TTCL

EQUITY

Thursday, December 3, 2015

Makonda asimamisha uzalishaji Urafiki



 Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.

MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, ameagiza usimamishaji shughuli za uzalishaji katika Kiwanda cha Nguo cha Urafiki kilichopo jijini Dar es Salaam hadi pale matatizo kati ya mwajiri na wafanyakazi yatakapopatiwa ufumbuzi.

Pia Makonda alishangazwa na hatua ya uongozi wa kiwanda hicho kukimbia ofisi wakati wafanyakazi wake wakiwa katika mgomo, huku akihoji kuwa watakimbia ofisi zao hadi lini.

Akizungumza mara baada ya kufika eneo hilo huku akiwa ameongozana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camilius Wambura, alitoa agizo la kusitisha shughuli za uzalishaji na kuahidi kulipekeleka suala hilo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Bishara kwa maamuzi zaidi.
"Ndugu zangu nakumbuka tumeshafanya mazungumzo mara kadhaa juu ya stahiki zenu na tulikubaliana na uongozi wenu kwamba ifikapo Desemba mosi, mwajiri ataanza kulipa viwango vipya vya mishahara yenu, lakini hadi kufikia leo (jana) hajalipa sasa nawaahidi suala hili napeleka kwa katibu na Jumatatu nitarudi hapa saa mbil asubuhi kuwapa majibu,"alisema Makonda.

Alisema Jumatatu ataenda kiwandani hapo kwa ajili ya kuwapa majibu na juu ya hatua zingine zitakazofuata. Alitaka wafanyakazi hao washikamane na asitokee hata mmoja akawageuka kwa kurudi kiwandani hapo na kufanyakazi.

Pia Makonda alisema wafanyakazi hao walitakiwa wafahamishwe kinachoendelea kwa maana walishakaa vikao vingi kwa ajili ya kuzungumzia maslahi yao na walifikia makubaliano ya kuwalipa. Alisisitiza kuwa mwajiri huyo alitakiwa kuwalipa deni la sh. bilioni tisa, lakini hawajalipwa hadi leo.

Makonda alilitaka Jeshi la Polisi kuacha kutumia nguvu kwa kutumia mabomu kama njia ya kushughulikia matatizo ya watu, kwani kufanya hivyo kunaweka historia mbaya kwa vizazi vijavyo.
"Kulikuwa hakuna haja ya kutumia mabomu kwani hawa watu wazuri ambao wakiambiwa wanasikia kwani awali waliwahi kugoma kwa siku nne, lakini nilipofika na kuzungumza nao walikubali na kurudi kazini, hivyo hata ninyi mlitakiwa kutumia njia mbadala ya mazungumzo na si kutumia mabomu,"alisema Makonda.

Kabla ya kufika Makonda, Jeshi la Polisi lililazimika kutumia mabomu kwa lengo la kutawanya wafanyakazi hao ambao walikuwa wamefunga mageti ya kiwanda hicho na kutoruhusu mtu yeyote kuingia wala kutoka hadi pale mkuu wa wilaya atakapofika.

Awali akizungumza na Majira kwa sharti la kutotaja jina mmoja wa wafanyakazi hao alisema wanalipwa mshahara wa sh.100,000 kabla ya makato na kwamba wanataka walipwe 150,000 na posho 65,000 lakini mwajiri hataki. 

No comments:

Post a Comment