. Dkt Mkumbo asema njama za kuvuliwa nyadhifa zao ni mkakati wa viongozi wa juu chamani
.Ukosoaji wa hesabu za chama moja ya chanzo cha kuvuliwa uanachama Kabwe
. Kamati kuu ina wasi wasi wa siasa za ushindani 
-Wasema ni mbio za uchaguzi  mkuu wa chama Desemba mwaka huu
.Posho za kukaa bungeni (Sitting Allowance) kaa la moto
IMG_5201
 
VIONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliovuliwa nyadhifa zao hivi karibuni Dkt. Kitila Mkumbo na Zitto Kabwe wamesema kwamba njama zilizotumika kuwavua madaraka ni mkakati wa viongozi wa juu wa chama katika kujipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa chama unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu. MOblog inaripoti.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo asubuhi jijini Dar es Salaam katika hoteli ya Serena, aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Dkt. Kitila Mkumbo amesema waraka wa siri unaojulikana kama Mkakati wa Mabadiliko 2013 uliandaliwa na kuhaririwa na yeye kwa kuwa katika siasa za ushindani kuandaaa mkakati wa ushindi si uhaini.
“siamini hata kidogo kwamba kugombea nafasi yeyote iliyo wazi ndani ya chama cha siasa ni uhaini na hujuma. Msingi namba moja wa Chadema ni Demokrasia na hakuna namna ya kudhihirisha mapenzi kwa Demokrasia zaidi ya kuruhusu ushindani katika nafasi za uongozi na hasa uongozi wa juu kabisa,” amesema Dkt. Mkumbo
Amesema kwamba viongozi wa juu wa Chadema wana hofu ya siasa za ushindani baada ya kukaribia kwa uchaguzi mkuu ndani ya chama na yeye pamoja na Samson Mwigamba wanaamini kwamba madadiliko ya uongozi wa juu wa chama ni lazima.
IMG_5215

Dkt. Mkumbo aliendelea kusema kwamba mkakati kwa ajili ya uchaguzi iwe ndani ya chama au nje ya chama ni haki ya kikatiba kwa sababu ni mkakati wa uchaguzi hata viongozi wa juu wa sasa wa Chadema walikuwa na mkakati wao katika kujiandaa na uchaguzi ndani ya chama.
“Siasa za ushindania ndani ya chama cha siasa ni kujenga Demokrasia ya kweli na kama chama kikuu cha upinzani kinakataa kujenga Demokrasia kinachoililia kila siku kwenye chama tawala ni Udikteta usiokubalika katika dunia ya leo,” alisisitiza Dkt. Mkumbo
Amesema waraka wa Mkakati wa mabadiliko 2013 uliandaliwa na watu wanne tu bila Zitto Kabwe kujulishwa ingawa alikuwa mlengwa mkuu wa mkakati ambapo waandaji walipanga kumfuata na kumshawishi ajiunge.
Kwa upande wake Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amesema kwamba hatarajii kutoka ndani ya chama na hana mpango wa kuvunja chama chake kilichomlea na kumkuza miaka nenda rudi kwa sababu yeye ni muumini mwaminifu wa chama.
Amesema kuwa cha kushangaza ni waraka wa siri uliomuhusisha yeye na viongozi wa Chama cha Mapinduzi na wa Usalama wa Taifa kwamba anatumika kuhujumu chama chake na waraka huo ulisambazwa na viongozi wa juu wa chadema kama mkakati wao wa kumdhoofisha kisiasa kuelekea mbio za kugombea uongozi katika uchaguzi wa chama mwishoni mwa mwaka huu.
IMG_5241

Amesema sababu ya pili ni kuwakosoa viongozi wa Chadema yakutokupeleka hesabu za chama kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kamati kuu ilidai alipaswa kuwatonya kwanza kabla ya kwenda kwa umma na waandishi wa habari.
“dhamira yangu ilikataa na nitaendelea kusimamia ukweli kwamba hesabu za vyama vya siasa lazima zikaguliwe na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa fedha za Serikali kama sheria inavyotaka,” amesema
Zitto aliendelea kusema kuwa kama kuchagua kati ya chama na nchi yake atachagua nchi kwanza kabla chama na kwamba ataendelea na msimamo wake pia wa kukataa posho ya kukaa yaani (Sitting Allowance) kwa sababu analipwa mshahara na fedha za kujikimu. 
IMG_5252 

Mgogoro ndani ya Chadema ulipamba moto baada ya Kamati Kuu kuwavua uongozi Zitto Kabwe na Dk Kitila Mkumbo, huku Makamu Mwenyekiti Taifa, Said Arfi akiandika barua ya kujiuzulu Ijumaa ya wiki hii.
Zitto alivuliwa uongozi wa Naibu Katibu Mkuu Taifa na Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wakati Dk Mkumbo amevuliwa ujumbe wa Kamati Kuu. Wawili hao wanatuhumiwa kukisaliti chama.
Taarifa zilisema hoja ya kukisaliti chama pia ilimkumba Arfi akidaiwa kumwezesha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kupita ubunge bila kupingwa, katika uchaguzi mkuu uliopita na ndiyo sababu ya kuamua kuachia ngazi nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Taifa.
Mbali ya kuwavua uongozi Zitto na Dk Mkumbo, pia Kamati Kuu imewapa siku 14 wajieleze kwa nini wasifukuzwe uanachama. Kwa uamuzi huo Zitto amebaki na wadhifa wa ubunge wake wa Kigoma Kaskazini na wadhifa mwingine kwenye Kamati ya Bunge.
IMG_5274 

Kujiuzuru kwa Arfi
Makamu Mwenyekiti wa Taifa, Said Arfi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, Ijumaa ya wiki hii aliwasilisha barua ya kujiuzulu nafasi ya uongozi wa chama, akisema; “…kuchoshwa na unafiki unaoendelea ndani ya chama. Napenda ifahamike pia kwangu masilahi ya wapigakura, wakazi na wananchi wa Mpanda Mjini na Wilaya ya Mpanda ni muhimu katika kuwatumikia, hivyo basi sipo tayari kuchaguliwa marafiki.
Katika barua hiyo anasema amechochwa na tuhuma ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake kuwa alimsadia Waziri Mkuu Mizengo Pinda kupita bila ya kupingwa  katika uchaguzi wa ubunge katika uchaguzi mkuu uliopita.
“Kwa kipindi kirefu zimekuwepo shutuma dhidi yangu na kutiliwa shaka uhusiano wangu na Mhe Pinda Waziri Mkuu. Pamoja na kulijadili katika vikao kadhaa Mpanda na Dar es Salaam bado yapo mashaka kwa nini alipita bila kupingwa. Huo ulikuwa uamuzi wa Wanampanda kwenu imekuwa ni tatizo, lakini hamsemi kwa nini. Majimbo mengine 16 nchini yalipita bila kupingwa mlikuwa wapi na nani alaumiwe? Huu ni unafiki  wa kupindukia.
Vilevile, katika barua hiyo, Arfi anasema amechukizwa na kauli ya mwasisi wa chama hicho, aliyemtaja kwa jina moja la Mtei kuwachagulia marafiki.
“Aidha mmechukizwa sana kwa nini nilihoji kauli ya Mwasisi wa chama, Mhe Mtei kutuchagulia viongozi.  Naomba ifahamike wazi kwamba huu ni mtazamo wangu na utabakia hivyo siku zote kwa chama cha demokrasia kutoruhusu uongozi wa kiimla kwa kukidhi matakwa ya waasisi ambao huvigeuza vyama kuwa mali binafsi.
IMG_5324
IMG_5364
IMG_5365
IMG_5373
IMG_5398
IMG_5429
IMG_5417
IMG_5434

Mh.Zitto Kabwe akiongea na vyombo vya habari leo


1. Utangulizi
Katika kikao chake cha siku mbili kilichofanyika tarehe 20 - 22 Novemba 2013, Kamati Kuu ya CHADEMA, pamoja na mambo mengine, iliazimia kunivua nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama. Kwa mujibu wa taarifa ya chama iliyotolewa katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa tarehe 22 Novemba 2013, ilielezwa kwamba sababu za kuvuliwa uongozi mimi na Dk Kitila Mkumbo ni uhaini na hujuma kwa chama kutokana na waraka unaojulikana kama mkakati wa uchaguzi 2013. Ukweli ni kwamba waraka uliotajwa si sababu ya mimi kuvuliwa nafasi zangu za uongozi kama ilivyojadiliwa katika Kikao cha Kamati Kuu.

Sababu za kufukuzwa kwangu kama zilizojadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu ni tuhuma lukuki ambazo si mara yangu ya kwanza kuzisikia zikijadiliwa ndani na nje ya vikao vya chama. Hitimisho la tuhuma hizi ni kwamba mimi nimekuwa nikikisaliti chama kwa kutumika na CCM na Usalama wa Taifa. Nitazianisha tuhuma hizi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vyama.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI

Ninatambua kwamba chama changu kinapita katika wakati mgumu sana sasa hivi. Nataka nitamke mapema sana kwamba mimi Zitto Zuberi Kabwe sitokuwa chanzo cha CHADEMA kuvunjika. Hiki ndicho chama kilichonilea na kunifikisha hivi nilivyo. Ningependa chama hiki mtoto wangu atakapokuwa mtu mzima na atakapoamua kujiunga na siasa aingie CHADEMA. Bado nina imani kubwa na chama changu na ninaamini ndicho kinachostahili kuendesha nchi jana, leo na kesho.

2. Kuhusu tuhuma mbalimbali zinazo elekezwa kwangu

Zipo tuhuma nyingi ambazo zimekuwa zikirudiwarudiwa katika vikao vya chama na nje ya vikao na baadhi ya viongozi wenzangu. Tuhuma hizi zinalenga kuonyesha kwamba mimi ni mbinafsi na kwamba ninapokea rushwa ili kukihujumu chama changu. Nitazianisha tuhuma kwa kifupi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vya chama.

i) Tuhuma kwamba sikushiriki kumpigia kampeni mgombea wetu wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2010. Ningependa kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili:

  • Mimi nilikuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Kaskazini huko Kigoma.
  • Pamoja na kuwa mgombea wa ubunge, nilifanya kampeni katika majimbo mengine 16 katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Mtwara, Pwani, Shinyanga, Mara na Rukwa. Hakuna kiongozi yeyote wa juu aliyefanya kampeni katika majimbo mengi kama mimi, ukiacha mgombea urais.
  • Kote nilipopita nilimpigia kampeni wagombea wetu wa udiwani, ubunge na Rais.
  • Katika Mkoa wa Kigoma nilizunguka na mgombea urais katika kata zote za Kigoma Kaskazini na majimbo yote manane ya Mkoa wa Kigoma.
ii) Tuhuma kwamba katika Mkoa wa Kigoma nilishindwa kuwapigia kampeni wagombea wetu kiasi kwamba peke yangu ndiye niliyeshinda katika uchaguzi huo. Ukweli ni kwamba niliwapigia sana kampeni wagombea wetu, na hivyo ndivyo wapiga kura wa Kigoma walivyoamua.

iii) Tuhuma kwamba nilishiriki kuwashawishi wagombea wetu katika baadhi ya majimbo kujitoa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ili kuwapisha wagombea wa CCM wapite bila kupingwa kwa njia ya rushwa. Majimbo yanayotajwa ni pamoja na Sumbawanga, Musoma Vijijini na Singida Mjini. Kama nilivyokwisha kueleza katika vikao mbalimbali vya chama jambo hili si la kweli na hakuna popote ambapo watoa tuhuma hizi wamewahi kutoa ushahidi kwamba nilifanya jambo hili. Nipo tayari kwa uchunguzi ndani ya chama na watoa tuhuma waje na ushahidi bayana wa jambo hili. Si afya kwa chama kuendelea kurudiarudia tuhuma hizi kila mara tangu mwaka 2010 bila uchunguzi wowote kufanyika na jambo hili lifikie mwisho.

iv) Tuhuma kwamba nimekuwa sishiriki katika operesheni mbalimbali za chama: Ukweli ni kwamba nimeshiriki sana katika operesheni mbalimbali za chama ndani na nje ya nchi. Kwa mfano, mwaka 2011 tulikuwa na operesheni kubwa katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na nilikwenda katika mikoa yote tuliyotembelea. Mwaka 2012 baada ya hoja ya mkonge bungeni nilifanya ziara Mkoa wa Tanga. Mwaka 2012 kulikuwa na operesheni kubwa moja katika mikoa ya kusini ya Mtwara na Lindi. Operesheni hii sikushiriki kwa sababu nilikuwa nchini Marekani kufungua matawi kwa mwaliko wa Watanzania wanaoishi huko.

v) Tuhuma kwamba nimekidhalilisha chama kwa tamko la PAC kwamba Hesabu za Vyama hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG): Katika jambo hili ninatuhumiwa kwamba mimi kama Naibu Katibu nilipaswa kuwasiliana kwanza na viongozi wa chama 'kuwatonya' ili wajiandae. Kwamba kutokuwatonya kumekidhalilisha chama na kukiweka kundi moja na CCM na nastahili kuadhibiwa vikali kwa kuwa katika taarifa yangu nilikuwa na nia mbaya na chama chetu. Maelezo yangu niliyoyatoa na ambayo ningependa kuyakariri hapa kuhusu jambo hili ni kama ifuatavyo:

  • Utawala bora hautaki mimi kutumia nafasi yangu ya uenyekiti wa PAC kulinda chama changu na kuonea vyama vingine. Kufanya hivyo ni kuendeleza tabia zile zile ambazo tunazipinga na ambazo tunapigania kuzibadilisha
  • Napenda kusisitiza kwamba hakuna chama ambacho kimewahi kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). Natambua kwamba mahesabu ya chama changu yamekuwa yakikaguliwa na wakaguzi wa nje kwa utaratibu tuliojiwekea. Lakini matakwa ya kisheria ni kwamba mahesabu ya vyama vya siasa hayajakaguliwa na CAG, na hili ni kosa la kisheria, bila kujali kosa hili ni la nani.
vi) Tuhuma kwamba mimi ni mnafiki katika kukataa kwangu kuchukua Posho za Vikao
Mtakumbuka kwamba mimi nilikataa kuchukua posho tangu mwaka 2011 kama ishara ya kuonyesha kwa vitendo msimamo wa chama chetu wa kupinga posho za kukaa na matumizi mengine yasiyofaa katika fedha za umma kama ilivyoanishwa kwenye Ilani yetu ya mwaka 2010-2015. Mtakumbuka kwamba hivi karibuni Mheshimiwa Lema amenishutumu kwamba kukataa kwangu kuchukua posho ni unafiki kwa sababu ninapokea posho kubwa zaidi katika mashirika ya umma ambapo mimi ni mwenyekiti wa kamati husika. Ninapenda kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili:

  • Sipokei posho yeyote ya vikao (sitting allowance) ndani na nje ya Bunge tangu mwaka 2011. Hii ni pamoja na vikao vyote katika Kamati za Bunge ninavyohudhuria. Mtu yeyote mwenye ushahidi vinginevyo auweke hadharani.
  • Swala la kukataa posho (sitting allowance) ni swala la kiilani katika chama chetu, na kwangu ni swala la kimisingi zaidi. Katika Wilaya yangu vifo vya kina mama wajawazito ni 1900 kati ya wanawake 100,000 wenye ujauzito. Vifo hivi vinatokana na ukosefu wa huduma kwa sababu ya bajeti finyu. Ndiyo maana nilifurahi sana kwa chama chetu kuliweka swala la kupunguza matumizi ya Serikali katika Ilani, na kuondoa posho za wabunge, ambao tayari wanapokea mishahara mikubwa, kungesaidia sana kupatikana fedha ambazo zingeokoa vifo vingi vya kina mama.
  • Jambo hili si suala la ugomvi baina yangu na Mheshimiwa Lema. Ni suala la msingi katika chama chetu.
3 . Usambazaji wa Ripoti ya Siri kuhusu Zitto Kabwe
Hivi karibuni kulisambazwa waraka unaoitwa ripoti ya siri kuhusu mimi ukibeba lundo la tuhuma kwamba nimehongwa fedha nyingi ili kukihujumu chama changu. Waraka huu ulidaiwa kuwa umechomolewa kutoka makao makuu ya CHADEMA. Jambo hili pia lilijadiliwa katika kikao cha juzi kwa kifupi, na majibu ya viongozi wa chama ilikuwa ni kwamba waraka huu haukuandaliwa wala kusambazwa na makao makuu. Katika mchango wangu nililalamikia mambo matatu yafuatayo:

  1. Kwamba baadhi ya waliokuwa wanasambaza waraka ule walikuwa ni viongozi wa chama chetu. Bahati mbaya hadi leo hakuna hata mmoja ambaye amekwishachukuliwa hatua za kinidhamu. Ninaamini kwamba kuna siku watu hao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za chama chetu.
  2. Kwa kuwa chama kimekana rasmi kuhusika na waraka huu, nitaendelea na taratibu za kisheria ili kuhakikisha kwamba wote waliohusika kutengeneza hekaya ile wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria.
4. Hitimisho
Ninatambua kwamba kuna watu walitegemea leo ningejibu mapigo na ningewazodoa watu kwa majina kama ilivyo kawaida katika siasa za Tanzania. Natambua pia kwamba, kama ilivyo kawaida wakati wa migogoro katika vyama vya siasa hapa Tanzania, kuna watu walitegemea leo ningetangaza 'maamuzi magumu'. Natambua kwamba wapo ambao wangependa kupata nafasi ya kuendelea kutumia suala hili katika harakati zao za kudhoofisha mapambano ya demokrasia na uthabiti wa siasa za ushindani nchini mwetu. Napenda wanachama wa CHADEMA na wapenda demokrasia na siasa safi wote nchini watambue kwamba mimi bado ni mwanachama mwaminifu wa chama hiki na nitakuwa wa mwisho kutoka kwenye chama hiki kwa hiari yangu. Nitafuata taratibu zote ndani ya chama katika kuhitimisha jambo hili.

Naomba wanachama waelewe kwamba mimi kama binadamu ninaumia ninapopigwa. Tuhuma ninazorushiwa ni kubwa na zinanikwaza. Tuache siasa za uzushi ili tujenge chama chetu na nchi yetu, ili hatimaye tuwakomboe Watanzania wenye matarajio na imani kubwa kwa chama chetu.

Kama mwanasiasa kijana niliyekaa katika siasa kwa muda sasa yapo mengi mazuri nimeyafanya. Lakini kuna maeneo nilipojikwaa na yapo makosa niliyofanya kisiasa katika maisha yangu ya siasa.

Kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza demokrasia. Ni mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya wahafidhina, waumini wa uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu na wapenda siasa safi dhidi ya watukuzao siasa majitaka. Hii ni changamoto kubwa ndani ya chama chetu inayohitaji uongozi shupavu kuikabili. Nitasimama daima upande wa demokrasia. Kama alivyopata kunena mmoja ya wanasiasa maarufu, 'kiwango cha juu kabisa cha uzalendo katika nchi ni kukubali kutofautiana kimawazo', na ninatamani huu ndio uwe utamaduni wa chama chetu.


Kabwe Zuberi Zitto, Mb Dar es Salaam. 24 Novemba, 2013