SIKU moja baada ya Rais John Magufuli kuamuru fedha zilizotengwa kwa
ajili ya sherehe za Uhuru zikajenge barabara ya Bagamoyo kipande cha
kilometa 4.3 cha Mwenge – Morocco, jijini Dar es Salaam, ujenzi huo
umeanza jana.
Gazeti hili lilishuhudia tingatinga mbili mali ya kampuni ya
ukandarasi ya Estim katika eneo la Mwenge, yakisafisha eneo la barabara
hiyo, ikiwa ni maandalizi ya upanuzi, kama maagizo ya Rais yalivyosema.
Dk Magufuli juzi aliamuru fedha zilizopaswa kutumika kugharamia
sherehe za Sikukuu ya Uhuru ambazo zingefanyika Desemba 9, mwaka huu,
kutumika kufanya upanuzi wa barabara hiyo ya Mwenge hadi Morocco kwa
kuongeza njia mbili za barabara za lami.
Aidha, tayari fedha hizo Sh bilioni nne zimepelekwa kwa Wakala wa
Barabara (TANROADS) kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hilo, ambalo
limeanza kutekelezwa mara moja kupitia mkandarasi huyo, Estim wa jijini
Dar es Salaam.
Dk Magufuli alimuagiza Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale
walipokutana Ikulu Dar es Salaam juzi, kuwa ujenzi wa barabara hiyo
uanze haraka ili kukabiliana na adha ya msongamano wa magari katika
barabara hiyo.
Mmoja wa wasimamizi wa ujenzi huo kutoka kampuni ya Estim ambaye
hakutaka kutaja jina lake, alipohojiwa na gazeti hili kuhusu kuanza kwa
ujenzi huo na utachukua muda gani, alisema taarifa zote zipo Tanroads.
Hata hivyo, jitihada za kumpata Mfugale hazikuzaa matunda baada ya
kutafutwa mara kadhaa kwa simu na kuambiwa kuwa yupo kikaoni na
wasaidizi wake walisema yeye ndiye mwenye taarifa kamili.
No comments:
Post a Comment