TTCL

EQUITY

Wednesday, December 2, 2015

Suala la usafi liwekewe mkazo

 
HIVI karibuni Rais John Magufuli aliamua kuwa Sherehe za Uhuru na Jamhuri, zitakazofanyika tarehe 9 Desemba mwaka huu, zitumike kwa kufanya kazi. Kwamba sherehe hizo zitumike kuchochea kujenga tabia ya kufanya kazi katika Taifa letu.
Rais alielekeza kwamba siku hiyo, Watanzania wote waitumie kwa kufanya kazi mbalimbali, kama vile shambani, ofisini, sokoni, viwandani na usafi wa miji yao katika kutimiza dhana ya “Uhuru na Kazi” kwa vitendo.
Rais alisisitiza kuwa sherehe hizo ni muhimu katika kuadhimisha kumbukumbu ya uhuru wa nchi yetu, hivyo zitaendelea kuadhimishwa kila mwaka kama kawaida kuanzia mwakani.
Tunaunga mkono hatua hiyo ya Rais, kwa sababu tuna hakika fedha zilizotengwa kwa ajili ya sherehe hizo, sasa zitatumika kwa ajili ya shughuli za kijamii, kama vile kupambana na maradhi, hasa kipindupindu, kununua dawa za hospitali na vitanda vya hospitali. Ni wazi hatua hiyo ya Rais Dk Magufuli, inaturejesha miaka kadhaa baada ya uhuru wa nchi yetu, ambapo kaulimbiu za sherehe hizo zilikuwa ni “Uhuru na Kazi” na “Uhuru ni Kazi”, ambapo Watanzania waliungana kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano.
Tunahimiza maadhimisho hayo ya mwaka huu, yaanze kwa kishindo kuanzia tarehe 1 Desemba mwaka huu hadi tarehe 9 Desemba, siku ya kilele. Jambo hili lifanyike kwa nguvu na umakini, hasa katika miji mikubwa, kama Dar es Salaam, Mwanza, Morogoro na Dodoma. Itakuwa ni fedheha kubwa, endapo jambo hilo litafeli na kisha itakapofika tarehe 9 Desemba, viongozi wa mikoa na wilaya, waanze kutoa visingizio vingi.
Tunamsihi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Mecky Sadiki ambaye alitangaza juzi kuwa kwa mkoa wake, usafi huo utakuwa endelevu, basi asimamie maneno yake; na atekeleze kweli kwa vitendo kauli yake hiyo. Tunasema hivyo kwa kuzingatia hali mbaya ya taka ngumu na majichafu katika mkoa huo.
Taka ngumu zimezagaa sokoni, viwandani, nyumbani, mitaani, vyuoni, shuleni, sehemu za burudani na maeneo ya wazi. Majitaka ni kero kubwa mitaani na majumbani. Magari ya majitaka, hayapiti kuzoa maji hayo machafu.
Vyoo vya nyumba nyingi mkoani Dar es Salaam vimejaa na kufurika kinyesi na majitaka, hivyo kutoa harufu kali. Vyoo hivyo havitolewi uchafu, bali hutapishwa tu kidogo mvua zinaponyesha. Hata mabwana afya, walioajiriwa na halmashauri za manispaa, hawapiti majumbani kukagua vyoo na usafi kama zamani, hivyo wenye nyumba wanafanya wapendavyo.
Mfano wa maeneo yenye vyoo vingi vilivyofurika uchafu ni Manzese, Tandale, Mburahati, Mabibo, Ilala, Kariakoo, Magomeni, Temeke, Buguruni na Vingunguti. Kote huko hakuna mabwana afya mitaani? Wapo tu ofisini!
Tuna imani, kupitia sherehe za mwaka huu, sasa Mkuu wa Mkoa atakutana na mabwana afya hao na kuwakumbusha wajibu wao. Watendaji wa kata, mitaa nao watimize wajibu wao kwa kuhakikisha maeneo wanayoyasimamia, yanakuwa safi muda wote ili kuepukana na magonjwa ya mlipuko.
Pia, watendaji wahimize wananchi wa maeneo yao, kutafuta vifaa vya usafi, badala ya kusubiri kuletewa na halmashauri. Pale itapobainika eneo fulani ni chafu, basi mtendaji wa eneo hilo, afikishwe katika vyombo vya sheria.

No comments:

Post a Comment