NA DK. CHALE
KUMEKUWA na hali fulani ambayo huwapata
baadhi ya wanawake hasa wa umri kati ya miaka ishirini na tano hadi
arobaini, kujihisi wagonjwa siku chache kabla ya kupata damu ya hedhi.
Hali hii huwafanya wanawake hawa wakapime presha kama imepanda au
imeshuka, mara wakapime malaria, lakini mwisho wa siku vipimo vyote
huonekana vipo sawa na akishapata tu damu ya hedhi kila kitu mwilini
mwake kinakuwa sawa.
CHANZO CHA TATIZO
Kama tulivyoona, tatizo hili la kujihisi mgonjwa kabla ya hedhi
Premenstrual Tension huwapata wanawake wenye umri wa miaka 25 hadi 40.
Hadi sasa chanzo halisi cha ugonjwa huu hakijajulikani ingawa kisayansi
inasadikiwa huwatokea wanawake wanapokuwa na kiwango kikubwa cha homoni
ya Progesterone na Estrogen kwenye miili yao hasa kipindi cha pili cha
mzunguko wa hedhi, yaani baada ya upevushaji wa mayai Ovulation.
Hali hii ya kuwa na kiwango kikubwa cha homoni hizi mwilini
husababisha kuongezeka kwa mgandamizo wa madini ya Sodium mwilini ambayo
hufanya mkusanyiko mkubwa wa maji mwilini na kufanya mwili uwe mzito na
kiwango hicho cha maji husababisha kuvimba kwa tishu za neva na hata
maji hayo hujikusanya hadi kwenye ubongo na kukuletea hali iitwayo
Cerebral Edema ambapo pia tishu za ubongo huvimba kipindi hicho.
JINSI MWANAMKE ANAVYOJIHISI
Baada ya hali hii kutokea, mwanamke huanza kujihisi mgonjwa na
atakuambia hajui hata nini kinamuuma, kichwa huuma sana, maumivu ya
mwili, mwili huchoka huhisi kichefuchefu, anakuwa mkali na hana raha,
kila sehemu ya mwili inauma, akili inakuwa haipo sawa, wakati mwingine
anashindwa kuendelea na kazi zake, hupatwa na msongo wa mawazo na
kujikuta anaweza hata kugombana na watu wake wa karibu.
Hali hii inapoanza kutokea huwa ni taratibu na kabla ya kupata damu
ya hedhi humtesa mwanamke takriban siku saba hadi kumi kabla hajaona
damu ya hedhi na hupotea masaa machache baada tu ya kupata hedhi na
kujikuta hajambo kabisa na kushangaa siku zote alizokuwa anaumwa.
UCHUNGUZI
Ni vigumu kugundua tatizo hili moja kwa moja kwani wengine hali hii
inapotokea huambatana na dalili nyingine kama maumivu ya mwili mfano
kiuno, mgongo, kichwa, miguu hata nyama za mwilini.
Pia wanawake wengine huhisi maumivu ya tumbo chini ya kitovu, kufunga
kupata haja kubwa, maumivu ya kifua, moyo kwenda mbio au kupatwa na ute
mzito ukeni. Kwa hiyo unapoona tatizo hili linakuandama kila mwezi,
basi ni vema umuone daktari wa magonjwa ya akina mama katika hospitali
ya rufaa ya mkoa ili ufanyiwe uchunguzi wa kina.
Kwa kuwa ugonjwa huu unafanana sana na magonjwa mengine kufuatana na
dalili zake, pia dalili zake zinachukua muda mrefu au siku saba hadi
kumi, basi unaweza kujikuta mara kwa mara unatibiwa tatizo ambalo siyo,
mfano unaweza kusikia mwanamke akilalamika kila mwezi anatibiwa malaria
au kila mwezi anatibiwa yutiai au mwingine taifoidi, basi ilimradi kila
mwezi unatibiwa ugonjwa huohuo usioisha.
Ugonjwa huu huchunguzwa kwa umakini kuzingatia historia ya tatizo na
vipimo kuangalia kiwango cha vichocheo au homoni hizo mbili za
Progesterone na Estrogen ambazo tumezitaja hapo awali. Pia kiwango cha
madini ya Sodium kitahakikiwa kwenye damu ili kujiridhisha na tatizo.
Baada ya hapo daktari atakushauri nini cha kufanya pamoja na matibabu ya
ugonjwa wako.
MATIBABU NA USHAURI
Inashauriwa unapokuwa na tatizo hili hakikisha unakuwa mtulivu,
jiweke kwenye hali ya usafi, hakuna ugonjwa ambao hauponi au haupati
nafuu. Maana kama hauponi na imethibitishwa na madaktari, basi kuna njia
ya mgonjwa kupatiwa nafuu.
Ugonjwa huu huwa unapona wenyewe pale mwanamke anapopata tu damu ya
hedhi na huanza tena siku saba hadi kumi kabla ya tarehe ya kuona damu
ya hedhi. Matibabu mengine yatatolewa kadiri daktari atakavyoona inafaa.
No comments:
Post a Comment