Serikali
imesema kuwa visima vingi Jijini Dar es Salaam vimechimbwa bila ya
kufuata kanuni na taratibu za uchimbaji hivyo maji yake si salama kwa
matumizi ya binadamu.
Waziri
wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Mhandisi Gerson Lwenge aliyasema
hayo wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake Bungeni mjini
Dodoma.
Mhe.
Lwenge alibainisha kuwa katika kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa
Kipindupindu uliotokea mwezi Agosti 2015 Jijini Dar es Salaam na kuenea
nchini, Serikali ilifanya uchunguzi wa sampuli za maji ya visima 108 vya
jijini humo na matokeo ya uchunguzi huo yalionesha kuwa visima 66
maji yake si salama.
“Wizara
yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na wadau wengine ilifanya
ukaguzi na kupima uwepo wa vimelea vya vijidudu vya ugonjwa huo katika
visima vya maji vinavyotumika jijini Dar es Salaam na sampuli za maji ya
visima 108 zilichukuliwa, kati ya hivyo visima 20 vifupi na visima 46
virefu maji yake yaligundulika kuwa si salama. Kwa ujumla visima vingi
vilivyopo kwenye maeneo ya watu vimechimbwa bila ya kufuata kanuni na
taratibu,” alisema Mhe. Lwenge.
Aidha,
Waziri Lwenge alisema kuwa Serikali pia ilifanya ukaguzi wa ubora wa
maji kwenye vyanzo vya maji katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Mara,
Manyara, Kagera, Kigoma, Morogoro na Dodoma ambapo vyanzo vya maji
vipatavyo 600 vilikaguliwa na kubaini kuwa maji yaliyo salama ni chini
ya asilimia 40.
Mhe.
Lwenge alieleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Afya
Duniani (WHO) imekamilisha uandaaji wa miongozo ya utekelezaji wa Mpango
wa Usalama wa Maji (Water Safety Plan) kwa Vyombo vya Watumiaji wa Maji
na Mamlaka za Maji.
“Miongozo
hiyo inakusudia kuboresha huduma za upatikanaji wa maji safi na salama
kwa Mamlaka za Maji na Vyombo vya Watumiaji wa Maji Vijijini (COWSOs)
kuanzia kwenye chanzo cha maji hadi kwa mtumiaji,” alifafanua Mhe.
Lwenge.
Kutekelezwa
kwa mpango huo kutaboresha usimamizi wa usalama wa maji katika vyombo
hivyo na kuwaepusha wananchi kutumia maji yasiyo salama pamoja na
kupunguza upotevu wa maji katika mifumo ya kusambaza maji kote nchini.
No comments:
Post a Comment