Lwakatare akamatwa
Mh. Wilfred Lwakatare
JESHI la Polisi nchini limemkamata Mkurugenzi wa Ulinzi na
Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred
Lwakatare, kwa tuhuma za kuhusika na matukio ya mashambulizi dhidi ya
watu hapa nchini.
Taarifa kutoka Ofisi za Makao Makuu ya CHADEMA Kinondoni jijini Dar
es Salaam zilieleza kwamba Lwakatare alikamatwa saa 7 mchana na watu
wanne waliojitambulisha kama maofisa wa Jeshi la Polisi ambao walifika
na gari aina ya Toyota Land Cruiser jeupe lenye namba za usajili T 140
BLA likiwa na chata ya kitalii.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, alisema Lwakatare amekamatwa kwa tuhuma zilizosambazwa kwenye mtandao.
Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Zanzibar, Hamad Yusufu Musa, ambaye
alishuhudia tukio la kukamatwa kwake, aliliambia Tanzania Daima kuwa
kiongozi huyo anatuhumiwa kupanga njama za matukio ya kushambulia raia
yaliyotokea hapa nchini.
Hata hivyo Musa hakusema ni matukio gani yanayomhusisha kigogo huyo,
lakini mtu aliyesambaza mkanda wa video katika mitandao ya kijamii jana
aliandika chini yake maneno yasemayo: ‘Mikakati ya mateso ya Kibanda
na mwandishi mwandamizi wa gazeti la Mwananchi, mhusika mkuu huyu
hapa.’ akimaanisha Lwakatare.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk.
Willibrod Slaa, alisema kukamatwa kwa Lwakatare na kuhusishwa na
matendo hayo ya utekaji na kushambulia watu, kumedhihirisha kuwapo kwa
njama chafu zenye lengo la kukichafua chama hicho mbele ya jamii.
Dk. Slaa alisema njama hizo zinaratibiwa na kigogo mmoja serikalini
ambaye analitumia Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola
kuidhoofisha CHADEMA.
“Ikiwa ni kweli wanamshikilia kutokana na hiyo video, ni furaha
kwetu, kwa sababu ukombozi wa nchi umekaribia,” alisema bila kufafanua.
Hata hivyo Dk. Slaa alisema ameshangazwa na uharaka wa polisi wa
kumkamata Lwakatare siku moja tu baada ya video hiyo kuwekwa mtandaoni,
na kuacha hata kumhoji mmoja wa mawaziri aliyetajwa na baadhi ya
magazeti jana akihusishwa kutekwa na kuteswa kwa Kibanda.
“Waziri hajakamatwa wala kuhojiwa, alitekwa Ulimboka akamtaja ofisa
wa Ikulu, lakini hajakamatwa wala kuitishwa gwaride la utambulisho.
“Aliuawa kinyama Mwangosi (Daudi Mwangosi), katikati ya kundi la
maofisa wa polisi na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, lakini hakuna
aliyechukuliwa hatua. Lakini kwa video ambayo haijulikani asili yake,
polisi wameharakisha kumkamata na kumpekua nyumbani kwake, kulikoni?”
alihoji Dk. Slaa.
Alisema ni wazi kwamba sasa lazima Watanzania wafumbue macho na wajue
ukweli ulivyo na namna polisi wanavyotumika kuiangamiza CHADEMA,
lakini akadai kuwa ukweli utajulikana muda si mrefu.
Wakili wa Lwakatare, Nyaronyo Kicheere, akizungumza na gazeti hili,
alisema mteja wake majira ya saa 10 alikwenda kupekuliwa nyumbani kwake
Kimara.
“Kwa sasa tumeshafika nyumbani kwa Lwakatare Kimara King’ong’o na
maofisa wapatao saba wanaendelea na upekuzi katika nyumba yake,”
alisema mwanasheria huyo.
No comments:
Post a Comment