JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limesema ajali za
barabara zimepungua hadi 7,570 kwa kipindi cha Januari hadi Novemba
mwaka huu ikilinganishwa na ajali 13,466 zilizotokea kwa kipindi kama
hicho mwaka jana.
Kamanda wa kikosi hicho, Mohamed Mpinga aliyasema hayo jana Dar es
Salaam wakati akikabidhi gari kwa mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Jackson Kapongo aliyejinyakulia gari aina ya Toyota surf lenye
thamani ya zaidi ya Sh milioni 24 katika shindano lililochezeshwa na
Kampuni ya kuuza magari ya Enhance Auto.
Alisema katika ajali hizo, vifo vilipungua kutoka 3,437 mwaka jana
hadi kufikia vifo 3,195 mwaka huu huku majeruhi wakipungua kutoka 13,495
mwaka jana hadi 8,566 mwaka huu.
Kamanda Mpinga alisema ajali hizo zimepungua kutokana na elimu ya
usalama barabarani inayoendelea kutolewa kwa wananchi ambapo kwa wastani
wa ajali za kila mwezi zimepungua kutoka zaidi ya 1,000 kwa mwaka jana
na chini ya 1,000 kwa mwaka huu.
Alisema mara nyingi kipindi cha kuelekea Sikukuu za Krismasi na Mwaka
Mpya ajali nyingi zaidi hutokea na kusababisha vifo na majeruhi na
kuwataka wananchi kuyatumia magari yao vizuri na kuzingatia sheria za
usalama barabarani ili kuepukana na ajali hizo.
“Tatizo kubwa la ajali za barabarani ni mwendokasi, magari mabovu,
ulevi na kupita gari la mbele bila tahadhari hivyo tufuate sheria za
usalama barabarani ili tuepukane na ajali hizi,” alisema.
Akizungumza kampuni hiyo, Mpinga alisema imekuwa ikichezesha shindano
hilo kila mwaka na kushirikisha nchi mbalimbali Afrika ambapo kwa mwaka
jana mshindi alipatikana kutoka Zambia, lakini kwa mwaka huu ameshinda
Mtanzania hivyo ni jambo la kujivunia.
Alisema mbali na kutoa zawadi, lakini kampuni hizo za magari zina
jukumu kubwa la kutoa mchango kwa usalama barabarani kwa kutoa elimu
sambamba na kuuza magari yenye viwango vinavyokubalika ili kuepusha
ajali zisizo za lazima.
“Natoa mwito kwa kampuni zingine kuwekeza katika usalama barabarani
na wasifikirie tu kuuza magari bali wahakikishe magari yanakuwa salama
na wanaoendesha wanakuwa salama... tuagize magari yenye viwango maana
ajali nyingi pia zinasababishwa na ubovu wa magari,” alisema.
Mapema Mkurugenzi wa Enhance Auto, Aatif Farooq Butt alisema mshiriki
alitakiwa kushiriki kwa kuchagua mitandao yao ya kijamii kwa wingi
zaidi na lilishirikisha nchi ambazo wanafanya nao biashara ikiwemo
Botswana, Burundi, Jamhuri ya Congo, Malawi, Msumbiji, Sudan Kusini,
Uganda, Zambia, Zimbabwe na Tanzania.
No comments:
Post a Comment