NOVEMBA 19 mwaka huu haikuwa siku nzuri kwa wafanyabiashara raia wa
China, wanaozalisha mabati nchini, katika maeneo mawili yaliyopo Tabata,
Dar es Salaam. Wafanyabiashara hao wanamiliki viwanda vya kuzalisha
mabati; Snow Leopard Building Materials Company Limited kilichopo
Segerea jijini humo na Red East Building Materials Company Limited.
Hawamiliki kampuni hizo pamoja, bali kila mfanyabiashara anamtaji
wake na kiwanda chake. Kwa maana hiyo viwanda hivyo viwili vinamilikiwa
na watu tofauti, ingawa makosa yao yanafanana, yaani kuzalisha mabati na
kuyaingiza sokoni bila kuthibitisha ubora. Haikuwa siku nzuri kwao kwa
sababu walibainika wakiendesha uzalishaji wa mabati na kuyauza kwa
wateja tofauti kiholela, jambo lililosababisha kufungwa kwa viwanda
vyao.
Timu ya maofisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), wakiongozwa na
Mkaguzi wa Shirika hilo, Inspekta Azizi Abdallah, ilifanya ukaguzi wa
kushtukiza katika viwanda hivyo siku hiyo na kujionea jinsi Sheria ya
Viwango Namba 2 ya mwaka 2009 inavyokiukwa na kuhatarisha usalama wa
wateja na mazingira. Walikuta uzalishaji ukiendelea huku wafanyabiashara
hao wazalishaji wakiendelea kuuza mabati kwa wateja waliofika viwandani
mwao kununua bidhaa hiyo.
Hata baada ya maofisa hao kujitambulisha na kuwaeleza kuwa walipaswa
kuacha kuzalisha mara moja hadi ubora wa mabati yao utakapothibitishwa
kuona kama uko sawa au la, waling’ang’ania kuwa wao wako sahihi na
wataendelea kuzalisha kwa sababu walikwisha wasiliana na shirika hilo la
viwango. Bila kumung’unya maneno, mwanamke mmoja raia wa nchi hiyo
aliyeonekana kushangazwa na hatua ya shirika la viwango kuwataka watoe
ushirikiano kwa kutoka nje ya kiwanda hicho ili kifungwe alisikika
akisema, “Sisi tunafuata sheria na tunaheshimu TBS.
Tumetuma mtu akaenda huko (Shirika la Viwango) na kutuletea leseni ya
TBS tunayoitumia kuzalisha mabati na kuyauza katika soko la ndani”.
Alisema na kuongeza, “Tena alitueleza gharama za kupata leseni ya ubora
kuwa ni Sh milioni tano na sisi tulimpa na akatuletea leseni
tunayoitumia kuendesha uzalishaji katika kiwanda chetu, sasa mkisema
mnafunga kiwanda tunashangaa.”
Kwa bahati nzuri, safu hii ilikuwepo kwenye viwanda hivyo wakati
shughuli ya kuvifunga ikiendelea, hivyo kusikia maelezo ya pande zote
mbili, yaani wafanyabiashara wenye viwanda na maofisa wa TBS, jambo
lililowezesha kugundua jinsi wafanyabiashara wa nje wanavyoshawishiwa na
Watanzania wasio waaminifu kutojali suala la ubora wa bidhaa, bila
kujua.
Wanadanganywa kwa kila njia na watu hao wanaojiita; watu wa kati,
madalali, warahisisha kazi ambao mara nyingi hudanganya wasiowafahamu
hasa wageni kuwa wanafahamiana na kila ‘mkubwa’ katika kila taasisi ya
serikali, lengo likiwa kujipatia fedha kwa njia za mkato, zisizo halali.
Kudanganya kwao kuhusu kufahamiana na wakubwa kunaelezwa kuwa na nia ya
kuonesha uwezo wao wa kutumia rushwa kama wanavyoiita ‘kitu kidogo’
kufanikisha mambo makubwa bila kufuata utaratibu uliowekwa.
Katika kiwanda cha Segerea, yaani Snow Leopard, mwanadada huyo
mfanyabiashara wa China alisisitiza kwa kujiamini kuwa huyo mtu wao
Mtanzania wanamuamini sana ndio maana hawakuwa na wasiwasi na uzalishaji
wao hata kwa kuhisi kuwa unawezekana ukawa unakiuka sheria za Tanzania
kuhusu viwango vya ubora. Pamoja na wenzake, waliomba maofisa wa TBS
waelekee kwenye ofisi yao wakaone ni kwa nini wanasema wanaleseni ya
ubora.
Sikubaki nyuma ingawa sikuwa ofisa wa shirika la viwango, nilifika
kushuhudia walichokuwa wakikionesha na kushangaa kama walivyoshangaa
maofisa wa shirika la viwango. Ilikuwa ni barua waliyoibandika vizuri
ukutani na kuitengenezea umaridadi ili isichafuke wala kuchanika
wakiamini kuwa ndio leseni ya ubora wa mabati yao kumbe ni barua
inayowaeleza kuwa wameruhusiwa kuendelea na taratibu nyingine za kupima
ubora wa mabati yao nchini, baada ya kufanikiwa kuingiza malighafi
kutoka nje.
Masikini! Mtanzania yule asiyemuaminifu alitumia kutojua kiingereza
kwa raia hao wa China kuwa ni mwanya wa kuwalaghai na kuwalia mamilioni
ya Shilingi. Hakuona sababu ya kuwaeleza ukweli kuhusu kilichokuwa
kimeandikwa kwenye barua ile yenye nembo na muhuri wa TBS, matokeo yake
kawasababisha wazalishe kiholela na kuingiza mabati yao sokoni kwa
kujiamini bila kujua kuwa walikuwa wakitenda kosa. Kwa sababu sheria ni
msumeno, utetezi wao haukusaidia.
Azma ya shirika hilo ilikuwa kuhakikisha wanapima ubora wa mabati
yao, hivyo kulazimika kufunga viwanda vyao kuzuia wasiendelee kuuza au
kuhamisha mabati yaliyokuwa tayari yamezalishwa. Maofisa wa TBS
walichukua sampuli ya mabati hayo na kuipeleka kwenye maabara ya shirika
la viwango ili ipimwe ubora na kutoa matokeo ambayo wahusika
wataelezwa.
Gladness Kasema ambaye ni Ofisa Masoko Mwandamizi wa Shirika la
Viwango Tanzania alisema kiwandani hapo kuwa, maelekezo ya nini
wafanyabiashara wazalishaji wa bidhaa na wauzaji wanapaswa kufanya
kukidhi matarajio ya shirika hilo hayauzwi wala kulipiwa hivyo
wasikubali kurubuniwa.
“Mfanyabiashara hapaswi kukubali kusikia maelezo yetu kupitia mtu wa
kati au mrahisisha kazi, aje mwenyewe ofisini atasaidiwa na kueleweshwa
ni nini afanye ili kuwa salama katika uzalishaji na uuzaji wake wa
bidhaa, hasakatika eneo la viwango vya ubora,”Kaseka anasema.
Anaongeza kuwa, mfanyabiashara raia wa wa nje, kama alivyo wa ndani
anapaswa kuambiwa ukweli kuhusu sheria na taratibu mbalimbali za
kuendesha biashara nchini, na si kudanganywa. Akiachwa azalishe zilizo
hafifu watumiaji wataumia na mazingira kuharibika.
No comments:
Post a Comment