Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Elimu, Clifford Tandari akishiriki kwenye kongamano la kujadili Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu (ESDP) |
Imekuwa
fasheni katika miaka ya karibuni watu kukosoana kwa asili zao, hali zao
za maisha, rangi , maumbile yao na hata aina ya elimu waliyonayo ama
waipatayo.
Si
tatizo watu kukosoana , bali wakosoane kwa hoja na hoja haziji kwa
hulka, mihemko ama mahaba na jambo jadiliwa bali hoja huja kwa ujuzi na
maarifa ambavyo ni zao la elimu.
Elimu ni nini?
Ukitaka
kujua maana ya neno elimu unaweza ukaja na majimbu mbalimbali kichwani
mwako ama kwenye vichwa vya watakao kupa hiyo maana.
Kwa
uelewa wangu elimu ni ujuzi ama stadi ambazo mtu ama kiumbe hujifunza
(kwa hiari ama lazima) ama hufunzwa ili kukabiliana na mazingira.
Viumbe hukabiliana na mazingira ili kuweza kuishi na kutengeneza maisha bora ya vizazi tarajiwa.
Kwa
binadamu elimu hutolewa /hupatikana kwa njia kuu mbili ile iliyorasmi
na isiyo rasmi.Mifumo isiyorasmi ilianza tangu zama za ujima ambapo
kupitia elimu moto ukapatikana, watu wakafuga, wakawinda na kufanya
mengi ambayo yamekuja kusaidia vizazi vilivyofuata na mifumo rasmi kwa
barani Afrika ililetwa kipindi bara hili lilipoanza kushirikiana na
jamii za mabara mengine kama Asia na Ulaya huku mashirika ya dini ya
kiisalam na kikristo.
Elimu
hii ya mfumo rasmi ambako kuna mitaala iliyoandikwa ndiyo iliyoleta
mbadiliko makubwa katika jamii nyingi za kiafrika.Hapo ndipo mgawanyo wa
kazi na matabaka yakatengenezwa na kuimarishwa badala ya matabaka kuwa
katika nyanja za uchumi na kisiasa pekee elimu hii iliongeza matabaka ya
waliosoma na wasiosoma kisha hata uchumi na siasa ukaanza kuingiliwa na
matabaka ya elimu.
Kwa
Tanganyika, elimu ya mfumo rasmi iliyoletwa na watangulizi wa wakoloni
ikatumika kipindi cha ukoloni hadi wakati wa azimio la Arusha.Elimu ile
iliyolenga kutoa ujuzi kidogo na kuandaa watumishi wa kuwatumikiwa
wakoloni na kuimarisha dola yao ,ilifanyiwa mageuzi kadhaa ambayo bado
madoa yake ni ngumu kufutika.
Baada
ya azimio la Arusha ikaonekana misingi bora ya kuifanya elimu kweli ni
njia ya kuifanya jamii iweze kukabili mazingira(kuyafanya mazingira kuwa
mahali pa kuishi na kupata mahitaji kiurahisi/maendeleo).
Ugunduzi
ulizingatiwa ,uzalendo na utamaduni pia , lakini baada ya miaka kadhaa
pale tulioingia kwenye ile mipango ya kimaendeleo ya kibepari (SAP na
mingine kama hii) hapo tukapoteza lengo na kujikuta tukitumbukia kwenye
ile elimu tuliyoikataa wakati tunaleta azimio la Arusha.
Mitaala
ikaanza kubadilishwa na wanasiasa walivyojisikia, shule tena haikuwa
mahali pa kupata uzalendo bali kuwagawanya watu katika matabaka ya
waliosoma na wasiosoma.Kuwa na elimu ikawa ni kufika sekondari ama chuo
kikuu na si shule ya msingi na VETA.
Baadaye zikaanzishwa shule zilizokuwa na mlengo wa kijamaa (shule za kata) na zikaanza kufanya kazi ya kibepari.
Hapo
ndipo ujanja wa kisasa ulipoanza, tuliobahatika kusoma shule hizo
tukakosa ujanja, usichangie sehemu utaambiwa ulisoma shule za kata,
hamna kitu ni kayumba nyie hamjui kiingereza sayansi hamuijui wazee wa
zero na mengine mengi hapo ujanja ni kutosoma shule za kata wakijua
umesoma huko una hatari.
Walioanzisha
shule za kata na walioanza kutoa mawazo haya ni wale ambao ama walipata
elimu ya kikoloni ama ya kijamaa sasa tumlaumu nani aliyesoma shule za
kata ama aliyeanzisha shule za kata kwa kujua ama kutojua ili kuleta
matabaka.Shule zilizoitwa za vipaji maalum hazikutosha kupokea wanafunzi
wote walifahulu kukahitajika mbadala lakini hawa wasomi wa zamani
wakatuletea mbadala usiokamilika na madaraja yakaongezeka.
Nitawaambia
wanangu kuwa sikutoka kapa kusoma shule za kata japo tulionekana
masikini na wasio na akili nilipata ujuzi ambao ulinifanya nikaishi
maisha bora pengine kuwazidi wale waliojiona bora, shule za kata ndizo
zilizokuwa daraja nikafika kidato cha tano na chuo kikuu ambako
nikakutana na wajanja wa shule za matajiri wanaoongea kiingereza kama
malkia lakini wana ujuzi sawa , zaidi ama kidogo kuliko ujuzi nilionao.
Hao
ndio niliowahi kuwapa akili ya kupika wali na chai na kukifanya chakula
cha jioni nilipowakuta wakilia hawana mboga huku wana mchele na sukari
ndani kifupi walishindwa kupambana na mazingira licha ya ujanja wao.
No comments:
Post a Comment