MAWAZIRI wapya walioteuliwa na Rais John Magufuli wameshauriwa
kutekeleza majukumu yao mapya kwa kuguswa na matatizo ya Watanzania kama
anavyoguswa Rais na sio wafanye kazi zao kwa nidhamu ya woga.
Wakizungumza kwenye mdahalo wa kujadili hotuba ya Rais John Magufuli
aliyoitoa bungeni hivi karibuni, ambao umeandaliwa na Shirikisho la
Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (Tahliso), baadhi ya wasomi na wanazuoni
walisema mawaziri wanapaswa kufanya kazi zao kwa dhamira ya kweli kutoka
moyoni na sio kujionesha kwa Rais.
“Nawashauri wasifanye kazi kwa nidhamu ya woga, ila kama watafanya
kwa kuguswa na matatizo ya nchi kama ilivyo kwa Rais watafika mbali;
lakini kama wanafanya kwa nidhamu ya woga itakuwa ni nguvu ya soda,”
alisema mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest
Ngowi.
Profesa Ngowi alisema mawaziri wakishindwa kutekeleza majukumu yao
sio kwamba watakuwa wamemwangusha Dk Magufuli, bali watakuwa
wamewaangusha Watanzania ambao ndio wanahitaji matunda kutoka kwa
watendaji hao wakuu wa Serikali.
Alishauri pamoja na Dk Magufuli kuonesha dhamira ya kujenga reli,
barabara na bandari, lakini ni vyema akajikita pia katika ujenzi wa
miundombinu ya mawasiliano kwa kuwa dunia yote inaelekea huko.
Dk John Jingu alizungumzia hoja ya kujenga viwanda nchini kuwa
inawezekana kwani kuna nchi tajiri kama China zinatafuta kuhamisha
ujenzi wa viwanda kwenda nchi zingine na akashauri Tanzania kutumia
fursa hiyo kupitia sera ya mambo ya nje.
Pia alisema ujenzi wa viwanda utakuwa na faida kubwa iwapo ujenzi wa
miundombinu kama reli utawasaidia wakulima kufikisha bidhaa zao kwenye
masoko ya nje.
Alitoa mfano kuwa ujenzi wa reli kutoka Dar es Salama hadi Rwanda na
nchi zingine za Maziwa Makuu utasaidia upatikanaji wa masoko wa bidhaa
za alizeti inayolimwa katika mikoa inakopitia Reli ya Kati. Kwa upande
wa kodi, alisema Dk Magufuli ameanza vizuri katika eneo hilo, kwani nchi
inatakiwa kukusanya mapato yake ili wananchi wake ndio wapange
vipaumbele ya taifa.
Alisema nchi ikitegemea wahisani katika mapato yake itatekeleza pia
sera na vipaumbele vya wahisani hao. Kwa upande wake, Balozi Christopher
Liundi alisema Dk Magufuli ni kiongozi na zawadi kutoka kwa Mungu kwani
anachosema ndicho anachosimamia.
Alisema mawaziri wake ambao amewateua wanatakiwa waige kasi hiyo
katika utendaji wake, lakini pia wafanye kwa dhamira ya dhati ya
kuisaidia nchi.
“Mawaziri wakienda na kasi yake, Rais atapumua na atapata muda wa
kushughulikia matatizo mengine ya nchi,” alisema Balozi Liundi na
kuwataka Watanzania wamuunge mkono kwani kiongozi huyo sio malaika, bali
ni binadamu mbaye wakati mwingine anafanya makosa.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni aliyehudhuria mdahalo huo, Paul Makonda
alishauri mfumo wa elimu nchini ufumuliwe kwa maelezo kuwa unazalisha
watendaji wabovu ambao wanatoa huduma hafifu na za ovyo kwa wananchi.
Alisema watendaji wengi hawana ubunifu ambao unalenga kuokoa fedha za
umma. Alishauri pia viwanda vitakavyojengwa visaidie kupunguza tatizo
la ajira na akaonya kuwa kama Serikali haitakuwa makini wawekezaji
wanaweza kuleta viwanda; lakini kazi ikawa inafanywa na maroboti na
hivyo kutofikia lengo la utoaji wa ajira ambalo serikali inalenga.
Makonda aliyesema amehudhuria kama mwananchi na sio kama DC, alisema
Tanzania ni tajiri ila fedha nyingi zinazotengwa na Serikali kwa ajili
ya kuendesha miradi mbalimbali inaishia kwenye mifuko ya wananchi
wachache na akasema amelishuhudia Wilaya ya Kinondoni ambako barabara
nyingi zilizojengwa kwa lami ziko chini ya kiwango.
“Kwenye mapambano haya ya kupambana na rushwa, hata akifinywa baba na mama yako kaa kimya ili tuweze kufika,” alisema Makonda.
Chisaye Robert alisema busara za Dk Magufuli zibadilishwe ziwe sheria
ili hata akiondoka madarakani falsafa yake iendelee. Pia alimshauri
afumue mikataba ya madini na kuwepo na uwazi kwenye mikataba hiyo kuona
namna nchi inayonufaika.
“Namshauri pia awekeze zaidi kwenye elimu, sio kusomesha watu wengi,
bali kwenye ubora wa elimu inayotolewa kwenye vyuo vyetu vikuu ili
waweze kukidhi mahitaji ya soko ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki,”
alisema.
Awali mdahalo huo uliofunguliwa na Waziri wa Habari, Utamaduni,
Wasanii na Michezo, Nape Nnauye nusura uvunjike baada ya uongozi wa
Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupinga kufanyika
chuoni hapo kwa maelezo kuwa Tahliso inashindwa kusimamia masuala ya
wanafunzi hasa mikopo.
Walitaka kwanza Tahliso ishughulikie mikopo ya wanafunzi ambao
walisema wengi hawajapata katika vyuo mbalimbali na sio kuandaa mdahalo
wa kujadili hotuba ya Rais Magufuli ambayo itajadiliwa na wabunge.
Vurugu hizo zilizimwa na Nape ambaye aliwataka Daruso kama wana
malalamiko ya Tahliso kumaliza matatizo yao kupitia vikao.
“Kama mnaona viongozi wa Tahliso hawashughulikii matatizo yenu
waondoeni ila nawaomba tuache mdahalo huu ufanyike,” alisema Nape.
Alisema kama kuna wanafunzi ambao hawajapata mikopo, leo CCM itafuatilia suala hilo kwa kutuma mtu kwenye Bodi ya Mikopo.
“Bahati nzuri mimi bado ni Katibu Mwenezi wa CCM iliyoiweka serikali
madarakani, kwa hiyo hilo tutaenda kulifuatulia kujua kwa nini baadhi ya
wa
No comments:
Post a Comment