UNAPOKUWA na kovu au makovu ni ushahidi kuwa palikua na kidonda, kwa
sababu ni hali ya kawaida kidonda kuacha kovu ingawa hutofautiana ukubwa
kulingana na ukubwa wa kidonda.
Makovu mengine hupotea baada ya siku kadhaa, mengine wiki, miezi,
mengine huchukua miaka kupotea na kuna mengine hayapotei kabisa
yanabaki siku zote. Kawaida kovu halina maumivu, kama kuna maumivu
basi bado ni kidonda na hakijapona, kovu huwa kama kumbukumbu tu lakini
isiyo na maumivu.
Kuna sababu nyingi zinazoleta vidonda vinavyoacha makovu. Kuna makovu
yanayoachwa na vidonda vilivyopatikana katika kujifunza, kujifunza vitu
kama vile wakati wa utoto unapojifunza kutembea ukaanguka na kuumia,
unapojifunza kuendesha baiskeli na mafunzo mengine. Bila kujifunza
huwezi kufahamu na katika kujifunza unakutana na vidonda vinavyoacha
makovu.
Makovu mengine yanapatikana katika kufanya yale unayopaswa kufanya
kama vile katika kazi unazofanya mfano kupika ukaungua, unajenga nyumba
ukaumia na kuna makovu yanapatikana kutokana na kusababishwa na watu
wengine, kusukumwa ukaumia, kupigwa na mambo yanayofanana na hayo na
mwisho makovu yatokanayo na vidonda ulivyopata wakati unamsaidia mtu.
Vidonda vya makovu haya yote vinauma, lakini kuna ambavyo maumivu
yanaishia mwilini na mengine yanaingia hadi rohoni, katika maisha yetu
ya kawaida pia tunakutana na kuumia kwingi, kunakoacha makovu ya aina
mbalimbali. Makovu mengine unayasahau baada ya muda mfupi, lakini
mengine hayaondoki kabisa.
Unaweza kuumizwa unapotafuta kazi ukatendewa jambo ambalo likakuumiza
sana lakini baada ya kupata kazi ukasahau kabisa, au ukaumia katika
masomo yako, hali ikawa mbaya lakini unapokuja kumaliza na kufaulu
unasahau yote.
Lakini kuna maumivu hasa ya kutendwa na mtu wa karibu sana kama
mchumba, kutengwa na ndugu, kuachwa baada ya kuvalishwa pete, kutendwa
na mume au mke, kufukuzwa kazi bila kosa na mengine ya aina hiyo ambayo
mara nyingi hukaa muda mrefu au hayaishi kabisa.
Katika haya yote unapaswa kuzingatia kuwa kovu halina maumivu.
Litakuwepo pale kukukumbusha kuwa ulipitia haya na sasa umevuka,
kukuonya kuwa usipite mahali fulani utaumia na kukutia moyo kuwa
yamepita na sasa ni mshindi na kwa imani tunasema umeshinda na zaidi ya
kushinda.
Kumbuka kovu halina maumivu ila ni kumbukumbu na si kizuizi katika
maisha yako, ingawa wapo watu wanaamini kutumia makovu kama kizingiti
ama kizuizi katika maisha yao. Nasema hivi kwa kuwa kuna ushahidi wa
baadhi ya watu ambao wameamua wenyewe kuacha makovu yawe vizingiti vya
kuwazuia kusonga mbele na kama kovu hilo ni maumivu, basi linadhihirisha
kuwa kidonda hakijapona.
Si siri wapo watu wamepitia machungu na maumivu makali sana katika
maisha yao, ambayo kiuhalisia wameachwa na makovu makali ambayo kwa
akili na uwezo wa kibinadamu, hayawezi kufutika na hivyo yanakuwa ni
kizingiti miaka na maisha yote. Unapofikia katika hatua hii, sijui imani
yako ni nini?
Lakini nasema unapofikia katika hatua hii ya kuendelea kuwa na kovu
lisilopona, basi mgeukie Mungu kwani ndio tabibu wa kweli akuponye
kidonda na kuondoa maumivu yote.
Kumbuka kidonda kilichopona kovu haliumi, kwa sababu kovu halioneshi
kesho yako itakuwaje ila linaonesha nyuma ulipitia nini, usikubali kuwa
mfungwa ama mtumwa wa makovu kwa sababu ukiruhusu hivyo umejiwekea
vizingiti vya kusongambele.
No comments:
Post a Comment