Meneja Uhusiano wa Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud
KAMPUNI ya madini ya Tanzanite One imetoa likizo ya malipo kwa
wafanyakazi 635 kwa lengo la kujiweka sawa katika shughuli za uendeshaji
wa kampuni hiyo. Wafanyakazi hao wamepewa likizo ya malipo kuanzia jana
huku mchakato wa kuwaachisha kazi baadhi ya wafanyakazi ukiendelea kwa
kuhusisha pande zote.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Meneja wa Kampuni
hiyo, Apolinari Modest alisema kwa sasa uongozi wa kampuni hiyo tayari
ulishafuata taratibu zote za kuachisha kazi wafanyakazi.
Modest alisema hakuna mfanyakazi atakayeachishwa bila ya kufuata
sheria na taratibu za kazi kwani uongozi umezingatia kila kitu na
kuwataka wafanyakazi kuacha kuwa na wasiwasi juu ya hilo.
Alisema mchakato wa kupunguza wafanyakazi umetokana na kampuni
kushindwa kujiendesha kutokana na kukosekana kwa uzalishaji kwa muda
mrefu na gharama za uendeshaji kuwa kubwa.
Alisema kwa sasa kazi ya kuchambua wafanyakazi wa kuachishwa iko
katika vikao mbalimbali kwa kuhusisha uongozi wa Kampuni ya Tanzanite
One, viongozi wa vyama vya wafanyakazi tawi la kiwandani hapo na uongozi
wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).
Naye Mwanasheria wa Tanzanite One, Kisaka Mnzava alisema kuachishwa
kazi kwa wafanyakazi kutafuata sheria zote za kazi na zitasimamiwa na
pande zote na hakuna mfanyakazi atayeachishwa bila kufuata sheria za
nchini.
Alisema kupunguzwa kazi kwa wafanyakazi sio mchakato mgeni katika
kampuni hiyo kwani ulishafanyika na hakukuwa na malalamiko yoyote.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Tawi la Tanzanite One, Daniel Hagay
alikiri kuwepo kwa mchakato wa kupunguza wafanyakazi, lakini alikuwa na
wasiwasi juu ya taratibu kukiukwa, hivyo kuutaka uongozi kukamilisha
kwanza taratibu za kuachisha wafanyakazi ili kila mfanyakazi
atayeachishwa awe na haki yake ya msingi.
Akithibitisha hilo, Mkurugenzi wa Sky Group, Faisal Shahbhai alisema
kupunguzwa kwa wafanyakazi ni kutokana na gharama za uendeshaji kuwa
kubwa kuliko uzalishaji hivyo kushindwa kutekeleza baadhi ya ahadi
walizoahidi kabla ya kuchukua kitalu hicho C katika mgodi wa Tanzanite
Mirerani wilayani Simanjiro, Manyara.
Alisema mchakato mzima wa upunguzaji wa wafanyakazi utafuata taratibu
na sheria za kazi ikiwamo kushirikisha pande zote ikiwemo Stamico,
mwakilishi wa serikali kama mbia na viongozi wa wafanyakazi.
Alisema Sky Group imekuwa ikifanya kazi katika mazingira magumu tangu
ichukue kitalu hicho C kilichokuwa kikimilikiwa na Tanzanite One
kutokana na kukosa uzalishaji kwa muda mrefu, lakini pia imekuwa na
madeni makubwa ya nyuma.
No comments:
Post a Comment