Usimdharau mteja kwa kupungukiwa fedha
INAELEZWA kuwa dharau kwa mteja aliyepungukiwa fedha ya kununua
bidhaa au huduma kutoka katika duka au hoteli, baa na biashara nyingine
ni utovu wa nidhamu. Mtandao wa maswali, www. ask.com unasema, nidhamu
inayozungumziwa katika suala hilo ni ya biashara. Kwa mujibu wa mtandao
huo, mfanyabiashara anasahau kuwa mteja mwenye kiasi kisicho tosha
kununua chochote katika duka lake, anaweza kuwa ubao mzuri wa matangazo
ya biashara yake, ikiwa atahudumiwa kwa ukarimu.
Kutokana na maelezo ya mtandao huo, mteja wa aina hiyo, hasa kama
amefika kutafuta huduna au bidhaa husika katika duka la mfanyabiashara
anayemdharau, bila kuwa na lengo baya la kufanya kejeli ya bei, anaweza
kusambaza habari nzuri kuhusu nidhamu aliyoiona, hasa kama ataeleweshwa
ni kwa nini fedha zake hazitoshi na kutakiwa kurudi atakapopata kiasi
cha kuongezea.
“Badala ya kumdharau mteja wako kwa kumwacha kwenye kaunta ya duka
lako, eti kwa sababu ana fedha zisizotosha kununua bidhaa anayoitaka, ni
vizuri ukampa matumaini ya kuikuta kesho ili akaongeze fedha,”mtandao
huo unaeleza. Aidha, unaonya kuwa si wakati wote wateja wanakuwa
‘wamejaa’ fedha katika pochi au mifuko yao, kwa hiyo wafanyabiashara
hasa kwenye maduka makubwa na ya kati wanapaswa kujenga tabia ya
kuangalia tofauti ya gharama na kiasi cha bei walichokipanga kuona
endapo wanaweza kufanya liwezekanalo mteja asiondoke dukani bila bidhaa
aliyoifuata.
“Ni rahisi sana, kwa wateja wanaotaka faida kubwa kupita kiasi katika
bidhaa ambazo gharama zake si za juu kiais hicho, wanaweza kupunguza
kiasi cha bei walichokipanga na kuacha faida kidogo ili mteja mwenye
fedha zisizotimia aipate bidhaa anayoitaka,”www.ask.com inasema. Kwa
upande wa mtandao wa majibu, www.answers.com, ni afadhali kuingiza faida
ya wastani katika huduma na bidhaa, kuliko kuwafukuza wateja kwa
dharau, kwa sababu wamekosa kiasi cha fedha cha kutosha kununua bidhaa
kwenye duka lako.
Mtandao huo nao ulikuwa na maelezo yanayofanana na ule wa maswali,
kuhusu mteja aliyepungukiwa fedha kutumika kama ubao wa matangazo.
Wataalamu katika mtandao huo wanasema, kwa sababu ya kufurahishwa na
ukarimu wa muuza au mmiliki wa biashara, mteja aliyepungukiwa fedha
anaweza kusambaza ujumbe wa sifa kwa wengine kuhusu alichokiona au
alichotendewa.
“Lakini ikitokea kuwa mfanyabiashara amemfuuza mnunuzi kwa kuwa
amepungukiwa fedha, habari hiyo inaweza kusambazwa kwa haraka na
kuogopesha wateja wengine waliokuwa na nia ya kufuata huduma au bidhaa
kwenye duka hilo,”www.answers.com inasema. Kwa ufupi, mitandao hiyo
inashauri wafanyabiashara kuwachukulia wateja wote kuwa ni watu wa
muhimu, wanaosababisha biashara zao ziendelee kuwa hai.
Pia, www.ask.com inashauri wafnyabiashara kutangaza bei za bidhaa na
huduma zao kwa kutumia njia ambazo wateja wengi watapata taarifa
kuzihusu, hivyo kuepuka kufika dukani na kuanza kushangaa bei. Pamoja na
hilo, www.ask.com inaeleza kuwa ni vizuri wafanyabiashara hususan wa
bidhaa wakajiwekea utaratibu wa kuzingatia utamaduni wa watu wa maeneo
wanakofungua biashara kuepuka kuwakwaza na kuwakimbiza.
Unataja baadhi ya utamaduni ambao baadhi ya watu katika maeneo
mbalimbali wanauendekeza kuwa ni pamoja na kuomba kupunguziwa bei ya
vitu wanavyokuwa wamekwenda dukani kuvinunua. Inaelezwa na wataalamu hao
wa biashara kutoka katika mitandao hiyo kuwa, ni kawaida kwa watu wa
maeneo fulani kuomba kushushiwa bei,hasa ya bidhaa za vitu katika maduka
ya kawaida ambapo bei za bidhaa hizo hazijabandikwa mahali popote
kuonesha kuwa hazipungui.
“Sasa inapotokea kuwa mfanyabiashara anataka kuendana na wateja wake
waliozoea kushushiwa bei ,ni lazima apeleke dukani bidhaa zikiwa na bei
iliyoongezwa kiasi ili litakapokuja ombi la kupunguza aondoe kiasi hicho
kilichozidi”,mtandao huo unasema. Hata hivyo, mtaalamu huyo anasema
kiasi hicho ‘cha juu’ hakipaswi kuwa kikubwa wala hakistahili kuongezwa
ikiwa tayari bei ya bidhaa husika imekwisha fanywa ya juu. “Faida si
lazima ipatikane yote kwa mara moja kwa kunyonya wateja.
Ikiwa gharama za biashara hiyo ni za wastani, kwa kuzingatia uwezo wa
wanunuzi kifedha, na kiasi cha faida kinachotakiwa, muuza au mmiliki wa
duka anaweza kuamua kuweka bei za wastani pia”www.ansk.com inasema.
Zaidi, mtandao huo unasema kuwa, kunahatari kwa biashara kukosa wateja
endapo mfanyabiashara ataamua kung’ang’ania bei za juu apate faida zaidi
ya mara mbili.
Maelezo kutoka kwa wataalamu hao yanaonesha umuhimu wa
fanyanyabiashara kujali na kuthamini wateja bila kujali wanafedha nyingi
au pungufu. Siamini kama mteja anaweza kutoka alikotoka na kufika
dukani kununua bidhaa anayofahamu kuwa inauzwa bei ya juu asiyoimudu.
Wakati mwingine wauzaji wanafanya uamuzi wa bei bila kufanya utafiti
kuona wauzaji katika maduka mengine wanatoza bidhaa au huduma husika kwa
kiasi gani.
Sikatai kuwa bei katika soko huria hutegemea gharama ambazo
mfanyabiashara amezitumia kununua bidhaa au kuandaa huduma anayouza,
lakini, ni lazima kuwe na utaratibu wa kupanga bei si kujifanyia mambo
kiholela. Mtaalamu katika www. answers.com anaweka bayana kuwa , wauzaji
wengine wanapandisha bei ya bidhaa na huduma papo kwa papo kulingana na
aina ya wateja wanaofika kuiulizia.
Tabia hiyo inatajwa kuwa chanzo kimojawapo cha kusababisha biashara
iendeshwe kwa harasa kwa sababu wateja wanapogundua ‘ubabaishaji’ huo
hukimbia. Wengi wanaofanya hivyo huwa wauzaji waliokosa uaminifu
wasiohofu kuwadhihaki wateja hasa wanaposhindwa kumudu gharama
wanazowatajia.
No comments:
Post a Comment