arusha ikaonekana misingi bora ya kuifanya elimu kweli ni njia ya kuifanya jamii iweze kukabili mazingira(kuyafanya mazingira kuwa mahali pa kuishi na kupata mahitaji kiurahisi/maendeleo).
Ugunduzi ulizingatiwa ,uzalendo na utamaduni pia , lakini baada ya miaka kadhaa pale tulioingia kwenye ile mipango ya kimaendeleo ya kibepari (SAP na mingine kama hii) hapo tukapoteza lengo na kujikuta tukitumbukia kwenye ile elimu tuliyoikataa wakati tunaleta azimio la Arusha.
Mitaala ikaanza kubadilishwa na wanasiasa walivyojisikia, shule tena haikuwa mahali pa kupata uzalendo bali kuwagawanya watu katika matabaka ya waliosoma na wasiosoma.Kuwa na elimu ikawa ni kufika sekondari ama chuo kikuu na si shule ya msingi na VETA.
Baadaye zikaanzishwa shule zilizokuwa na mlengo wa kijamaa (shule za kata) na zikaanza kufanya kazi ya kibepari.
Hapo ndipo ujanja wa kisasa ulipoanza, tuliobahatika kusoma shule hizo tukakosa ujanja, usichangie sehemu utaambiwa ulisoma shule za kata, hamna kitu ni kayumba nyie hamjui kiingereza sayansi hamuijui wazee wa zero na mengine mengi hapo ujanja ni kutosoma shule za kata wakijua umesoma huko una hatari.
Walioanzisha shule za kata na walioanza kutoa mawazo haya ni wale ambao ama walipata elimu ya kikoloni ama ya kijamaa sasa tumlaumu nani aliyesoma shule za kata ama aliyeanzisha shule za kata kwa kujua ama kutojua ili kuleta matabaka.Shule zilizoitwa za vipaji maalum hazikutosha kupokea wanafunzi wote walifahulu kukahitajika mbadala lakini hawa wasomi wa zamani wakatuletea mbadala usiokamilika na madaraja yakaongezeka.
Nitawaambia wanangu kuwa sikutoka kapa kusoma shule za kata japo tulionekana masikini na wasio na akili nilipata ujuzi ambao ulinifanya nikaishi maisha bora pengine kuwazidi wale waliojiona bora, shule za kata ndizo zilizokuwa daraja nikafika kidato cha tano na chuo kikuu ambako nikakutana na wajanja wa shule za matajiri wanaoongea kiingereza kama malkia lakini wana ujuzi sawa , zaidi ama kidogo kuliko ujuzi nilionao.
Hao ndio niliowahi kuwapa akili ya kupika wali na chai na kukifanya chakula cha jioni nilipowakuta wakilia hawana mboga huku wana mchele na sukari ndani kifupi walishindwa kupambana na mazingira licha ya ujanja wao.

Uanzishwaji maeneo ya kiutawala ni mgumu-TAMISEMI

Serikali imesema kuwa uanzishwaji wa maeneo mapya ya utawala kwa ajili ya kupelekea huduma muhimu wananchi karibu zaidi ni suala gumu kiutekelezaji ambalo linahitaji uvumilivu kutoka kwa wabunge wanaomba uundwaji huo kutokana na ufinyu wa bajeti.
Waziri wa TAMISEMI, Mhe George Simbachawene.
Akitolea ufafanuzi juu ya suala hilo leo Bungeni,Waziri wa TAMISEMI,Mhe George Simbachawene, amesema kuwa kuna maombi mengi kutoka kwa wabunge ambao wanataka maeneo yao kuanzishwa kwa halmashauri au wilaya suala ambalo ni gumu kutekelezeka kutokana na bajeti ya serikali.

Mhe. Simbachawene amesema kuwa wabunge wengi wameahidi wananchi wao kuwa watayafanya maeneo yao kuwa na halmashauri au Miji midogo hali ambayo inakua vigumu kwa serikali kujenga ofisi kuu za maeneo hayo mapya kwa wakati wanahitaji wabunge.

Mhe. Simbachawene amewataka wabunge hao kuwa wavumilivu wakati serikali ikiendelea kuongeza bajeti ya kuboresha maeneo mapya yaliyoanzishwa lakini pia wanaendelea kufuatilia mchakatao wa uanzishwaji wa maeneo hayo.

Rais Magufuli ateua wa makatibu tawala wa mikoa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 25 Aprili, 2016 amefanya uteuzi wa Makatibu Tawala wa Mikoa 26 ya Tanzania Bara.

Taarifa iliyotolewa leo na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa kati ya Makatibu tawala hao 10 ni wapya, 2 wamebadilishiwa vituo vya kazi na 13 wamebakisha katika vituo vyao vya sasa.

Makatibu Tawala wapya walioteuliwa ni kama ifuatavyo;
Arusha - Richard Kwitega
Geita - Selestine Muhochi Gesimba
Kagera - Armatus C. Msole
Kilimanjaro - Eng. Aisha Amour
Pwani - Zuberi Mhina Samataba
Shinyanga - Albert Gabriel Msovela
Singida - Dr. Angelina Mageni Lutambi
Simiyu - Jumanne Abdallah Sagini
Tabora - Dkt. Thea Medard Ntara
Tanga - Eng. Zena Said
Makatibu Tawala waliobadilishwa vituo vya kazi ni kama ifuatavyo;
Kigoma - Charles Amos Pallangyo (Kutoka Mkoa wa Geita)
Morogoro - Dkt. John S. Ndunguru (Kutoka Mkoa wa Kigoma)
Makatibu Tawala waliobakishwa katika vituo vyao vya sasa vya kazi ni kama ifuatavyo;
Dar es salaam -Theresia Louis Mbando
Dodoma - Rehema Hussein Madenge
Iringa - Wamoja Ayubu Dickolagwa
Katavi - CP Paul Chagonja
Lindi - Ramadhan Habibu Kaswa
Mara - Benedict Richard Ole Kuyan
Manyara - Eliakimu Chacha Maswi
Mbeya- Mariam Amri Mjunguja
Mtwara - Alfred Cosmas Luanda
Mwanza - CP. Clodwing Mathew Mtweve
Njombe - Jackson Lesika Saitabau
Rukwa - Symthies Emmanuel Pangisa
Ruvuma - Hassan Mpali Bendeyeko

Makatibu Tawala wa Mikoa 10 ambao wameteuliwa kwa mara ya kwanza, wataapishwa siku ya Jumatano tarehe 27 Aprili, 2016 saa tatu asubuhi Ikulu Jijini Dar es salaam.

Mwigulu Nchemba atoa sababu 5 kilimo kuendelea TZ

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mh. Mwigulu Nchemba ametoa sababu tano muhimu ambazo zinaweza kusaidia nchi kupiga hatua mbele kwenye kilimo na kusema moja ya hatua ni kuhakikisha watu wanaacha kilimo cha jembe la mkono kwa kuanza kutumia matrekta.
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mh. Mwigulu Nchemba
Ili kukuza kilimo Mh. Nchemba amesema serikali inatakiwa kutengeneza mazingira ya kuunganisha mikoa kwa mifereji ili kuwezesha kilimo cha umwagiliaji ambacho kitakuwa hakina msimu wala hakitategemea mvua kama kilimo cha sasa ambacho kimekuwa kikitegemea mvua za msimu.
"Ili kilimo kiendelee Tanzania kinahitaji yafuatayo kwanza, kilimo cha kutumia Matrekta. Ni lazima kubadili mlinganyo uliopo wa watu wengi kutumi jembe la mkono kwenda watu wengi kutumia matrekta na kidogo kutumia Wanyama kazi. Jembe la mkono linatakiwa kuonekana Makumbusho ya Taifa yaani Museum na makaburini. Pili Kilimo cha Umwagiliaji, lazima serikali kuunganisha Mikoa kwa mifereji ya Umwagiliaji ili wakulima wayatoe maji kwenye hiyo mifereji kwenda mashambani mwao, pana safari ndefu hapa," alisisitiza Mwigulu Nchemba
Lakini mbali na hayo alizidi kutoa ufafanuzi kuwa matumizi ya pembejeo ni muhimu katika kufanya kilimo na zinatakiwa kupatikana popote nchini na kwa watu wote masikini na matajiri kama ambavyo watu wanaweza kununua vinywaji baridi.
"Matumizi ya Pembejeo, ni lazima mbolea, mbegu bora na dawa zipatikane madukani kama sodaa inayopatikana popote na kwa wakati, kwa tajiri na masikini na kwa bei ya kumudu kila mtu. Nne Lazima yawepo maghala na viwepo viwanda kwa ajili ya kuyapokea mazao haya kwa kila zao lichakwatwe na kupata by product, mfano kwa pamba tupate nguo hapa hapa nchini, kwa ngozi tupate viatu na mikanda, begi hapa hapa, matunda tupate juisi hapa hapa nk ili kuondoa post harvest loses.
Mbali na hayo Mwigulu Nchemba alisema kuwa tunahitaji kuwa na wataalam wa kutosha wa kilimo pamoja na vyuo imara vyenye kutoa wataalam makini na kuwa na vyuo vya utafiti ambavyo kazi yake kubwa itakuwa kufanya takwimu mbalimbali zenye kulenga tija katika kilimo chini.
"Tano Lazima tuwe na wataalam na uimara wa vyuo vya utafiti. Lazima wakulima walime kwa kufuata utaalam. Kwa Mifugo lazima tuwe na mitambo ya mifugo wa kisasa wa maziwa na nyama ili kupata tija kubwa kutokana na kundi dogo. Lazima tuwe na maeneo ya malisho ambayo mifugo itakaa kwa uwiano wa kitaalam huku na huduma kama maji, majosho na wataalam yakipatikana hapo katika ufuagaji wa kibiashara, " alisisitiza Mwigulu Nchemba.

LHRC serikali iweke mfumo wakutatua matatizo

Mkurugenzi wa LHRC Dkt. Hellen Kijo - Bisimba
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini Tanzania (LHRC) kimeitaka serikali kuweka mfumo maalum wa kushughulikia matatizo ndani ya nchi.
Mkurugenzi wa LHRC Dkt. Hellen Kijo-Bisimba ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na East Africa Television na East Africa na kuainisha kuwa ni lazima kuwe na mfumo maalum ambao utaweza kusaidia mambo yaende kwa kufuata sheria na Katiba ya nchi ilinavyoelekeza.

 
Amesema Rais Dkt John Pombe Magufuli ameanza kutekeleza mambo ambayo makundi ya kutetea haki za binaamu waliyapigania kwa miaka mingi na hayakuweza kutekelezwa kwa wakati huo kutokana na kuwepo kwa usimamizi mbovu kwa baadhi ya sekta mbalimbali nchini hivyo ni vema kuwa na uangalifu wa hali ya juu katika utekelezaji wake.

Amesema kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinamuunga mkono rais Dkt. Magufuli na kituo cha LHRC kina nia njema na wananchi wa Tanzania pamoja na serikali yake ndiyo maana kituo kimekuwa mstari wa mbele kusimamia haki itendeke kwa kuzingatia mfumo na utawala wa sheria ya nchi inavyoelekeza.

 
Kwa upande mwingine Dkt. Kijo - Bisimba amesema kitendo kinachofanywa na kambi ya upinzani Bungeni cha kutoka kwenye baadhi ya vikao vya Bunge ni aina mojawapo ya uwasilishwaji wa jambo fulani hivyo ni lazima wanasiasa watumie njia ya Kidemokrasia katika kuwatumikia wananchi wake.

China kushirikiana na Tanzania ujenzi reli ya kati

China imekubali kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli ya kati yenye urefu wa kilometa 2,561 kwa kiwango cha kisasa yaani "Standard Gauge" ambao zabuni za ujenzi zinatarajiwa kutangazwa hivi karibuni.
Balozi wa China hapa nchini Mheshimiwa Dkt. Lu Youqing ametoa kauli hiyo leo tarehe 25 Aprili, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambapo pia amemkabidhi barua yenye ujumbe kutoka kwa Rais wa China Mheshimiwa Xi Jinping.
Katika Mazungumzo hayo Rais Magufuli amemweleza Balozi Lu kuwa Tanzania imedhamiria kuanza ujenzi wa Reli ya kati haraka iwezekanavyo na tayari imetenga fedha kiasi cha shilingi Trilioni 1 katika bajeti yake ijayo kwa ajili ya kuanza awamu ya kwanza ya ujenzi huo.
"Tuna imani kuwa mradi huu utasaidia kuleta mapinduzi makubwa ya uchumi katika nchi yetu na katika nchi nyingine za Afrika Mashariki na kati zikiwemo Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ndio maana hatutaki kupoteza muda kwa mazungumzo marefu, tunataka kazi ianze na watu waanze kunufaika" Amesisitiza Rais Magufuli.
Kwa upande wake Balozi China hapa nchini Dkt. Lu Youqing amempongeza Rais Magufuli na serikali yake kwa kujiandaa kwa fedha, vifaa na rasilimali watu kwa ajili ya kutekeleza mradi huu mkubwa na kwamba Serikali ya China, Taasisi za fedha za China na Makampuni mbalimbali yatatoa ushirikiano wote katika utekelezaji wa mradi huu.

 
"Kama ambavyo Prof. Mbarawa amefanya mazungumzo na Serikali ya China, Taasisi za fedha za China na Makampuni, naahidi kuwa tutaanza kazi kama ambavyo taratibu na viwango vya ujenzi vimewekwa, tutafanya kazi kwa kujali muda, ubora na gharama nafuu" Amesema Balozi Lu.
Mradi mzima wa ujenzi wa reli ya kati unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani Bilioni 6.8 na umepangwa kutekelezwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa kilometa 1,216 za kutoka Dar es salaam - Tabora - Isaka - Mwanza na itajengwa kwa ushirikiano wa Tanzania na China.
Tayari Rais Magufuli amemtuma Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa Mnyaa kwenda nchini China kukamilisha mazungumzo juu ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo wa ujenzi wa reli ya kati, ambapo Prof. Mbarawa anasema hatua inayofuata sasa ni kutangaza zabuni ya ujenzi wa reli hiyo kwa uwazi, ili makampuni mbalimbali ya ujenzi yaombe na hatimaye kupata washindi watakaoanza kazi mara moja.

Sunday, April 24, 2016

RAIS MAGUFULI AWASHTUA WENGI,STAILI YAKE YA KUIBUKA MTAAANI YAWAPA HOFU KUBWA

Rais John Pombe Magufuli akiwasalimia walemavu.
 
DAR ES SALAAM: Staili inayotumiwa na Rais John Pombe Magufuli kuibuka katika maeneo mbalimbali mitaani pasipo kutarajiwa, inaonekana kuwashtua wengi huku wengine wakihoji juu ya usalama wake, Risasi Jumamosi linakupa zaidi.
Wakizungumza kwa njia ya simu kutoka maeneo mbalimbali nchini, wananchi wameonesha mshtuko wao, wakisema staili hiyo inaweza kuwapa nafasi maadui zake, waliodai ni wengi, kuweza kumdhuru kwa namna yoyote.
“Unajua utendaji kazi wa Magufuli umempatia maadui wengi na bahati mbaya, wabaya wake ni watu wenye uwezo wa kufanya lolote wakati wowote, sasa anapojitokeza katika maeneo ya wazi bila ya kuwepo ulinzi wa kutosha inatutisha sana, wanaweza kumdhuru hawa mafisadi,” alisema Theo Marson kutoka Arusha.
 
Mwananchi mwingine aliyepiga simu kutoka Morogoro, akijiita Mahsen, alisema ulinzi na usalama wa Magufuli unapaswa kuwa wa hali ya juu, kwani nchi inamhitaji katika mapambano dhidi ya ufisadi, nidhamu na uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa umma.

“Hii ibukaibuka yake uswahilini tuna wasiwasi ipo siku wajanja wanaweza kumdhuru, tunamuomba aache, wananchi tusingependa kuona jambo lolote baya linamtokea maana yeye ni mtu muhimu sana kwa Tanzania tunayoitaka, mtusaidie kuziambia mamlaka zinazohusika, ulinzi wake uimarishwe,” alisema Mary Jopel kutoka Mtwara.

Gazeti hili lilijaribu kuwasiliana na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Grayson Msigwa ili kupata ufafanuzi wa hofu hiyo ya wananchi, lakini baada ya kuomba aandikiwe ujumbe mfupi kupitia simu yake, hakuweza kutoa majibu hadi gazeti hili linakwenda mtamboni.

Tangu kuchaguliwa kwake, Rais Magufuli ameshaibuka sehemu tatu pasipo kutegemewa. Mara ya kwanza ilikuwa ni wakati alipotembelea ofisi za Hazina, akikatisha kwa miguu kutoka ikulu. Pia aliibuka ghafla katika Soko la Kimataifa la Feri jijini Dar es Salaam na kushirikiana na wananchi kufanya usafi.

Katika tukio la karibuni zaidi, wiki iliyopita Rais Magufuli aliibuka katika Tawi la Benki ya CRDB, Holland House, makutano ya mitaa ya Samora na Ohio, jijini Dar es Salaam akiwa katika gari la kiraia bila msafara kama ilivyozoeleka.

Mafanikio ya ziara ya wafanyabiashara wa Oman nchini


  MAFANIKIO YA ZIARA YA WAFANYABIASHARA WA OMAN NCHINI



Tanzania na Oman zimesaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano baina ya Tanzania Chambers of Commerce  na Oman Chambers of Commerce ili  kuanzisha Kampuni ya Oman Tanzania Investment (OTIC) kwa lengo la kutafuta fursa za uwekezaji zilizoko Tanzania na Oman.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Bibi. Mindi Kasiga  amesema kuwa mkataba huo ni matokeo ya ziara ya siku tatu ya Waziri Viwanda na biashara wa  Oman , Dkt. Ally Mohamed Al Sunaidy, pamoja na ujumbe wa wafanyabiashara 108 na maafisa wa Serikali ya Oman iliyofanyika nchini mwezi Aprili mwaka huu.

Amesema lengo la ziara hiyo lilikua kuwawezesha wafanyabishara wa Oman na Tanzania  kushiriki kongamamo la biashara la uwekezaji lililowawezesha wafanya bishara hao kubaini fursa za uwekezaji zilizoko nchini Tanzania na Oman.

Amesema tayari  Serikali ya Oman imeonesha nia ya kuwekeza katika kiwanda cha Sukari cha Kagera kilichopo mjini Morogoro ambacho  kitazalisha tani laki nne za sukari  itakayouzwa hapa nchini huku Tanzania ikitarajia kuzalisha  spiriti na hamira itakayouzwa nchini Oman pamoja na nchi za Mashariki ya kati.
‘’ Wafanyabishara wetu na wale wa Oman kupitia makubaliano haya watanufaika na fursa za uwekezaji kwa kupata mikopo mbalimbali na tayari mtaji wa Dola za Marekani milioni 25 zitatumika kwa wawekezaji hao’’ Amesema Bibi. Kasiga.

Aidha,amesema Wafanyabiashara  kutoka Oman tayari wameonesha nia ya kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo madini, viwanda na biashara, kilimo, utalii  pamoja na ujenzi wa nyumba za kisasa katika miji ya Dar es Salaam na Zanzibar.

Ameongeza kuwa uwekezaji  utaongeza  ajira akitoa mfano wa  kiwanda cha Sukari cha Kagera kitakachozalisha ajira 500 pamoja na kuongeza wigo wa soko.

Katika hatua  amesema kuwa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa itawapeleka watumishi 105 wa ngazi mbalimbali katika Balozi 35 zilizo katika nchi mbalimbali duniani  na kuwarudisha  nyumbani watumishi 79.

Bibi Mindi, ametaja sababu za kurudishwa kwa watumishi hao kuwa ni pamoja kuisha kwa muda wao wa kuhudumu nje ya nchi ambao ni miaka minne(tour on duty) pamoja, kustaafu na sababu mbalimbali.
Amezitaja Kada za watumishi wanaorudishwa nchini kuwa ni mabalozi, wahasibu, makatibu muhktasi na maofisa wa ngazi mbalimbali.

Hata hivyo, hadi kufikia sasa tayari mabalozi watatu wamerudishwa nchini ambao ni Balozi Peter Kalaghe aliyekuwa Uingereza, Balozi James Msekela aliyekuwa Italia na Balozi Batilda Burian aliyekuwa Japan kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe  Magufuli alilolitoa Januari 25, 2016 kuitaka wizara hiyo kuwarudisha nchini mabalozi waliomaliza muda wao wa kuhudumu ili wapangiwe kazi nyingine.

Mchakato wa ukusanyaji maoni ya uboreshaji sera ya Taifa ya TEHAMA Mkoani Mbeya

Wizara ya Ujenzi ,Uchukuzi na Mawasiliano  imetoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbalikuendelea kutoa maoni na mapendekezo ili yatumike kuboresha Sera mpya ya Taifa ya Habari  Teknologia ya Mawasiliano(TEHAMA) ya (2016) ili kuisaidia serikali kutatua changamoto za upatikanaji wa habari na mawasiliano katika jamii
 
Wito huo umetolewa jijini Mbeya  na Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia maswala ya simu katika Wizara ya Ujenzi ,Uchukuzi na Mawasiliano Ndugu John Mwera wakati wa zoezi la uchukuaji maoni lililofanyika katika viwanja vya chuo cha Uhasibu (TIA) jijini Mbeya

 Amesema Teknolojia ya habari na mawasiliano hapa nchini imekuwa ikikua kwa kasi kubwa katika kipindi cha miaka kumi tangu serikali ilipotunga sera kwa mara ya kwanza mwaka 2003.

 Amesema hali hiyo imechangia kuwepo kwa miundombinu ya huduma za mawasiliano   kila mahala  na kufanya matumizi kuwa makubwa ambapo Zaidi ya watu milioni 39 wanatumia mawasiliano ya simu hivyo kufanya kuibuka kwa changamoto mbalimbali katika sekta hiyo.

Amesema ili kufahamu changamoto wanazo kutananazo wananchi pamoja na mtizamo wao  katika utumiaji wa mawasiliano,  wizara hiyo imeamua kuweka utaratibu wa kuweka vituo vya kukuza ubunifu katika jamii katika kila mkoa ambapo kila mwananchi anakuwa huru katika kutoa maoni yao na ushauri ili kuisaidia serikali katika kupanga mikakati ya kuweza kuzitatua changomoto hizo.

“Huwezi kukaa ofisini ukatunga sera ambazo haziwahusu mwananchi wa kawaida hivyo lazima twende  kwa wananchi na kujua wanahitaji nini ili kutunga sera na kuweza kuzitatua”Alisema Mwela.

Aidha amesema kuwa kila maoni yanayotolewa na wananchi serikali inayathamini katika kuweza kutoa muelekeo wa sekta ya mawasiliano kwani sekta hiyo bado inamchango mkubwa sana katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.

Hata hivyo amesema bado wizara inakabiliwa na changamoto mbalimbali  ikiwa ni elimu ndogo kwa waanchi juu ya utunzaji wa miundombinu ya sekta ya mawasiliano hususani mkongo wa taifa

sanjali na wizi wa mafuta kwenye minara ya simu hivyo amewataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu hiyo ili kuendelea kukuza sekta hiyo sanjali na kulahisisha upatikanaji wa huduma kwa jamii. Amesema zoezi hilo la uchukuaji maoni kwa wananchi juu ya uboreshaji wa sera ya TEHAMA itaendelea inchi nzima katika mikoa yote ya Tanzania bara na Visiwani.

Mhandisi  Enock Mpenzwa Idara  Mawasiliano  toka Wizara ya Ujenzi ,Uchukuzi na Mawasiliano akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Forest jijini Mbeya waliofika kwa ajili ya zoezi la utoaji maoni na ushauri juu ya uboreshaji wa sera mpya ya Taifa ya TEHAMA katika viwanja vya Chuo Cha Uhasibu TIA jijini Mbeya April 22 ,2015.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Forest jijini Mbeya wakiwa katika foleni ya kujiandikisha ili kutoa maoni yao na ushauri juu ya uboreshaji wa sera ya Taifa ya TEHAMA,zoezi ambalo limefanyika katika viwanja vya Chuo Cha Uhasibu Mbeya (TIA) April 22 ,2015.
Mwanafunzi shule ya sekondari Forest jijini Mbeya Mariam Jordan akijiandikisha kwa ajili ya kutoa maoni yake katika zoezi la uboreshaji wa sera ya Taifa ya TEHAMA zoezi ambalo limeratibiwa na Wizara ya Ujenzi ,Uchukuzi na Mawasiliano ,katika viwanja vya Chuo Cha Uhasibu Jijini Mbeya( TIA)
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Cha Uhasibu Jijini (TIA)wakijibu baadhi ya Maswali kama sehemu ya ukusanyaji maoni ili kuboresha sera ya TEHAMA .
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Cha Uhasibu Jijini (TIA) na wadau mbalimbali kutoka Mkoani Mbeya wakijibu baadhi ya Maswali kama sehemu ya ukusanyaji maoni ili kuboresha sera ya TEHAMA .

Thursday, April 21, 2016

Tigo wakabidhi madawati 400 kwa wilaya ya Mwanga katika shule 8

Kampuni ya Tigo Tanzania imetoa msaada wa madawati 400 yenye thamani ya shilingi milioni 66 kwa shule nane za msingi katika manispaa ya Mwanga, mkoa wa Kilimanjaro, ikiwa ni mchango wa kampuni hiyo katika kuisaidia serikali kukabiliana na upungufu wa madawati katika shule za msingi nchini. 
 
Akizungumza leo katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika shule ya msingi Reli Juu katika manispaa ya Mwanga, Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Kaskazini George Lugata amesema mchango huo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya kampuni hiyo ya kuunga mkono jitihada mbalimbali za kuleta maendeleo nchini.
 
“Mchango huu ni sehemu ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Tigo katika kusaidia utekelezaji wa miradi yenye tija kubwa kwa jamii. Tunaamini kwamba kupitia msaada huu, Tigo inatoa mchango wake katika kujenga viongozi wa baadaye wa taifa hili na wanataluuma mbalimbali wakiwamo madaktari, wahandisi na wengineo, “amesema Lugata.

tigo 1
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Meck Sadiki akikabidhi madawati 400 yenye thamani ya shilingi milioni 66 kwa Mwenyekiti wa halmashauri ya Mwanga, Theresia Msuya yaliotolewa na Kampuni ya Tigo, Kulia ni Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Kaskazini George Lugata.

Lugata amesema mwaka jana Tigo ilikabidhi msaada kama huo wa madawati katika shule za msingi katika mikoa ya Shinyanga, Mbeya Iringa na Morogoro na kuongeza kwamba kampuni hiyo itaendelea kutoa madawati zaidi sehemu mbalimbali nchini siku za zijazo.

Makabidhiano yalihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro mheshimiwa Meck Sadiki ambaye alisema madawati hayo 400 yataboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto katika Mkoa wa Kilimanjaro na kutoa wito kwa wadau wengine kuunga mkono zoezi hilo.

tigo mwanga
 Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Meck Sadiki (Kulia), akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya  Mwanga Theresia Msuya (katikati) Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Kaskazini George Lugata.

 “Tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa kampuni ya Tigo kwa kuwa mdau muhimu kwetu katika jitihada zinazoendelea za kujaribu kupunguza tatizo la ukosefu wa madawati ya kutosha katika shule za msingi za mkoa wetu wa Kilimanjaro. Ni dhahiri kwamba msaada huu wa madawati 400 yatawawezesha mamia ya wanafunzi wetu kupata sehemu za kukaa na hivyo kujipatia elimu zao katika mazingira bora zaidi,” alisema Sadiki.

Madawati hayo yametolewa kwa shule za msingi nane kama ifuatavo, Mramba,Kawawa, Mwanga, Naweru,Kiboriloni, Lawate na Reli Juu.