TTCL

EQUITY

Thursday, December 3, 2015

Wenye ulemavu wanaweza kutumiwa kukuza ajira

 
“INAWEZEKANA kujiajiri kwa mtu mwenye ulemavu hasa wa viungo, ingawa kuna changamoto nyingi kutokana na hali halisi ya kimaumbile, pamoja na kutokuwa na mtandao wa watu wenye fedha wanaoweza kutoa mitaji ili angalau mwenye ulemavu aanzishe shughuli itakayomuingizia kipato...”. “Kwa ufupi, ulemavu si umasikini.
Inawezekana mtu mwenye ulemavu akajiajiri au kuajiriwa na kufanya kazi yenye matokeo mazuri kama yanayoletwa na mtu mwingine yeyote asiye na ulemavu. Jambo kubwa linalopaswa kutazamwa ni namna atakavyopata mtaji ajiajiri. Kuwa mlemavu wa viungo haimaanishi kuwa ni kukosa uwezo wa kufanya kazi”.
Mjumbe wa Chama cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) wilayani Kahama, Edward Charles ndiye anayesema maneno hayo na kuweka wazi kuwa, watu wengi wenye ulemavu hasa wa viungo wanakuwa wamejaaliwa maarifa ya aina mbalimbali yanayohitaji kutumiwa kwa njia tofauti ili mchango wao katika nchi uwe na manufaa kwa wengine.
Anasema, lakini kutokana na kukosa uwezo wa mitaji, wanashindwa kutumia maarifa yao ipasavyo hivyo kujikuta wakipoteza muda kutaka wasaidiwe kwa kuomba omba, kana kwamba maisha ya kujishughulisha na kujitengenezea ajira au kuajiriwa hayapo katika upande wao. Charles ni mlemavu wa miguu anayejishughulisha na ushonaji na ung’arishaji viatu katika wilaya ya Kahama.
Anasema wenye ulemavu wa viungo wanaweza pia kufanya kazi, kutegemea na aina ya ulemavu wa viungo walio nao. Kwa mujibu wake, mbali na kufikiria kuajiriwa serikalini au kwenye mashirika ya umma na binafsi, watu wenye ulemavu ambao wana vipaji na maarifa ya aina mbalimbali, wanaona ni vema kuchangia kuzalisha ajira kwa kutumia vipaji na uwezo wao wa maarifa.
Anasema, kuona kwa watu wenye ulemavu kuwa ni vema kuchangia kukuza ajira na kipato kunaweza kufikia hatua ya utekelezaji, ikiwa watawezeshwa zaidi kuwa na kianzio, yaani mitaji itakayowawezesha kuanzisha shughuli wanazoweza kuzisimamia na kuziendeleza kwa kuajiri watu wengi zaidi wenye ulemavu na wasio na ulemavu, huku wakijipatia kipato.
Anasema, “Uwezo tunao na nia ya kushiriki kukuza ajira nchini tunayo. Chabmsingi ni Serikali kutuwezesha zaidi mitaji ili tuweze kuichanganya na maarifa na ubunifu wetu kuanzisha kitu kikubwa kitakachowafanya vijana wengi wajishughulishe na si kubweteka au kukimbilia mijini kuendekeza kuombaomba”.
“Kwa mlemavu yeyote mwenye maarifa na mtaji suala la kusimama barabarani kuomba au kubweteka na kusubiri kuletewa ni fedheha. Lakini kwa anayelilia mtaji na kujihakikishia malengo ya kuendeleza shughuli atakayoianzisha kwa ajili yake na wengine ndani ya nchi yake ni ujasiri, hivyo ni vema ukaungwa mkono,”anasema. Funzo analotoa Charles anasema kuwa hakufikiria kubweteka ingawa hakuwa na mtaji mkubwa.
“Nilijikusanya na kuwekeza kiasi kidogo nilichokuwa nacho na kuanzisha biashara ya kung’arisha viatu ambayo kwa kiais fulani inamwezesha kuendeleza maisha yake,” anasema.
Kutokana na maelezo yake, chama chao kinafanya juu chini kuhakikisha wanapata mafunzo ya ujasiriamali kuepusha wasitawaliwe na mawazo ya kubweteka kwa kutegemea kupewa misaada ya hapa na pale, bali kuwaandaa wawe na fikra ya kuanzisha miradi ya maendeleo itakaowawezesha kuinua vipato vyao kwa kipindi kirefu.
“Mtu akikupa mtaji anakuwa amekutoa kimaisha tofauti na atakayekusaidia chakula leo na kesho na kuenda zake. Anayekupa mtaji anakuwa amekufungulia mlango wa kujipatia kipato na anayekupa mlo wa siku anakuwa amekusaidia, lakini msaada huo unaweza kukudumaza na kukufanya usifikirie kujiendeleza,” anaeleza.
Vijiweni Charles anawaonya watu wenye ulemavu wanaopoteza muda kukaa vijiweni wakijadili mambo yasiyo na maendeleo, kuacha kufanya hivyo na badala yake wafuate nyayo za wengine waliojiunga na vikundi vya ujasiriamali kutengeneza nguvu itakayowawezesha kujiajiri.
“Walemavu hapa Kahama hatupo wengi sana kiasi cha kushindwa kuwezeshwa mitaji na kuanzisha miradi. Tuna uwezo wa maarifa ya aina tofauti hivyo ni vizuri tukawepo pamoja na kufikiria ni nini tufanye ili Serikali itutazame zaidi kwa upande wa mitaji”, anasema.
Anaongeza kuwa, Mungu hamnyimi mtu kila kitu ndio maana unakuta mlemavu wa viungo iwe kwa sababu ya kuzaliwa na ulemavu au ajali, anakuwa na namna mbadala ya kufanya jambo ambalo mtu asiye na ulemavu analifanya.
Kinachokuwa kigumu ni kianzio tu (mtaji). Kwa walemavu waliosoma, amewashauri wasikubali kubweteka bali watumie elimu yao hata kutoa ushauri kwa walemavu wengine ili, pamoja na kuwanufaisha kwa kupanua mawazo yao kwa njia ambayo ni chanya zaidi, wasidumaze yao. Ombi kwa Serikali Anaiomba Serikali iendelee kuwatazama kwa jicho la karibu watu wenye ulemavu kwa kuwarahisishia mazingira ya kupata mitaji kutoka katika taasisi zake za fedha kwa kuwa wengi wao hawana dhamana inayoweza kukubaliwa na taasisi hizo.
Anasema, Serikali ya CCM imekuwa ikitukumbuka kwa njia mbalimbali, hasa kupitia wenzao walioko katika miji mikubwa kama vile Dar es salaam ambapo waliobahatika kupata vyombo vya usafiri zikiwemo bajaj wameruhusiwa kuendesha biashara ya usafirishaji katika maeneo ambayo wengine hawaruhusiwi. Kwa kufanya hivyo, imewatengenezea fursa nzuri ya kujiingizia kipato bila kushindanishwa na wasio na ulemavu.
“Sasa changamoto imebaki kwetu sisi tulio nje ya miji mikubwa, kwa sababu mitaji yetu ni midogo sana. Mwenye biashara inayoonekana kuwa kubwa ni pamoja na anayejishughulisha kama mimi hapa kwa kushona viatu, lakini ukiangalia hali halisi tunachokizalisha kwa mtaji huo mdogo hakitoshi na wala hatuzalishi ajira kama tunavyotaka,” anasema.
Anaeleza kuwa kuna mashirika yasiyo ya Serikali yanayojitoa kusaidia watu kwa kuangalia matabaka yao, jambo linalowafanya wenye ulemavu kushindwa kufikiwa. Kutokana na hilo, anaiomba Serikali iwaondoe katika fedheha ya kuachwa nyuma na mashirika ya aina hiyo kwa kuitengenezea jinsi ya kupata mitaji wajikwamue na kuwezesha wengine wengi zaidi kushiriki ajira katika miradi ya ujasiriamali watakayoianzisha.
“Kuna fedha za Serikali asilimia tano inayotolewa kwa kundi la vijana kupitia Halmashauri za Wilaya ili ziwawezeshe katika shughuli za maendeleo, sisi walemavu vijana wa Kahama hatujui lolote kuhusu fedha hizo hivyo tunaziomba mamlaka husika zitufikirie angalau katika awamu ya Tano ya uongozi wa Dk Magufuli zitufikie,” anasema.
Zaidi, anaeleza kuwa ikiwa watapata mgawo katika fungu hilo, watu wenye ulemavu katika eneo lao wataweza kufanya mambo ya msingi yatakayonufaisha wengi na si wao pekee. Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu wenye Ulemavu mkoani Shinyanga (SHIVYAWATA), Michael Nkanjiwa anasema wanamshuku Rais John Magufuli kwa kutoa kibali cha kufanya sherehe siku ya Walemavu kitaifa mkoani Mwanza, akiamini kuwa itachangia wengi kuhamasika kuwakumbuka watu wa kundi hilo.
“Tuna imani na Rais Magufuli kutokana na kauli alizozitoa wakati wa kampeni zake za urais. nakumbuka aliahidi kutowabagua watu wenye ulemavu kwa hiyo imani yetu imesimama katika kuona hilo linatokea,” anasema.
Anaeleza kuwa, jambo la muhimu wanalomuomba ni kuwaondolea imani mbaya wakopeshaji hasa taasisi za fedha kuwa watu wenye ulemavu si walipaji wa mikopo, kwa kuwapa taarifa sahihi za wanaoirejesha. “Tunaonekana ni wa kushindwa kurejesha mikopo, lakini ukweli ni kwamba nasi tunaweza kuilipa ikiwa masharti yatafanywa kuwa rahisi kulingana na hali zetu. Si kweli kuwa hatuwezi”.

No comments:

Post a Comment