TTCL

EQUITY

Monday, December 14, 2015

Zanzibar kununua meli mpya 2

 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein alizindua meli mpya ya kisasa mv. Mapinduzi II juzi. Akizungumza katika uzinduzi huo amesema meli hiyo ni hatua muhimu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya kuimarisha usafiri wa baharini.
Dk Shein alibainisha pia kuwa ujenzi wa meli ni sehemu za hatua za serikali za “kulifanyia mageuzi makubwa Shirika la Meli na Uwakala Zanzibar ili liweze kujiendesha kibiashara kama mashirika mengine ya serikali yaliyofanyiwa mageuzi,” alisema.
Katika hotuba yake kwa wananchi na wageni waliohudhuria hafla hiyo, Dk Shein alieleza kuwa katika kuhakikisha wananchi wanakuwa na usafiri wa baharini wa uhakika, Serikali imedhamiria kununua meli nyingine mbili.
“Wakati tukizindua meli hii, nataka wananchi watambue kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba ina mpango wa kununua meli mpya ndogo inayolingana na mv Maendeleo na meli mpya ya mafuta,” alisema Dk Shein.
Alibainisha kuwa meli ya serikali ya mv Maendeleo iliyopo sasa itauzwa kwa kuwa ni ya zamani na kusisitiza kwa sasa serikali haitaruhusu tena meli iliyozidi umri wa miaka 15 kusajiliwa Zanzibar.
Awali katika maelezo yake Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, Dk Juma Akil alieleza kuwa gharama za meli hiyo ni dola za Kimarekani milioni 30.6 chini ya mkataba uliotiwa saini kati ya serikali na kampuni ya Korea Kusini ya Daewoo International na mbia wake Kampuni ya Posco Plantec Co. Ltd.
Alitoa maelezo ya kiufundi Dk Akil alisema meli hiyo ina urefu wa mita 90 na upana mita 17 na ina uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na tani 200 za mizigo ikiwemo magari 80 madogo au magari 50 makubwa.
Alibainisha kuwa meli hiyo ina uwezo wa kufanya safari za kutoka Zanzibar hadi Pemba kwa saa 4 wakati safari ya Zanzibar hadi Dar es Salaam inachukua saa 3.
Meli hiyo alieleza ina madaraja 4, daraja la tatu linalochukua abiria 800, daraja la kwanza abiria 350 na watu maalumu (VIP) abiria 50. Dk Akil aliongeza kuwa meli hiyo inatumia teknolojia rafiki wa mazingira ambapo ina mitambo ya kusafisha mafuta mazito ya kulainisha injini yaliyochafuka na kuyatumia tena.
Katika maelezo yake mafupi kumkaribisha mgeni rasmi, Waziri wa Fedha Omar Yussuf Mzee ambaye pia ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia ujenzi wa meli hiyo aliwashukuru wajumbe wote wa kamati walioshiriki hadi kufikia hatua ya kukabidhiwa meli hiyo.

No comments:

Post a Comment