Mnara ukiwaka moto baada ya gesi kufunguliwa kutoka kisimani (MB3) Mnazi Bay, hivi karibuni.
KATIKA siku za hivi karibuni, kumekuwapo mjadala katika jamii nchini
juu ya uwepo wa gesi inayozalishwa kwa sasa, ambapo baadhi ya wananchi
walijikuta wakiaminishwa kuwa hakuna gesi inayozalishwa kabisa na
wengine wakisema gesi inayozalishwa ipo, lakini ni kidogo.
Mjadala huo ulisambaa zaidi wakati wa majaribio ya mtambo wa kufua
umeme wa Kinyerezi jijini Dar es Salaam, baada ya kuibuka taarifa potofu
iliyosambaa mitandaoni kwamba upatikanaji wa gesi asilia ni mdogo
kuliko uwezo wa mitambo ya ufuaji umeme. Lakini ukweli wa mambo ni
kwamba Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), limekuwa
likizalisha gesi asilia ya Mnazi Bay mkoani Mtwara na Songo Songo mkoani
Lindi, ambayo ni nyingi kuliko mahitaji.
Akizungumza na mwandishi wa makala haya hivi karibuni, Mkurugenzi
Mtendaji wa TPDC, Dk James Mataragio, alisema kiasi cha gesi
kinachopatikana kwa sasa katika maeneo hayo ni jumla ya futi za ujazo
milioni 240 za gesi asilia kwa siku. Kiasi hicho cha gesi, ni tofauti na
gesi iliyogunduliwa kuanzia Mwaka 2010 katika Bahari Kuu, ambayo hadi
kufikia Juni 2015, jumla ya kiasi cha gesi kilichogunduliwa huko
baharini pamoja na kilichogunduliwa nchi kavu kilifikia takribani futi
za ujazo trilioni 55.24.
Kwa mujibu wa Dk Mataragio, matumizi ya nchi mpaka sasa ni futi za
ujazo milioni 140 za gesi asilia tu kwa siku, hivyo kuwa na ziada ya
takribani futi za ujazo milioni 100 kwa siku ambazo zinapatikana Songo
Songo na Mnazi Bay katika mikoa ya Lindi na Mtwara. Historia ya gesi
hiyo Ni vyema kufahamu kwamba utafutaji wa mafuta na gesi asilia hapa
nchini, ulianza mwanzoni mwa miaka ya 1950 wakati wa Ukoloni na gesi
hiyo asilia, iligunduliwa kwa mara ya kwanza kisiwani Songo Songo mwaka
1974.
Pamoja na ugunduzi huo, utafutaji uliendelea kufanywa na Kampuni ya
Agip ya Italia, ambapo baadaye mwaka 1982, gesi zaidi ikagundulika Mnazi
Bay, mkoani Mtwara. Hata hivyo, kampuni hiyo ya Agip ya Italia,
haikuona umuhimu wa kuanza kuvuna gesi hiyo, kwa kuwa ilionekana kuwa
iko kidogo na hivyo isingekuwa na tija, ikilinganishwa na gharama ambazo
zingehitajika katika kuwekeza mitambo ya uvunaji wake.
Taarifa zinaonesha kuwa, Serikali haikukata tamaa hivyo ikaipatia
TPDC jukumu la kuendeleza utafiti wa rasilimali hiyo kwenye maeneo
yaliyoachwa na kampuni hiyo kutoka Italia. Matokeo ya shughuli za TPDC
yakazaa matunda, ambapo inaelezwa kuwa ugunduzi wa gesi zaidi ulifanyika
baada ya kuchimba visima vya uendelezaji huko Songo Songo na baadaye
Mnazi Bay.
Kutokana na ugunduzi huo, Serikali ikaanza kujenga miundombinu ya
kuchakata na kusafirisha gesi, ambapo Oktoba 2004, matumizi ya gesi
kutoka Songo Songo yakaanza kuzalisha nishati nchini na kufuatiwa na
matumizi ya gesi asilia kutoka Mnazi Bay yaliyoanza mwaka 2006.
Changamoto Taarifa za TPDC, zinaonesha kuwa ugunduzi wa gesi zaidi huko
Songo Songo na Mnazi Bay, uliendelea hivyo miaka minne tu tangu kuanza
kutumika kwa gesi kutoka maeneo hayo, miundombinu ya kuchakata na
kusafirishia gesi hiyo, ikashindwa kuhimili wingi wa gesi kutokana na
udogo wake.
Kutokana na changamoto hiyo, Serikali ikalazimika kujenga miundombinu
mikubwa zaidi ili kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya kuchakata
na kusafirisha gesi, ambapo kukajengwa mtambo mkubwa wa kuchakata gesi
katika kijiji cha Madimba, mkoani Mtwara na bomba kubwa kutoka Mtwara na
Lindi kwenda Kinyerezi Dar es Salaam, katika mitambo ya kufua umeme.
Ugunduzi zaidi, uhakika Akielezea uhakika wa gesi ya Mnazi Bay, Dk
Mataragio anasema Agosti mwaka huu walishuhudia uzalishwaji wa mara ya
kwanza wa gesi katika kisima cha “MB-3” huko Mnazi Bay mkoani Mtwara.
Anasema ilikuwa furaha kuanza kuzalisha gesi asilia ya Mnazi Bay katika
kisima hicho, ambayo itaenda kuchakatwa katika mitambo iliyoko Madimba
na kisha kusafirishwa hadi Kinyerezi jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya
matumizi mbalimbali.
Kwa mujibu wa Dk Mataragio, kisima hicho kipya cha “MB-3” kina uwezo
wa kuzalisha gesi asilia takribani futi za ujazo milioni 20 hadi 30 kwa
siku. Dk Mataragio anasema mwezi huo huo wa Agosti kulikuwa na matarajio
ya kuunganisha visima vingine kwa ajili ya kutoa gesi kutoka Mnazi Bay,
ikiwemo kisima namba MX-1, MB-2, MB-4, na MB-1 ambavyo vitasababisha
uzalishaji wa gesi asilia kutoka Mnazi Bay kufikia futi za ujazo milioni
130 kwa siku eneo hilo la Mnazi Bay pekee.
“Baadhi ya Watanzania walikuwa hawaamini kama tungefikia siku ambayo
tungeingiza gesi kwenye bomba na kuzalisha umeme kwa kutumia gesi
asilia,” anasema Dk Mataragio. Hali ya uzalisha kwa sasa Dk Mataragio
anafafanua kuwa jumla ya visima vinavyopatikana Songosongo ni vitano,
ambavyo ni SS-4, SS-5, SS-9, SS-10 na SS-11 na vina uwezo wa kuzalisha
jumla ya futi za ujazo milioni 150 za gesi asilia.
Pamoja na uwezo huo, lakini Dk Mataragio anasema mpaka sasa ni futi
za ujazo milioni 96 tu za gesi asilia kwa siku ndio zinazozalishwa
kutokana na mahitaji, huku kukiwa na ziada ya futi za ujazo milioni 54
za gesi asilia kwa siku. Anafafanua kwamba upande wa Mnazi Bay mkoani
Mtwara, futi za ujazo za gesi asilia zinazozalishwa ni milioni 90 kwa
siku, huku futi za ujazo milioni 43 za gesi asilia kwa siku zikiwa
ziada.
Matumizi ya Mtwara Kudhihirisha udogo wa matumizi ya gesi kwa sasa,
Dk Mataragio anasema; “licha ya mikoa ya Lindi na Mtwara kutumia umeme
unaozalishwa kwa gesi asilia, lakini mikoa hiyo inatumia futi za ujazo
milioni mbili pekee za gesi asilia kufua umeme kwa siku na kuacha ziada
ya futi za ujazo milioni 8 za gesi asilia kwa siku zinazotoka katika
kisima kimoja tu cha MB1, kilichopo Mnazi Bay.”
Dk Mtaragio anasema ziada inasubiri ongezeko la uhitaji wa gesi hiyo
na kuongeza kuwa ziada hiyo inatarajiwa kuzalisha umeme kwa kiasi
kikubwa zaidi. “Niwatoe hofu Watanzania kwa kuwahakikishia uwepo wa gesi
asilia ya kutosha nchini,” anaeleza Dk Mtaragio na kuongeza kuwa gesi
asilia ya ziada iliyopo Mnazi Bay na Songo Songo ikitumika yote futi za
ujazo takribani milioni 100 kwa siku, zina uwezo wa kuzalisha nusu ya
umeme wote unaopatika nchini kwa sasa.
Dk Mataragio anasema kwa kuwa TPDC ina dhamana ya usimamizi wa
masuala ya mafuta na gesi asilia pamoja na upatikanaji wa gesi hiyo.
Anasema shirika hilo litaendeleza jitihada za kuendeleza maeneo ambayo
yamekwishagunduliwa kuwa na gesi asilia, ili kufikia hatua ya
uzalishaji. “Novemba mwaka huu, TPDC imeendesha utafiti wa awali kwa
kutumia ndege maalumu inayoainisha maeneo yanayoweza kuwa na mafuta au
gesi asilia siku za usoni hususan maeneo yaliyopitiwa na Bonde la Ufa,”
anasema Dk Mataragio.
Mkurugenzi huyo ameainisha maeneo hayo kuwa ni Kitalu cha Ziwa
Tanganyika, Kitalu cha Eyasi Wembere na Mandawa, ambako utafiti huo
unatarajiwa kukamilika Januari mwakani na mikoa itakayohusika na vitalu
hivyo ni Arusha, Singida, Shinyanga, Simiyu, Tabora na Lindi.
No comments:
Post a Comment