Katika Waraka Elimu Namba 6 wa Mwaka 2015 kuhusu utekelezaji wa elimu
bure kwa shule za msingi na sekondari, wizara hiyo imetaja shule hizo
kuwa ni Shule ya Msingi Olympio (Dar es Salaam); Shule ya Msingi Diamond
(Dar es Salaam); Shule ya Msingi Oysterbay (Dar es Salaam); Shule ya
Msingi Iringa (Iringa) na Shule ya Msingi Mkapa (Mbeya).
Nyingine ni Shule ya Msingi Angaza (Mbeya); Shule ya Msingi Nuru
(Mbeya); Shule ya Msingi Lupilisi (Ruvuma); Shule ya Msingi Tanga
(Tanga); Shule ya Msingi Arusha (Arusha) na Shule ya Msingi Kisimani
iliyoko mkoani Arusha.
Wizara hiyo pia imesema waraka huo hauzihusu shule zinazomilikiwa na
mashirika ya umma ama taasisi za umma ambazo zinaendeshwa kwa taratibu
sawa na shule za binafsi. Katika waraka huo, wizara hiyo imetoa majukumu
yanayotakiwa kufanywa na Wizara hiyo, Tamisemi, wakurugenzi wa manispaa
na halmashauri ya wilaya, wakuu wa shule, bodi za shule, wazazi na
wananchi.
Majukumu ya wazazi na walezi Kuanzia Januari, wazazi wanatakiwa tu
kununua sare za shule na michezo, vifaa vya kujifunzia vikiwemo
madaftari na kalamu, na chakula kwa wanafunzi wa kutwa na kugharimia
matibabu kwa watoto wao.
Wanatakiwa pia kulipia nauli ya kwenda shule na kurudi kwa wanafunzi
wa kutwa na wanafunzi wa bweni wakati wa likizo; kununua magodoro,
shuka, vifaa vya usafi binafsi kwa wanafunzi wanaosoma shule za bweni na
wanaoishi katika hosteli zinazotumiwa na serikali; na kukemea na kutoa
taarifa kuhusu mienendo inayokwenda kinyume na elimumsingi bila malipo.
Wazazi na wananchi wengine pia wanatakiwa kuendelea kujitolea
nguvukazi na mali ili kuleta ustawi na maendeleo ya shule zilizoko ndani
ya jamii.
Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Katika waraka huo,
Wizara ina jukumu la kutenga fedha za kugharimia utayarishaji na
uendeshaji wa mitihani ya kitaifa kulingana na idadi ya wanafunzi;
kutenga fedha kwa ajili ya Uthibiti Ubora wa Shule na kutenga fedha za
kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utoaji wa elimumsingi bila malipo na
kuchukua hatua stahiki pale inapobidi.
Inachotakiwa kufanya Tamisemi Kwa upande wa Tamisemi, waraka huo
unaielekeza wizara hiyo kutoa miongozo ya matumizi ya fedha za umma kwa
wakuu wa shule, kuratibu uandaaji wa mipango na bajeti ili kupata
mipango na bajeti ya taifa kila mwaka inayozingatia mahitaji halisi ya
elimumsingi bila malipo.
Pia Tamisemi inatakiwa kufanya ukaguzi wa ndani, ufuatiliaji na
tathmini za mara kwa mara ili kuhakikisha elimumsingi bila malipo
inatolewa kwa ufanisi na viwango vya ubora inavyostahili.
Kuratibu utoaji mipango na bajeti za ruzuku ya uendeshaji wa shule
ikiwemo ulinzi, umeme, maji na ununuzi wa chaki na karatasi pamoja na
vifaa vingine vya kufundishia na kujifunzia.
Kutenga na kutuma fedha shuleni kwa ajili ya uendeshaji na usimamizi
wa mitihani na majaribio mbalimbali shuleni ikiwemo tathmini endelezi,
kununua vitabu, kemikali na vifaa vya maabara, samani yakiwemo madawati,
vifaa vya michezo, matengenezo ya mashine na mitambo pamoja na kujenga
na kukarabati miundombinu ya shule.
Kutenga na kutuma fedha shuleni za kugharimia wanafunzi wenye
mahitaji maalumu waliopo kwenye shule na vitengo vya elimu maalumu kwa
kuwapatia chakula yaani mlo mmoja kwa wanafunzi wa kutwa na milo mitatu
kwa wanafunzi wa bweni pamoja na vifaa na visaidizi.
Wakuu wa shule Waraka huo unawataka wakuu wa shule kuwapa maelekezo
wazazi kuhusu aina ya vifaa vinavyohitajika mfano rangi ya kitambaa cha
sare ya shule, sare za michezo, idadi na aina ya madaftari watakayotumia
wanafunzi ili wazazi wanunue wenyewe.
Pia wanatakiwa kusimamia na kuhakikisha fedha inayotolewa na Serikali
inatumika kama ilivyokusudiwa kulingana na taratibu za fedha za
Serikali na kutoa takwimu na taarifa sahihi za idadi ya wanafunzi na
mahitaji mengine ya shule.
Kamati au Bodi za Shule Wizara katika waraka huo inataka kamati za
shule kufuatilia na kusimamia matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali
ili ziweze kuleta tija; kuhakikisha kuwa sera, nyaraka, maelekezo na
miongozo ya Serikali inazingatiwa na kutoa ushauri stahiki.
Kuwashirikisha wazazi, walezi, walimu na wanafunzi katika maamuzi na
maazimio ya masuala mbalimbali yanayohusu maslahi na maendeleo ya shule
kwa ujumla.
Pia waraka huo umeainisha majukumu ya walimu ambao kazi yao kubwa ni
kusimamia sera na miongozo ya utoaji wa elimu bure. Wanafunzi ambao ndio
walengwa wakuu wa utoaji wa elimu pia wametakiwa kuhakikisha wanakuwepo
shule katika kipindi chote cha masomo.
No comments:
Post a Comment