TTCL

EQUITY

Wednesday, December 2, 2015

Mabalozi nchi mbalimbali wateta na Majaliwa


 


  
Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akizungumza na balozi wa Sudan nchini, Dk Yassir Mohamed Ali ofisini kwake Dar es Salaam jana. 
 

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na mabalozi watatu kutoka nchi za China, Jamhuri ya Sudan na Korea Kusini. Akizungumza kwa nyakati tofauti na mabalozi hao jana mchana ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu aliwashukuru mabalozi hao kwa pongezi walizokwenda kumpatia na kuahidi ushirikiano zaidi na nchi zao.
Kwa upande wake, Balozi wa China, Dk Lu Youqing alisema Serikali itaendelea kuisaidia Tanzania kwenye sekta za uendelezaji viwanda, miundombinu, maji, afya na elimu, ikiwa ni ishara kuendeleza mahusiano ambayo yamekuwepo kwa muda mrefu baina ya China na Tanzania.
Alisema Tanzania imeteuliwa kuwa miongoni mwa nchi tatu zitakazosaidiwa na China kuendeleza viwanda na kwamba makubaliano ya mpango huo yatafikiwa kwenye Mkutano wa Ushirikiano baina ya China na Nchi za Afrika (FOCAC - 6) unaotarajiwa kuanza Desemba 4, mwaka huu Johannesburg, Afrika Kusini.
Nchi nyingine mbili zitakazonufaika na mpango huo ni Kenya na Ethiopia. Balozi wa Jamhuri ya Sudan, Dk Yassir Mohamed Ali alisema nchi yake inao madaktari wengi na kwamba kumekuwa na majadiliano ya kuona ni jinsi gani wanaweza kuja kuongeza nguvu kwenye sekta ya afya.
“Tuna madaktari wasiopungua 4,000 ambao wanahitimu kila mwaka na tungependa kushirikiana na Tanzania katika eneo hili,” alisema Dk Ali. Kwa upande wake, Balozi wa Korea Kusini, Chung Il ambaye pia alitumia fursa hiyo kuagana na Waziri Mkuu Majaliwa, alisema anatumaini kuona ubalozi wa Tanzania ukifunguliwa nchini mwao katika muda siyo mrefu.

No comments:

Post a Comment