TANGU aingie madarakani Novemba 25, mwaka huu, Rais John Magufuli
amefanya mambo makubwa hasa kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi yake na
kaulimbiu aliyoitumia katika kipindi cha kampeni ya ‘Hapa Kazi Tu’.
Kauli hiyo sasa inayojibainisha kuwa maana yake ni kuwa na Serikali
itakayowabijika na kuhakikisha inawaletea maendeleo wananchi,
itakayopambana na ufisadi, rushwa na ubadhirifu lakini pia inayomaanisha
kuwa Tanzania sasa itakuwa ni taifa la wachapakazi na si vinginevyo.
Imekuwa ni kawaida kwa viongozi wengi wa siasa duniani ikiwemo
Tanzania, pale wanapowania nafasi za juu wakihitaji kura za wananchi,
hutoa ahadi nyingi lakini matokeo ya utekelezaji wa ahadi hizo, mara
nyingi yamekuwa hayafikii kile walichoahidi.
Hata hivyo, hali imekuwa tofauti kwa Magufuli ambaye sasa ni Rais wa
Serikali ya awamu ya tano, baada ya kumpokea kijiti, Rais mstaafu Jakaya
Kikwete, kwani siku chache tu alipoingia Ikulu alianza kazi kwa kasi
iliyoonekana si Tanzania pekee bali duniani kote.
Kiongozi huyo, mbali na kupiga marufuku safari holela za nje kwa
maofisa waandamizi wa serikali, alifanya ziara ya ghafla katika ofisi
nyeti ya nchi ambayo ni Wizara ya Fedha na kisha akaenda Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili ambako kote hakuridhishwa na kasi ya utendaji na
kuchukua hatua zilizolenga kuboresha utendaji na kuongeza kasi ya
uwajibikaji.
Katika Hospitali ya Muhimbili, alilazimika kubadili uongozi kutokana
na uozo aliokuta ambao ni pamoja na wananchi kukosa huduma za msingi za
tiba, mashine muhimu za vipimo kushindwa kufanyakazi kwa muda mrefu
lakini pia hali ya malazi ya wagonjwa kutokuwa ya kuridhisha.
Dk Magufuli hakuishia hapo, kwani mara baada ya kutembelea ofisi hizo
nyeti na kubadili hali ya utendaji hasa utolewaji wa huduma, aliamua
kuhakikisha anapunguza matumizi yasiyo ya lazima na fedha zinazopatikana
kupelekwa katika maeneo muhimu yenye mahitaji.
Katika kutekeleza dhamira yake hiyo, aliagiza fedha zilizokusanywa
kwa ajili ya hafla ya kufungua Bunge la 11 takribani Sh milioni 250
sehemu kubwa ya fedha hizo itumike katika kununulia vitanda vya wagonjwa
Hospitali ya Muhimbili na kiasi kidogo kilichobaki, ndio kitumike
kufanyia hafla hiyo.
Mwishoni mwa wiki, baada ya kuchaguliwa kwa Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa, kiongozi huyo naye kwa kasi aliyonayo, Rais Magufuli alifanya
ziara ya ghafla katika bandari ya Dar es Salaam na kukuta madudu
yaliyosababisha kusimamishwa kazi kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) Rished Bade.
Pamoja na Bade pia walisimamishwa kazi wafanyakazi wengine watano wa
mamlaka hiyo na Mamlaka ya Bandari (TPA) kwa tuhuma za uzembe, ufisadi
na rushwa.
Mwingine aliyesimamishwa ni Kamishna wa Kodi na Forodha, Tiagi
Masamaki. Baadhi ya maofisa hao bado wanashikiliwa na Polisi kwa
mahojiano zaidi. Ukweli ni kwamba kwa kasi hiyo, ya Dk Magufuli na
uongozi wake, ni wazi kuwa Watanzania sasa wanatarajia kuona ufanisi
mzuri kutoka kwa watendaji wa Serikali yao, ikiwa ni pamoja na kupata
huduma bora ambazo hapo awali zilishindikana kutokana na uhaba wa fedha.
Naamini kuwa huo bado ni mwanzo wa utendaji wa Serikali hiyo, kwani
bado zipo idara nyeti zinazohitaji kukaguliwa kwa jicho la tatu kama
ilivyofanyika Muhimbili, Hazina na TRA ambako pia madudu yatafichuliwa
bila shaka na hivyo, kuondokana na watendaji wanaoendekeza kujinufaisha
wenyewe.
Ni wazi kuwa, kasi hiyo ya Dk Magufuli imeamsha ari kwa wananchi na
kuwazindua wavivu, wategaji, wabinafsi, mafisadi na wala rushwa ambao
sasa watafanyakazi kwa ajili ya kunufaisha taifa na si matumbo yao.
Ni wazi kuwa Watanzania wanatakiwa kuendelea kumuombea kiongozi huyo
na menejimenti yake yote, ili azidi kufanyakazi kwa bidiii kwa manufaa
ya Watanzania kama alivyosema mwenyewe kuwa, kwa sasa anahitaji maombi
kwa kuwa kazi ya kutumbua majipu si ndogo.
No comments:
Post a Comment