TTCL

EQUITY

Monday, December 8, 2014

KAFULILA APENDEKEZA DOKTA SLAA KUWA MGOMBEA URAISI WA UKAWA 2015

katibu mkuu wa chadema Dk Willbrod Slaa akizungumza na wanahabari ofisini kwake hivi karibuni 

Dar es Salaam. Wakati vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vikitafakari jina la mgombea urais, Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila tayari anaye mtu anayefaa; anamtaka Dk Willbrod Slaa.

Kwa maoni yake, si kwamba viongozi au wanachama wa vyama vingine vinavyounda Ukawa hawana sifa za kuwania nafasi hiyo ya juu katika siasa nchini, bali Dk Slaa ana sifa ya ziada; ana mvuto.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Kafulila, ambaye alikuwa mwanachama wa Chadema kabla ya kuondoka na kujiunga na NCCR-Mageuzi mwaka 2010, alisema Dk Slaa ana nafasi kubwa kuliko viongozi wa vyama vingine vya siasa vinavyounda umoja huo ambavyo ni Chadema, NCCR, NLD na CUF kwa sababu katibu huyo mkuu wa Chadema anakubalika zaidi katika jamii kulinganisha na wengine.

Vyama hivyo vinne vilitia saini ya makubaliano ya ushirikiano Oktoba 27, hasa ya kusimamisha mgombea mmoja katika chaguzi zote, kuanzia wa Serikali za Mitaa mwaka huu na madiwani, wabunge na rais mwaka 2015.

Hata hivyo, bado kamati maalumu inatafakari jinsi ya kutekeleza makubaliano hayo ili kuzuia uwezekano wa mpango huo kuvurugika kama ilivyowahi kutokea kwenye chaguzi zilizopita.

Miongoni mwa watu wanaopewa nafasi ya kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya Ukawa ni pamoja na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Dk Slaa.

“Kwa maoni yangu bado namwona Dk Slaa kuwa ni mtu ambaye ana nafasi kubwa kuliko wenzake. Kwa vyovyote itakavyokuwa yeye ndiye anawazidi wenzake kwa kukubalika,” alisema Kafulila (32) alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu mgombea urais kwa tiketi ya Ukawa na kuongeza: “Siyo kama wengine hawawezi, hapana, ila si kila mwenye mvuto anaweza kuongoza na wala si kila mwenye sifa anayeweza kuwa na mvuto. Pia si kila anayekubalika anaweza na si kila anayeweza anakubalika. Ni adimu kukuta mtu anaweza na anakubalika pia.”

Katika matokeo ya utafiti wa taasisi ya Twaweza, Dk Slaa alishika nafasi ya tatu nyuma ya waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na wa sasa, Mizengo Pinda akipewa asilimia 11 ya ushindi kulinganisha na Pinda (asilimia 12) na Lowassa (asilimia 13).

Lipumba amegombea urais mara nne, akiwa ameshika nafasi ya pili mwaka 2000 na 2005 kabla ya kushuka mwaka 2010 wakati Dk Slaa alipopata asilimia 26 za kura katika uchaguzi ambao mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete aliposhuka kwa takriban asilimia 20 ya kura alizopata mwaka 2005.

Mbowe aligombea urais mwaka 2005 na kushika nafasi ya tatu wakati James Mbatia hajawahi kugombea urais na katika siku za karibuni ameonekana kuelekeza nguvu kugombea ubunge wa Jimbo la Vunjo, ambako kuna uwezekano mkubwa akapambana vikali na mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema.

Alipoulizwa kama kuna uwezekano wa mgombea wa umoja huo kuibuka na ushindi, Kafulila alisema: “Ni mapema mno kusema Ukawa inaweza kushinda. Hiyo itategemea tunajipangaje, tukifanya makosa tutashindwa vibaya. Makosa ya CCM na Ukawa yanategemeana kwenye kuamua nani agombee.”

Akizungumzia vigogo wa CCM wanaotajwa kuutaka urais kama wana uwezo wa kuchuana na Dk Slaa, Kafulila alisema mpaka sasa hajaona hata mtu mmoja mwenye uwezo na sifa za kuwa rais wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment