TTCL

EQUITY

Monday, February 27, 2017

Philip Bilden akataa kuchukua wadhifa baada ya kuteuliwa na Trump

media Philip Bilden, mteuliwa wa Rais Donald Trump akataa kuchukua wadhifa. REUTERS/Carlos Barria
Rais wa Marekani Donald Trump, amemteua Philip Bilden kujaza wadhfa wa waziri wa jeshi la wanamaji lakini muda mchache baadaye afisa huyo amekataa kuchukua wadhifa huo baada ya kuonekana kukiuka sheria za taifa kuhusu mgongano wa maslahi.
Philip Bilden ni mtu wa pili kuteuliwa na Rais Trump na kukataa kuchukua wadhifa. Mapema Mwezi huu mteuliwa wa Rais Trump aliyependekezwa kusimamia jeshi la Marekani alijiondoa kwenye wadhifa huo.
Philip Bilden ameeleza wasiwasi wake kuhusu maisha yake ya usiri na changamoto alizokumbana nazo katika kujitenganisha na biashara zake.
Hata hivyo Waziri wa usalama, Jim Mattis, amesema atampendekeza mtu atakayechukua nafasi ya Bilden katika kipindi cha siku chache zijazo.
Rais Donald Trump ameendelea kukukabiliwa na hali ya sintofahamu na kukosolewa ndani na nje ya nchi ya Marekani kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya wahamiaji hasa raia wa kigeni waishio nchini Marekani.

Thursday, February 16, 2017

Sirro: Tumekamata Watuhumiwa 349 wa Unga na Anayesambaza Majina ya Viongozi Kuwa Wanatumia Madawa

Kamanda Sirro akizungumza na wanahabari leo
 Leo Februari 16, 207 Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa taarifa ya kukamatwa kwa jumla watuhumiwa 349 katika oparesheni ya kuwasaka watu wanaohusika na dawa za kulevya.
 
 
Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro amesema kati ya watuhumiwa hao wamo wauzaji, wasafirishaji na watumiaji wa dawa za kulevya, na kwamba Wataanza kufikishwa mahakamani siku ya kesho, huku mmoja akipandishwa kizimbani leo.
 
Pia ametoa taarifa ya kijana mmoja anayedaiwa kusambaza taarifa za uongo, ambapo amesema kuwa jeshi hilo linamshikilia kijana huyo ambaye ni mwanafunzi mwenye umri wa miaka 23, anayedaiwa kutaja majina ya viongozi na kuwatuhumu kuwa wanahusika na dawa za kulevya.

Kuhusu askari 9 waliotuhumiwa kuhusika na dawa hizo, Kamanda Sirro amesema askari hao wamekabidhiwa kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
 
Kamanda Sirro amesema hadi sasa jumla ya kete 612 pamoja na bangi vimekamatwa na kwamba kuna watu wengine 17 ambao bado jeshi hilo linawafuatilia na watakuwa mbaroni wakati wowote.

Kijanaanayedaiwa kutaja majina feki ya vigogo watumia unga.

Wednesday, February 15, 2017

Watanzania 132 wafurushwa nchini Msumbiji

Maputo nchini Msumbiji
Maputo nchini Msumbiji
Takriban raia 132 wa Tanzania wanaoishi nchini Msumbiji wamefurushwa nchini humo huku wengine wasiojulikana wakidaiwa kukamatwa kufuatia operesheni ilioanzishwa na serikali ya taifa hilo.
Kulingana na serikali ya Msumbiji operesheni hiyo inalenga kuwatimua raia wa kigeni wanaoishi nchini humo kinyume cha sheria.
Taarifa ya wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika mashariki nchini Tanzania imesema kuwa raia waliofukuzwa ama hata kukamatwa ni wale wanaoishi mji wa Monte Puez kwa kuwa una raia wengi wa kigeni ikilinganishwa na miji mingine.
Kulingana na taarifa hiyo tayari ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji unaendelea kufanya mawasiliano ya kidiplomasia na serikali ya Msumbiji ili kuwahakikishia usalama raia wa Tanzania na mali yao nchini humo.
Inakadiriwa kuwa, Watanzania wapatao elfu tatu (3,000) wanaishi na kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii katika mji huo wa Monte Puez.
Hatua hiyo inajiri licha ya mataifa ya Msumbiji na Tanzania kufanya mkutano wa kuainisha maeneo ya ushirikiano yakiwemo maswala ya kibiashara na uhamiaji.
Na huku operesheni hiyo ikiendelea serikali ya Tanzania imekuwakumbusha Watanzania wote waishio ughaibuni, kufuata Sheria na taratibu za nchi hizo wanazoishi.

Theresa Mei kuanzisha utaratibu wa Uingereza kujiondoa katika EU

media 
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May.REUTERS/Dylan Martinez
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa Mei amethibitisha Alhamisi hii kwa ataanzisha rasmiutaratibu wa Uingereza kujiondoka katika Umoja wa Ulaya ifikapo mwishoni mwa mwezi Machi.
Baraza la Seneti na Bunge walipitisha Jumatano hii kwa idadi kubwa ya wajumbe nakala inayomrushu rasmi kiongozi wa serikali kutumia Ibara ya 50 ya Mkataba wa Umoja wa Ulaya ambayo itaanzisha mchakato wa Uingereza kujionda katika Umoja huo.

Kisha itabidi kuepo kwa kipindi cha miaka miwili ya mazungumzo na Umoja wa Ulaya juu ya suala la Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya. Majadiliano yatajikita juu ya masuala ya biashara, uhamiaji na usalama.

Nakala juu ya Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya inatazamiwa kupitishwa na baraza la Wazee wa Busara. Serikali inataka nakala hiyo ipitishwe Machi 7.

Mvutano wajitokeza saa chache kabla ya mazungumzo kuanza mjini Arusha

Mazungumzo baina ya Burundi yalizinduliwa rasmi nchini Uganda Jumatatu, Desemba 28, kupitia upatanishi wa rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni.
Mwezeshaji katika mgogoro wa Burundi, Benjamin Mkapa, anatazamiwa kujaribu tena kuleta pamoja serikali na upinzani kwenye meza moja ya mazungumzo kuanzia Alhamisi hadi Jumamosi wiki hii mjini Arusha (kaskazini mwa Tanzania), mchakato ambao unaonekana kutozaa matunda yoyote.
Rais mstaafu wa Tanzania anataka kujadiliwa kwa mara ya kwanza "masuala nyeti", kama vile muhula wa tatu wa Rais Pierre Nkurunziza unaoendelea kuzua utata na "uundwaji wa serikali ya umoja wa kitaifa," amesema mwanadiplomasia wa Afrika ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Rais mstaafu wa Tanzania amealika katika mazungumzo hayo "kundi la watu 33 kwa upande wa serikali na washirika wake, na upande mwengine wanasiasa wa upinzani," amesema mwanadiplomasia huyo.

 
Mazungumzo baina ya Burundi yalzinduliwa rasmi nchini Uganda, Desemba 28, 2016.
 
Mkapa amewaalika hasa viongozi wakuu wa muungano wa wanasiasa walio uhamishoni na ndani ya nchi (Cnared), ikiwa ni pamoja na kiongozi wake Jean Minani, pamoja na vigogo wa zamani wa chama tawala cha CNDD-FDD ambao wanaishi uhamishoni baada kupinga muhula wa tatu wa Rais Nkurunziza.
Hata hivyo, majaribio ya kuwaleta kwenye meza moja ya mazungumzo serikali ya Burundi na upinzani walio uhamishoni hadi sasa yameshindwa. Serikali ya Bujumbura imekataa mpaka sasa kuketi kwenye meza ya mazungumzo na Cnared licha ya shinikizo na vikwazo kutoka jumuiya ya kimataifa.
"Cnared vuguvugu ambalo halitambuliwi na sheria ya Burundi na linaundwa na watu wanaotafutwa na vyombo vya sheria vya Burundi," Willy Nyamitwe, Mshari Mkuu wa mawasiliano wa rais ameliambia shirika la habari la AFP.
"Kwa hiyo ni wazi kwamba kuwaalika katika mchakato wowote wa mazungumzo ni tusi ambalo haliwezi kamwe kukubaliwa na serikali," Willy Nyamitwe amesema na kuongeza kuwa serikali ya Bujumbura itakataa kuketi kwenye meza ya mazungumzo na Cnared au mpatanishi wa Umoja wa Mataifa kwa Burundi Jamal Benomar.
Cnared kwa upandeimetangaza kuwa haitoshiriki katika kikao hicho cha mazungumzo.
Muungano huo wa wanasiasa wa upinzani ulimkataa Benjamin Mkapa kama mwezeshaji wa mgogoro wa Burundi, baada ya kusema mwezi Desemba kuwa haifai kuendelea kupinga "uhalali" wa kuchaguliwa kwa mara nyingine tena Rais Pierre Nkurunziza.
Cnared, ambayo inabaini kwamba katiba ya Burundi haimruhusu Nkurunziza kuwania muhula wa tatu, hata hivyo, "itatuma ujumbe wake kwenda mjini Arusha kuonana na Mkapa na kupata maelezo kadhaa kabla ya kuchukua uamuzi wa mwisho wa kushiriki au la katika mazungumzo hayo, " amesema mmoja wa viongozi wake, ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Hayo yakijiri asasi za kiraia zaidi ya 11 nchini Burundi zimetoa wito kwa serikali ya Bujumbura, kutoshiriki kwenye mazungumzo ya amani ya Arusha, yaliyoandaliwa na mratibu wa mazungumzo hayo, rais wa zamani wa Tanzania Benjamini Mkapa, kwa kile asasi hizo zinasema ni kualikwa kwa upande unaotuhumiwa kushiriki katika jaribio la mapinduzi mwezi April 2015.
Burundi imetumbukia katika mgogoro mkubwa tangu mwezi Aprili 2015 pale Rais Pierre Nkurunziza alipotangaza nia yake ya kuwania muhula wa tatu na kuchaguliwa kwa mara nyingine tena mwezi Julai mwaka huo huo. Machafuko nchini Burundi yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 500 na watu zaidi ya 300,000 kukimbilia nje ya nchi.

TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE (JKCI) KWA KUSHIRIKIANA HOSPITALI YA BLK YA NCHINI INDIA WATOA HUDUMA YA MATIBABU YA MOYO BILA YA KUFUNGUA KIFUA KWA WAGONJWA 16

Madaktari Bingwa wa Moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Peter Kisenge (kushoto) na Subhash Chandra (kulia) kutoka Hospitali ya BLK ya nchini India wakimwekea mgonjwa kifaa kitakachosaidia moyo kupata umeme kwa jina la kitaalam Pacemaker . JKCI kwa kushirikiana na BLK hospital kwa kutumia mtambo wa Cath Lab wamewafanyia wagonjwa 16 huduma mbalimbali za matibabu ya moyo ya bila kufungua kifua (Catheterization).
 
Madaktari Bingwa wa Moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Peter Kisenge (kushoto) na Subhash Chandra (kulia) kutoka Hospitali ya BLK ya nchini India wakimwekea mgonjwa betri ambalo litatumiwa na kifaa kitakachosaidia moyo kupata umeme kwa jina la kitaalam Pacemaker . JKCI kwa kushirikiana na BLK hospital kwa kutumia mtambo wa Cath Lab wamewafanyia wagonjwa 16 huduma mbalimbali za matibabu ya moyo ya bila kufungua kifua (Catheterization).
 
Daktari bingwa wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Peter Kisenge akimuhudumia Monica Mahenge ambaye amelazwa katika Taasisi hiyo baada ya kufanyiwa matibabu ya moyo kupitia mishipa ya damu bila kufungua kifua (Catheterization) kwa kutumia mtambo wa Cath lab . Monica ni mmoja kati ya wagonjwa 16 ambao JKCI kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Hospitali ya BLK ya nchini India walitoa huduma za matibabu ya kuzibua milango ya moyo (Valve), balloon mitral valve procedure (Valvuloplasty), kuzibua mishipa ya damu ya moyo, kufunga kifaa kitakachosaidia moyo kupata umeme (Pacemaker) na kuangalia utendaji kazi wa Moyo.
 
Madaktari bingwa wa Moyo, Wauguzi, Technologists, wataalam wa dawa za usingizi wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza kumpatia mgonjwa huduma za matibabu ya kuzibua milango ya moyo (Valve) bila kufungua kifua (Catheterization) kwa kutumia mtambo wa Cath lab .
 
Kazi ya kutoa huduma ya matibabu ya Moyo kwa mgonjwa kupitia mishipa ya damu bila kufungua kifua (Catheterization) kwa kutumia mtambo wa Cath lab ikiendelea.

ORODHA YA MAHAKIMU NA MAJAJI WALIOVURUGA KESI ZA WAUZA UNGA KUTUA KWA JAJI MKUU

Kamishina wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini Rogers Sianga 
JAJI Mkuu anatarajia  kupokea  orodha ya  majina ya mahakimu na majaji  ambao wamevuga kesi za watu wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya.
Hayo ameyasema leo  Kamishina wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini Rogers Sianga wakati wa mkuatano wa viongozi mbalimbali wa kitaifa na waandishi wa habari ulioandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda  kwa ajili  kupambana na dawa za kulevya.

 Sianga amesema kuwa kesi zimevurugwa na mahakimu na majaji. hivyo wale wote wanaohusika watashitakiwa na hata wawe na mali ambazo wamezipata kwa biashara hiyo zitataifishwa.
Amesema kuwa watazunguka katika maeneo mbalmbali ya jiji la Dar es Salaam ili kuhakikisha mtandao huo unapatikana na kwenda hata Zanzibar na mbinu zote wanazijua katika kufanya biashara hiyo.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amemkabidhi orodha ya majina 97 wanaojihusisha na dawa za kulevya na kuongeza kuwa moto umewashwa dhidi ya watu wanaojihusisha na dawa za kulevya.
Amesema kuwa kuna nyumba 200 zinajihisisha na kufanya biashara ya madawa ya kulevya hapa jijini ambapo wote hao watafikiwa katika operesheni.
Nae Mohamed Khalid TID , amesema kuwa sasa ni mnyama ambae yuko tayari kupambana nawatu wanaouza pamoja na kutumia dawa za kulevya na amerudi kwa kufanya kazi na kuongeza kuwa kuimba hakuitaji dawa za kulevya.
Katika mkutano huo watu wawili wametakiwa kufika katika Kituo cha Polisi kati ambao ni Chidi Mapenzi,  Ayuob Mfaume Kiboko.

Kama Unampenda kwa Dhati, Huwezi Kushindwa Kumsamehe

Ni matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko poa! Leo utakuwa nami Rammy Gallis nataka kuzungumza nawe msomaji kuhusu ishu ya msamaha. Penzi la kweli husamehe! Yawezekana kauli hiyo ikawa nyepesi sana kuitamka mdomoni lakini ni wachache wenye moyo wa kuitekeleza.
Tunashuhudia katika maisha yetu ya kila siku jinsi watu waliowahi kupendana kwa dhati au wanandoa walioishi kwa furaha kwa muda mrefu wakiachana kwa vurugu na ugomvi kwa sababu ya mmoja wao au wote wawili kushindwa kusameheana na kufungua ukurasa mpya katika mapenzi yao.
Takwimu zisizo rasmi zinaonesha kuwa zaidi ya nusu ya wanandoa wanasalitiana na kati ya hao ni wachache mno huweza kuendelea na uhusiano baada ya kugundua kuwa wamesalitiwa na wenzi wao.
Zipo sababu nyingi zinazosababisha usaliti lakini lengo langu leo siyo kuzungumzia hilo bali ni kujaribu kuiponya mioyo ya wanandoa au watu wanaoishi kwenye uhusiano wa kimapenzi, waliojeruhiwa na usaliti.
Yawezekana ulitokea kumpenda sana mwenzi wako, ukaamini wewe ndiyo kila kitu kwake, ukamtimizia kila kilichokuwa ndani ya uwezo wako lakini mwisho, ukaambulia maumivu baada ya kugundua kuwa anakusaliti.
Vitabu mbalimbali vya dini vinaeleza kuwa kosa pekee linaloweza kuivunja ndoa, hata ile iliyofungwa kwa baraka za Mungu, iwe ni madhabahuni au msikitini, ni USALITI.
Sitaki kupingana na maandiko hayo lakini nataka tujadiliane, ni lazima kila unapogundua kuwa mwenzi wako amekusaliti dawa yake ni kupeana talaka au kuachana kwa ugomvi? Dunia imebadilika, wanaume wengi wanasaliti ndoa zao kwa sababu moja au nyingine, hali kadhalika wanawake.
Mathalani umefunga ndoa na kuishi na mwenzi wako kwa kipindi kirefu mkipendana, kujaliana na kuoneshana kila aina ya mahaba lakini akateleza na kukusaliti ilihali bado anakupenda, utakapoamua kuachana naye na kwenda kwa mwingine, ukigundua naye anakusaliti utafanya nini? Utaachana na wangapi? Utaolewa na kuachika mara ngapi?
Bila shaka umeanza kunielewa kwamba siyo mara zote talaka au kuachana ndiyo suluhisho la usaliti ndani ya ndoa. La hasha! Siwafundishi watu wasaliti ndoa zao au uhusiano wao kwa makusudi wakitegemea kusamehewa, hapana.
Ninachotaka kukijengea hoja ni kwamba, hata baada ya mwenzi wako kukusaliti, bado mna nafasi ya kuendelea na maisha yenu ikiwa tu mtaamua kulishughulikia tatizo hilo kwa kina bila kujali watu wa nje wanasemaje.
Usikilize moyo wako, ni kweli amekusaliti! Amekuumiza, unahisi dunia yote imekuelemea, unatamani kufa au kuua, lakini je, moyo wako unakuambia nini? Upo tayari kumruhusu mwizi wako ndiye awe mmiliki halali wa mwenzi wako ambaye umetumia muda mrefu kumjenga awe vile unavyotaka?
Jibu sahihi halitapatikana kwa kukurupuka, hakuna uamuzi wa busara unaotoka ukiwa na hasira, jazba au ukiwa na shinikizo kubwa kutoka kwa marafiki, ndugu, majirani na watu wanaokuzunguka.
Pata muda wa kurelax kisha usikilize moyo wako, majibu yatakayotoka ukiwa umetulia, ndiyo yatakayoamua kama uendelee au usiendelee na uhusiano uliosababisha ukaumia.
Yawezekana wewe ndiyo ulikuwa sababu ya mwenzako kuchepuka, au ni tamaa za kimwili ndizo zilizomsukuma kuyafanya hayo, lakini jambo la msingi ni kujiuliza; bado anakupenda? Anaonesha kujutia makosa yake? Anakiri na kukuomba msamaha? Kabla hajakusaliti, mmefanya mambo mangapi mazuri? Tuliza akili kisha amua.
Wanachokosea watu wengi, inapotokea ugomvi ndani ya nyumba au katika uhusiano wa mapenzi, wengi huweka vinyongo na matokeo yake, vinyongo hivyo hukua taratibu na siku matatizo yakitokea tena, ukichanganya na vinbyongo vya muda mrefu ambavyo mtu anakuwa amevihifadhi, matokeo yake hasira zinakuwa kali mara dufu na mtu anashindwa kabisa kusamehe, hata kama ni tatizo dogo limetokea.
Ushauri wa msingi, inapotokea mwenzi wako amekukosea na akakuomba msamaha, msamehe kwa moyo wote na siyo kuweka vinyongo moyoni. Na wewe unapomkosea mwenzako, muombe msamaha nausirudie makosa. Kwa namna hiyo, itakuwa ni rahisi kukusamehe.

Mwanamke kuumwaumwa kabla ya hedhi (Premenstrual Tension)

 
KUMEKUWA na hali fulani ambayo huwapata baadhi ya wanawake hasa wa umri kati ya miaka ishirini na tano hadi arobaini, kujihisi wagonjwa siku chache kabla ya kupata damu ya hedhi. 

Hali hii huwafanya wanawake hawa wakapime presha kama imepanda au imeshuka, mara wakapime malaria, lakini mwisho wa siku vipimo vyote huonekana vipo sawa na akishapata tu damu ya hedhi kila kitu mwilini mwake kinakuwa sawa.

CHANZO CHA TATIZO
Kama tulivyoona, tatizo hili la kujihisi mgonjwa kabla ya hedhi Premenstrual Tension huwapata wanawake wenye umri wa miaka 25 hadi 40. Hadi sasa chanzo halisi cha ugonjwa huu hakijajulikani ingawa kisayansi inasadikiwa huwatokea wanawake wanapokuwa na kiwango kikubwa cha homoni ya Progesterone na Estrogen kwenye miili yao hasa kipindi cha pili cha mzunguko wa hedhi, yaani baada ya upevushaji wa mayai Ovulation.
Hali hii ya kuwa na kiwango kikubwa cha homoni hizi mwilini husababisha kuongezeka kwa mgandamizo wa madini ya Sodium mwilini ambayo hufanya mkusanyiko mkubwa wa maji mwilini na kufanya mwili uwe mzito na kiwango hicho cha maji husababisha kuvimba kwa tishu za neva na hata maji hayo hujikusanya hadi kwenye ubongo na kukuletea hali iitwayo Cerebral Edema ambapo pia tishu za ubongo huvimba kipindi hicho.

JINSI MWANAMKE ANAVYOJIHISI
Baada ya hali hii kutokea, mwanamke huanza kujihisi mgonjwa na atakuambia hajui hata nini kinamuuma, kichwa huuma sana, maumivu ya mwili, mwili huchoka huhisi kichefuchefu, anakuwa mkali na hana raha, kila sehemu ya mwili inauma, akili inakuwa haipo sawa, wakati mwingine anashindwa kuendelea na kazi zake, hupatwa na msongo wa mawazo na kujikuta anaweza hata kugombana na watu wake wa karibu.
Hali hii inapoanza kutokea huwa ni taratibu na kabla ya kupata damu ya hedhi humtesa mwanamke takriban siku saba hadi kumi kabla hajaona damu ya hedhi na hupotea masaa machache baada tu ya kupata hedhi na kujikuta hajambo kabisa na kushangaa siku zote alizokuwa anaumwa.

UCHUNGUZI
Ni vigumu kugundua tatizo hili moja kwa moja kwani wengine hali hii inapotokea huambatana na dalili nyingine kama maumivu ya mwili mfano kiuno, mgongo, kichwa, miguu hata nyama za mwilini.
Pia wanawake wengine huhisi maumivu ya tumbo chini ya kitovu, kufunga kupata haja kubwa, maumivu ya kifua, moyo kwenda mbio au kupatwa na ute mzito ukeni. Kwa hiyo unapoona tatizo hili linakuandama kila mwezi, basi ni vema umuone daktari wa magonjwa ya akina mama katika hospitali ya rufaa ya mkoa ili ufanyiwe uchunguzi wa kina.
Kwa kuwa ugonjwa huu unafanana sana na magonjwa mengine kufuatana na dalili zake, pia dalili zake zinachukua muda mrefu au siku saba hadi kumi, basi unaweza kujikuta mara kwa mara unatibiwa tatizo ambalo siyo, mfano unaweza kusikia mwanamke akilalamika kila mwezi anatibiwa malaria au kila mwezi anatibiwa yutiai au mwingine taifoidi, basi ilimradi kila mwezi unatibiwa ugonjwa huohuo usioisha.
Ugonjwa huu huchunguzwa kwa umakini kuzingatia historia ya tatizo na vipimo kuangalia kiwango cha vichocheo au homoni hizo mbili za Progesterone na Estrogen ambazo tumezitaja hapo awali. Pia kiwango cha madini ya Sodium kitahakikiwa kwenye damu ili kujiridhisha na tatizo. Baada ya hapo daktari atakushauri nini cha kufanya pamoja na matibabu ya ugonjwa wako.

MATIBABU NA USHAURI
Inashauriwa unapokuwa na tatizo hili hakikisha unakuwa mtulivu, jiweke kwenye hali ya usafi, hakuna ugonjwa ambao hauponi au haupati nafuu. Maana kama hauponi na imethibitishwa na madaktari, basi kuna njia ya mgonjwa kupatiwa nafuu.
Ugonjwa huu huwa unapona wenyewe pale mwanamke anapopata tu damu ya hedhi na huanza tena siku saba hadi kumi kabla ya tarehe ya kuona damu ya hedhi. Matibabu mengine yatatolewa kadiri daktari atakavyoona inafaa.

Vyuo vikuu binafsi hatarini kukosa wanafunzi

Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako
HATUA ya Serikali ya kupandisha kiwango cha ufaulu wa kujiunga na chuo kikuu kutoka alama mbili hadi nne, itavifanya vyuo vikuu binafsi vikose wanafunzi katika mwaka wa masomo 2016/17, JAMBOLEO limeelezwa. 

Habari kutoka baadhi ya vyuo hivyo, ikiwamo vilivyofungwa kudahili wanafunzi mwaka huu, imeeleza kuwa uamuzi huo wa Serikali utawaondoa kwenye udahili wanafunzi 16,000 waliopata alama mbili katika matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa hivi karibuni.
“Kuna zaidi ya wanafunzi 16,000 ambao hawatapata fursa ya kujiunga na chuo kikuu mwaka huu, kulingana na mwongozo wa sasa kwamba waliopata alama mbili wasidahiliwe,” alisema Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Baamoyo, Profesa Costa Mahalu na kuongeza:
“Hiki ni kiama kwa vyuo vikuu binafsi, maana idadi ya waliopata alama nne ni ndogo na inawezekana wote wakaenda kwenye vyuo vikuu vya umma. Kibaya zaidi hakuna mahala ambako Serikali imepanga kuwapeleka hao ambao hawatadahiliwa.”
Kauli ya Profesa Mahalu iliungwa mkono na wahadhiri wengine kadhaa, waliosema kuwa kitendo cha Serikali kupandisha alama ya ufaulu wa kujiunga na chuo kikuu, kitaongeza ‘vilaza’ badala ya kuwapunguza.
Mmoja wa wahadhili hao kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba (IMTU), ambaye hakutaka kutajwa gazetini kwa kile alichoeleza kuwa si msemaji wa chuo, alisema: “Mtu hawezi kuwa ‘kilaza’ akiwa chuo kikuu.”
Alisema: “’Ukilaza’ unaanzia elimu ya msingi na sekondari. Jambo la maana hapa si kupandisha kiwango cha ufaulu ili kuondoa ‘vilaza’, muhimu ni kuangalia mfumo wetu wa elimu kuanzia chini. Elimu yetu haisaidii watoto kufanya kazi, inataka wawe na vyeti tu.”
Mhadhiri huyo alibainisha kuwa kwa sababu Serikali haijaandaa mahala pa kupeleka wanafunzi waliopata alama mbili, sasa watatafuta vyuo nje ya nchi kwa gharama ya vyuo vya ndani.
Alipoulizwa ilikuwaje ikakubalika wenye ufaulu wa alama mbili wajiunge na vyuo vikuu na sasa imefutwa, mhadhiri huyo alijibu: “Ndiyo maana nasema Waziri anakurupuka. Haya yalikuwa makubaliano kati ya vyuo na TCU. Sasa yeye anakuja kuyatengua bila kupata ushauri.”

Kufunga vyuo
Katika hatua nyingine, baadhi ya wahadhiri wa vyuo vitano vilivyofungwa kudahili wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2016/17 walimtuhumu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Joyce Ndalichako kwamba anatumika kuvihujumu. Kwa nyakati tofauti wasomi hao walisema hakuna sheria inayompa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, mamlaka ya kufunga vyuo, badala yake kupitia Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) anapaswa kuvieleza kasoro na kusimamia kuzisahihisha.
“Kuna mambo mengi ambayo sisi wadau tukiyaangalia tunashindwa kuelewa waziri ana nia gani na elimu ya Tanzania. Amekuwa akijiamulia mambo bila ushauri na kibaya zaidi anaingilia kazi za TCU,” alisema mmoja wa wahadhiri hao ambaye hakutaka kutajwa gazetini.
Mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) alieleza kuwa tangu Mei, Waziri amekuwa akifanya mambo matatu yanayoingilia utendaji wa vyuo vikuu na hata kutia hofu kwamba chini ya uongozi wake, kiwango cha elimu kitashuka.
Alitaja mambo hayo kuwa ni kuvifunga vyuo kudahili wanafunzi mwaka huu wa masomo, sakata la wanafunzi hewa na kupandisha kiwango cha ufaulu wa kujiunga na vyuo vikuu. Mapema Julai, Waziri Ndalichako alitangaza kuvifunga vyuo vitano kudahili wanafunzi kwa madai kuwa havijakidhi vigezo vya kuendesha kozi husika.
Vyuo hivyo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Bagamoyo (kozi zote), Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba (IMTU), Chuo Kikuu cha Dodoma (Utabibu), Chuo kikuu cha St. Francis na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar. Mmoja wa wahadhiri wa vyuo hivyo ambaye hakutaka kutajwa gazetini kwa alichoeleza kuwa anaweza kuandamwa na Waziri Ndalichako, alisema:
“Utadhani kuna uadui kati yetu na Waziri, kumbuka hakuna sheria ya kufunga vyuo, lakini pamoja na kwamba tayari ameagiza tusidahili wanafunzi mwaka huu, hatuna barua rasmi inayotuzuia kufanya hivyo.” Aliendelea “Kuna hatua kadhaa ambazo lazima zipitiwe, moja, wanakuja wakaguzi ambao kibaya zaidi wanaokagua vyuo hivyo wote wanatoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao ni washindani wetu katika kutafuta wanafunzi.
“Kama watabaini kasoro wanakieleza chuo husika na kukitaka kifanye marekebisho. Cha ajabu sisi tumefanya marekebisho na hawajaja kukagua tena, lakini tunasikia tu kwamba tumefungwa.”
Mhadhiri huyo alipendekeza iwepo Bodi maalumu ya kukagua vyuo, badala ya kutumia wakaguzi wa chuo kimoja cha Serikali ambao wanaweza kuwa na maslahi binafsi.
“Mwaka huu UDSM ilianzisha kozi tatu mpya; Udaktari Kilimo na Majenzi. Hapa unaona kwamba wanaleta ushindani katika vyuo vya Sokoine, Ardhi na vingine vinavyoendesha kozi hizo. Kwa nini wasiwe na maslahi wanapovikagua ili wawapoke wanafunzi?” Alihoji.
Wanafunzi hewa
Wahadhiri hao walisema uamuzi mwingine unaohatarisha uhai wa vyuo vikuu binafsi ni kutafuta wanafunzi hewa kuanzia Mei.
“Utekelezaji wake umetuathiri sana kwa kuwa tangu Mei, Bodi imesitisha mkopo kwa wanafunzi wote. Fikiria sisi (vyuo binafsi) tunajiendesha kwa ada za wanafunzi, halafu Bodi inasitisha mkopo, tutalipaje mishahara ya walimu, bili za umeme na maji?” Alihoji.
Aliendelea: “Julai 25, Waziri Ndalichako alikoleza moto kwa kutoa agizo la kuzuia wanafunzi wa kwenda kwenye mafunzo kwa vitendo kwa madai kuwa hakuna pesa. Wanafunzi wakaruhusiwa waende likizo, lakini baada ya wiki mbili akatoa tena tangazo kuwa wanafunzi wanatakiwa kwenda kwenye mafunzo hayo Agosti 8.
“Mwanafunzi aliye likizo utampata wapi asaini fomu ili aingiziwe pesa za vitendo?. Maana pesa haiwezi kuingizwa mpaka asaini,” alihoji na kubainisha kuwa maagizo kama hayo aliyoyaita ya kukurupuka, ndiyo yanayoleta picha kwamba kuna wanafunzi hewa.
Mhadhiri huyo aliponda uamuzi wa Serikali kutumia Takukuru kutafuta wanafunzi hewa vyuoni, akieleza kuwa hauna tija. “Kuna wanafunzi wanatumiwa fedha halafu wanakuja kusaini baadaye, unamwitaje hewa wakati tatizo hilo umelisababisha mwenyewe.”
Majibu ya Wizara
Waziri Ndalichako hakupatikana kuzungumzia suala hilo, lakini Ofisa Habari wa Wizara, Oliva Kato alisema Waziri ndiye mwenye dhamana na mambo yote yanayohusu elimu, hivyo uamuzi ule aliufanya kama mtu aliye na mamlaka ya kusimamia elimu. “Kama Waziri ameingilia mamlaka ya TCU ambaye angetakiwa kuleta malalamiko ni TCU, umeshasikia wamelalamika au unajua ukomo wa majukumu ya Waziri?” Alihoji Kato.
Aidha, alisema kuhusu vyuo hivyo kutopelekewa barua rasmi ya kusimamishwa kufanya udahili wa wanafunzi mwenye majibu ni TCU.
Kaimu Mkurugenzi wa TCU, Profesa Eliuter Mwageni alipotafutwa kwa njia ya simu atoe majibu, alisema haamini kama anaongea na mwandishi wa habari.
“Nitajuaje kama naongea na mwandishi, nitafute ofisini tutazungumza,” alisema.

Wachumi; Sababu ya fedha kupotea mitaani

WASOMI wa fani ya uchumi nchini, wametaja mambo yaliyochangia fedha kupotea kwenye mzunguko, tofauti na kauli ya Rais John Magufuli, kuwa huenda kuna watu wamezificha majumbani.
Huku wakitaka utafiti ufanyike kuhusu hali hiyo, wasomi hao wamesema hali hiyo pia imechang­iwa na hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano, ku­dhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Mhadhiri wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Pro­fesa Humphrey Moshi alisema kuto­kana na hatua hizo, watu wako ma­kini kwenye matumizi, kwa sababu fedha zinapatikana kwa wanaofanya kazi tu na ndiyo maana hazionekani mitaani.
“Watu wamekuwa makini katika utoaji na utumiaji wa fedha zao, mtu hawezi kutoa fedha tu wakati haz­alishi, zamani kabla ya kuingia Rais John Magufuli, fedha zilikuwa zi­nazagaa kwa kuwa kulikuwa na mi­anya mingi ya kupiga ‘dili’,’’ alisema.
Alitaja mambo yanayosababisha kupotea kwa fedha mtaani, kuwa ni pamoja na kusitishwa kwa safari za nje kwa watumishi wa umma, am­bazo kwa mujibu wa Profesa Moshi, safari hizo zilikuwa zikiwapa watu fedha za ziada.
Alitaja hatua ya Serikali kukabili­ana na watumishi hewa waliogun­dulika, kwamba kabla ya hapo tatizo hilo lilisababisha watu kupata fedha kwa njia zisizo halali na kuzitumia hovyo mitaani.
“Pia kuna wafanyabiashara wal­iokuwa wakiingiza bidhaa bila kuli­pia kodi, nao walikuwa wanatumia fedha vibaya ndiyo maana zilikuwa zinazagaa tu na watu wanafanya starehe,’’ alisema.
Profesa Moshi alisema baada ya hatua hizo za Serikali ambazo zi­naendelea, kwa sasa ili mtu apate fedha, ni lazima afanye kazi na kin­achotakiwa si wananchi kulalamika, bali kujitahidi kutafuta njia za kuji­ingiza kipato.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi alisema hata kudorora wa shughuli za uchumi na kodi kubwa, vinaweza kupunguza fedha mifukoni, hivyo ni vyema kufanyie utafiti utakaosa­idia kutoa majibu mazuri.
Kwa mujibu wa Profesa Ngowi, hata riba kubwa ya kukopa benki inaweza kupunguza fedha mitaani kwa kuwa zina tabia ya kukatisha tamaa wakopaji.
Alisema riba ya kuweka fedha ben­ki nayo ikiwa kubwa, huvutia watu kuweka fedha benki badala ya kuzi­acha kwenye mzunguko, lakini hata sera za kifedha za kupunguza fedha kwenye mzunguko kwa sababu mbalimbali kama vile kupunguza mfumuko wa bei, nazo huchangia kupunguza fedha.
“Lakini pia fedha zinaweza kuon­dolewa kwenye mzunguko na watu kwa sababu kadhaa na kwa njia to­fauti, ili hali hiyo ijitokeze na kute­temesha uchumi, lazima wawe watu wengi wanaofanya hivyo au wach­ache wenye fedha nyingi,” alisema.

Jecha ‘aahirisha’ kesi ya uchochezi

SWALI kuhusu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha limeilazimisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuahirisha kesi ya uchochezi.
Kesi hiyo inawakabili Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na wahariri wa Gazeti la Mawio, baada ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni kukataa kujibu swali la Lissu lililotaka kujua kama Jecha ana mamlaka ya kufuta Uchaguzi Mkuu au la.
Suali hilo lilizua mvutano mkali wa kisheria, wakati Lissu akijitetea katika kesi ya tuhuma za kuchapisha taarifa za uchochezi yenye kichwa cha habari kisemacho, Machafuko yaja Zanzibar.
Lissu alimtaka Hamduni kujibu swali hilo, kwa sababu hati ya mashitaka inaruhusu swali hilo, hali ambayo ilisababisha mvutano mkali uliosababisha mawakili wa pande zote kuja juu na kuona kila mmoja ana haki kwa kuvutia upande wake.
Lissu alimwambia Hamduni, “shahidi naomba unijibu swali, Jecha ana mamlaka ya kufuta Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar?”
Hamduni alikaa kimya huku Wakili wa Serikali, Paul Kadushi akisimama kupinga swali hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
“Hakimu shahidi si mwanasheria wala si mtafsiri wa sheria na wala si mtaalamu wa Katiba ya Zanzibar kwa hiyo napinga  kujibu swali hilo,” alisema Kadushi.
Jibu la Kadushi lilimfanya Lissu apaze sauti kwa kudai kuwa wakili wa Serikali anamlisha maneno ambayo hajayasema na pia anatakiwa ajibu kwa sababu katika hati, mashitaka ya pili yanahusiana na swali alilouliza.
Pia Lissu alikwenda mbali zaidi kwa kumtaka shahidi amweleze kama ilikuwa ni halali yeye kushitakiwa katika kesi hiyo, kutokana na kwamba yeye si mwandishi, mhariri, wala mmiliki wa Mawio wala mchapishaji, lakini shahidi alimjibu kuwa inaweza ikawa halali kutegemea na mazingira.
Lissu hakukubaliana na jibu hilo na kumtaka Kamanda huyo kumweleza ni njia gani ambayo walitumia kula njama ya kutenda kosa hilo, ambapo majibu ya shahidi yalikuwa kwamba hajui ni njia gani walitumia wala wapi walikaa kwa sababu kuna timu ya upelelezi ndiyo ilikuwa inashughulikia suala hilo.
Mbali na Lissu washitakiwa wengine ni Mhariri wa Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na  Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.
Kwa pamoja washitakiwa hao, wanakabiliwa na mashitaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.
Inadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, mwaka jana Dar es Salaam, washitakiwa Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.
Katika mashitaka ya pili wanadaiwa kuwa Januari 14, mwaka jana Dar es Salaam,  walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.
Mehboob  anadaiwa kuwa Januari 13, mwaka jana katika jengo la Jamana Ilala,  Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.
Alidai mshitakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila kuwasilisha hati ya  sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.
Mbali na mashitaka hayo washitakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuwa Januari 14, mwaka jana,  Dar es Salaam, bila mamlaka waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar   wasiweze kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.

Makonda akosolewa kwa hatua nyingine

KITENDO cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuwaonesha hadharani watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 na kuwatangaza wameathirika na Ukimwi kimekosolewa kuwa kimewaongeza watoto hao matatizo mengine.
Wanasheria na wabunge wametoa maoni hayo baada ya Makonda juzi kuwaonyesha watoto hao hadharani akisema wameacha dawa za kulevya huku mmojawapo akiathirika kwa Ukimwi.
Katika maoni yake, Mwanasheria James Marenga alisema alichofanya Makonda si sawa kisheria, huku akitoa angalizo kwa viongozi wengine kusoma sheria za nchi kabla ya kufanya mambo yao.
Marenga alisema baadhi ya vyombo vya habari vinapaswa kupongezwa kwa kutambua changamoto hiyo na kuficha sura za watoto hao.
Alisema ingawa sheria inaelekeza kuwa iwapo kitendo kinachofanyika ni kwa faida ya mtoto inawezekana kuwaweka wazi, lakini tukio la juzi ni kuongeza tatizo kwa watoto hao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mbunge wa Viti Maalumu na Mujumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Suzan Lyimo alisema kitendo hicho ni kinyume na sheria ya mtoto na kimethibitisha, kwamba Makonda hatoshi kwenye nafasi aliyonayo kwa kuwaongeza matatizo watoto hao na kuwadhalilisha.
Lyimo alisema sheria ya mtoto iko wazi kuhusu haki za mtoto hivyo anasikitishwa mtu aliyeapa kulinda Katiba anaivunja kwa makusudi.
“Kimsingi Makonda hatoshi katika nafasi aliyomo, nadhani hata katika ngazi ya ukuu wa wilaya alionesha kufeli, kilichopo ni kubebana, ndiyo maana kila siku anaibuka na mambo yanayokwenda kinyume na taratibu,” alisema.
Alisema kitendo cha kuwaonesha watoto hao hadharani kinahatarisha maisha yao, kwani upo uwezekano wa kuwa alikuwa na mpenzi na hakumwambia kuwa ameathirika hivyo kumdhuru.
Mbunge huyo alisema halikadhalika kitendo hicho kimeweka mazingira mabaya kwa watoto hao kwa miaka ijayo, kwani inaweza kuwa sababu ya kunyanyapaliwa.
Alisema yeye akiwa mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, atahakikisha kitendo hicho kinajadiliwa Bunge lijalo ili kuweka mambo sawa.
Mbunge Viti Maalumu, Anatropia Theonest (Chadema), aliungana na Lyimo kuwa kitendo hicho kinaongeza tatizo lingine kwa watoto hao.
“Kiuhalisia watoto hao wako kwenye matatizo ambayo yaliwapata wakiwa wadogo, halafu mtu mwingine kwa sababu ya kutafuta sifa anawaongeza tatizo, akiamini ndiyo njia sahihi ya kuwasaidia kumbe anapotea,” alisema.
Alisema viongozi kama Makonda ni janga kwa Serikali, hivyo hakuna sababu ya kuwavumilia kwani wanahatarisha usalama wa watu na nchi.
Dk. Hellen Kijo-Bisimba alisema ni wakati wa wasimamia haki kushikamana ili kukomboa Taifa kwa alichodai ni upungufu mwingi na ukiukwaji wa haki za watoto.
Mwenyekiti wa Bodi ya Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukita), Deus Kibamba alisema Makonda anajitahidi kufanya watu waache kujadili hoja za nchi na kumjadili mtu, jambo ambalo si sahihi.
Alisema zipo sheria zaidi ya tano ambazo zinaelekeza nini kifanyike kwa watoto kama wale, hivyo ni bahati mbaya kuna wakuu wa mikoa ambao wanavunja sheria na Katiba na si kuilinda.
“Inaniuma kukaa kujadili sokomoko ambalo analileta Makonda katika nchi kwa udhaifu wake wa kutojua sheria na Katiba au labda anafanya hivyo ili aonekane,” alisema.

BARUA YANGU YA WAZI KWA MHE. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI

Hali ya Elimu Tanzania

Katikadunia ya leo, ilikila mtuaweze kuboresha maisha yake ni lazima awe na elimu.
Elimu ndiyo inayomwezesha mtu kujitambua na kujimiliki yeye mwenyewe kwanza, pia kuzikabili changamoto zinazomsonga, kuyatawala na kuyatumia mazingira yanayomzunguka ili kuboresha maisha yake. Ndani ya utandawazi, elimu isiyotosheleza, tafsiri yake ni umaskini zaidi; wakati elimu zaidi tafsiri yake ni maisha bora zaidi.
 Related image
Hayati Rais mstaafu wa Afrika KusiniNelson Mandela amewahi kusisitiza umuhimu wa elimu kwa maendeleo ya jamii, kwa kusema kuwa;
“........elimu ni injini kubwa ya maendeleo ya mtu. Ni kupitia elimu ndipobinti wa mkulima mdogo anaweza kuwa daktari bingwa, kwamba mtoto wa kibarua wa mgodini anakuwa Mkuu wa Mgodi, na mtoto wa kibarua wa mashambani anakuwa Rais wa taifa kubwa”. (Mandela, 1991).
Ili elimu iweze kuleta mabadiliko ya kweli kimaendeleo, ni lazima iwe elimu bora ambayo inalenga kumbadilisha mtu na kumwezesha kufikiri, kubuni, kujitambua, kuhoji, kudadisi, kupenda kazi, kuwa na mwenendo mwema na kuboresha afya na maisha yake binafsi na ya jamii. 
Elimu ni ukombozi iwapo italenga kumpatia mtu uwezo wa kupambana na changamoto zinazoikabili jamii na taifa kwa ujumla. Elimu inamjenga mtu kuwa raia makini na mzalishaji ndani ya nchi yake.
Historia ya elimu nchini inatukumbusha malengo ya msingi ya elimu Tanzania. Ukiacha elimu ya kibaguzi iliyokuwa inatolewa kabla ya uhuru, elimu ya Tanzania baada ya uhuru ililenga kumjenga mtu katika nyanja zote ili awe mzalishaji mzuri katika nchi yake.
Ndiyo maana elimu na kazi vilisisitizwa, na vyuo vya ufundi pamoja na kazi za mikono vilipewa msisitizo mkubwa, huku suala la usawa, haki na misingi ya umoja wa kitaifa vikichanua na kushamiri kwenye nyaraka za serikali na kwenye vichwa vya watu.
Dhamira hii ikaleta maboresho makubwa yakiwamo ongezeko kubwa la uandikishaji, kutaifishwa kwa shule za binafsi na kufanywa za umma na kuzaliwa kwa Azimio la Arusha lililokuja kuwa dira ya kusimamia misingi ya haki, usawa, udugu na utu.
Solomon Eliufoo ndiye aliyeongoza michakato hii kama Waziri wa Elimu kutoka mwaka 1962 hadi 1965.
Katika kipindi chake, Eliufoo alipiga marufuku ada kwa wanafunzi wa sekondari, kuendeleza ujenzi wa shule za msingi na sekondari na upanuzi wa mafunzo kwa walimu wa daraja A na C na elimu ya watu wazima.
Pia ndani ya miaka hii mabadiliko mengine tuliyoshuhudia ni kuruhusiwa kwa Kiswahili kutumika kama lugha ya kufundishia katika elimu ya msingi na Kiingereza kwas sekondari, kupinga ubaguzi wa rangi katika elimu na elimu ya msingi kutangazwa kutolewa kwa miaka minane.
Kipindi cha 1965 hadi 1970 chini ya Waziri Chediel Mgonja, kilishuhudia uamuzi wa Rais wa Awamu ya Kwanza, Julius Kambarage Nyerere, akitangaza rasmi falsafa mpya ya elimu iliyojulikana kwa jina la Elimu ya Kujitegemea, kuanzishwa kwa Taasisi ya Elimu na uundwaji wa Baraza la Mitihani la Afrika Mashariki.
Mabadiliko mengine katika kipindi hiki yalihusu kutungwa kwa Sheria ya Elimu ya mwaka 1969, shule za msingi kufundishwa na Watanzania pekee na kuimarishwa kwa kisomo cha watu wazima na chenye manufaa.
Elimu ya watu wazima ndiyo iliyojenga nchi na kuiweka kwenye hadhi ya juu katika medani za kimataifa, hasa kwenye suala la upunguzaji wa ujinga.
Hadi kufikia mwaka 1986 kiwango cha Watanzania kujua kusoma na kuandika kilikuwa ni asilimia 91, tofauti na sasa ambapo kimeshuka hadi asilimia 69 kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya HakiEilmu mwaka 2001 na 2010. Miaka ya 1975 hadi 1980 ilishuhudia mabadiliko mengi tu kwenye mfumo wa elimu yetu.
Ni kati ya miaka hiyo, ujenzi wa vyuo vya maendeleo ya wananchi ulifanyika, kutolewa kwa Tamko la Elimu ya Msingi kwa wote, ujenzi wa vituo vya ufundi kwa wahitimu wa elimu ya msingi na kuzuiwa kwa mtihani wa darasa la nne. 
Pia Taasisi ya Ukuzaji Mitaala na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima vilianzishwa. Na mwaka 1978 ndiyo kipindi ilipotungwa Sheria ya Elimu namba 25 chini ya Waziri Nicholas Kuhanga.
Kuanzia mwaka 1995 hadi 2005, mengi yamefanyika ikiwamo kuanza kwa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu (ESDP), kuanza kwa Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Sekondari (MMES).
Mipango hii ndiyo inayoshika hatamu za kuiendesha elimu yetu kuelekea kwenye ubora na fursa sawa kwa wote. Je, tija ya mabadiliko haya tangu uhuru ina mwelekeo  gani kwa Taifa? Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Mkakati  wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA), Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM), Mpango wa Maendeleo.
Taarifa ya idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika aliyoitoa Naibu Waziri wa Elimu, Philip Mulugo bungeni Februari 15, 2011 ya Elimu ya Sekondari (MMMES) na Sera ya Elimu na Mafunzo vyote vinabainisha ukweli huu kuwa ili Tanzania ipige hatua kali za kimaendeleo ni lazima wananchi wake wapate elimu bora iliyokamilika. 
Lakini  je, elimu inayotolewa hapa Tanzania inakidhi haya yote? Ama ni kwa kiasi gani inawawezesha watoto na vijana kufikia malengo hayo? Hili ndilo swali la msingi linalopaswa kutuongoza kuelekea kwenye mipango na vitendo vinavyoipeleka mbele elimu yetu na siyo kuirudisha nyuma.
Hivi karibuni tumesikia mengi kutoka kwa viongozi wetu kuhusu elimu hapa nchini akiwamo Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Pombe Magufuli, akisemea kutoa elimu bure kwa watoto kuanzia awali hadi kidato cha nne.
Watanzania wanapenda elimu yenye ubora na siyo tu kwa kuwa itatolewa bure iwe chini ya kiwango, tunaamini kuwa “vya bure havina thamani” lakini hatutarajii kuona upuuzi huu ukiendelea. 
Imekuwa kawaida kuwaona wanafunzi waliohitimu darasa la saba wakiwa hawajui kusoma na kuandika. Masikio ya Watanzania na macho wanatamani kuiona kauli ya “elimu bure” ikifanyiwa utekelezaji mapema Januari mwaka ujao.  
Hadi mwaka 2010 zaidi ya watoto milioni 8 (ambao ni zaidi ya asilimia 90 ya uandikishaji halisi) wameandikishwa shule za msingi na zaidi ya wanafunzi 1,638,699 wako sekondari.
Lengo la makala yangu hii ni kutaka kutoa maoni ama ushauri wa namna gani wa sera ya elimu yetu inaweza kufanikiwa hususani kwa elimu ya msingi na sekondari ukilinganisha na miaka ishirini iliyopita ni kuwa na elimu inayomfanya kijana kujua ni nini dhumuni la yeye kusoma, au mantiki yake na zaidi mfumo wetu wa elimu utumike kumwandaa kijana kuwa tegemezi na kuweza kujiajiri.
Aidha nitoe rai yangu kwa serikali na wizara ya elimu sera ya viboko shuleni hapo awali ilitumika kumdhibiti mwanafunzi dhidi ya mienendo yake, ilimfanya mwanafunzi kuwa na nidhamu, na kuzingatia masomo yake ambapo kutokana na mfumo wa elimu ya sasa ungekuwepo hapo awali naamini taifa letu lingekuwa mbali kimtamzamo. lakini nimalizie kwa kusema kwamba kunayo haja kwa serikali kutoa maagizo kwa Taasisi za elimu kusimamia na kutekeleza hayo, aidha kuruhusu viboko, kukimbia mchakamchaka na pia ikifaa serikali iruhusu migambo wa jiji kuhakikisha wanapambana na wanafunzu wote wanaoonekana kudhurura mitaani, na maeneo mbalimbali ya mji mfano. standi, katikati ya mji, kwenye vibanda vya kuonesha sinema, magofu na nyumba zilizopo kwenye kipindi cha ujenzi. kukifanikishwa haya naamini kwamba Waziri wa elimu pamoja na watendaji wakuu wa wizara ya elimu, sayansi, teknolojia na ufundi mtafanikiwa kutimiza sera ya elimu ya awamu ya tano kwa njia rahisi na isiyo na mikwamo, amapo idadi kubwa ya vijana wadogo wanaotumia mihadarati na wanaojishughulisha na shughuli zisizo rasmi hatutakuwa nao tena kutokana na serika kuweka udhibiti wao.