Wapiga Kura Kibamba Wamtaka Mnyika Kuanza Kufanyia Kazi Ahadi Zake Badala Ya Kuendelea Kutoa Matamko Kwenye Vyombo Vya Habari
Wakazi
wa jimbo la kibamba wamemtaka mbunge wao, John Mnyika kuanza kufanyia
kazi ahadi zake badala ya kuanza kutoa matamko kwenye vyombo vya habari
kuzungumzia mambo ya kitaifa wakati ana mambo kadhaa ya kuyafanyia kazi
jimboni kwake.
Wakiongea na mwandishi wa Dar24,
wakazi hao wamesema pamoja na kushukuru sana kwa kupewa jimbo jipya
ambalo limegawanywa kutoka lililokuwa jimbo la Ubungo, wanatarajia
mbunge wao huyo, ambaye kwa kipindi kilichopita pia alitumika katika
eneo hilo atakuwa na eneo dogo la kulifanyia kazi hivyo kuwaletea
maendeleo kwa kutatua kero zao.
Mkazi kibamba aliyejitambulisha kwa jina la Rashid Uledi maarufu kama ‘Mzee wa Ukawa’ alisema
“Mnyika si mgeni na matatizo ya Kibamba kwani hili lilikuwa ni eneo
lake alipokuwa mbunge wa Ubungo. Hivyo hatutegemei kumwona akitumia muda
mrefu kuongelea mambo ya kitaifa badala ya kushughulikia kero zetu.”
“Tunamtaka
Mbunge wetu arudi jimboni kukaa na sisi ili atueleze mikakati aliyonayo
na pia muda wa kuanza kutimiza ahadi alizotuahidi badala ya kuanza
kulalamikia suala la ofisi aliyopewa kuwa ndogo. Hivi sasa kipaumbele
chake kiwe kero zetu badala ya kufikiria kuanza kukaa ofisini,” alisema Mwanaisha Swedi akiwa katika sehemu yake anayofanyia biashara ya kuuza vitafunio.
"Tunamtaka
mbunge wetu aache kulalamikia suala la ofisi, aje atuambie nasi tuna
uwezo wa kumjengea ofisi kubwa katika eneo hili. Tunamtaka aje aungane
nasi kujikwamua kwenye matatizo yetu ya kiuchumi na kimiundo mbinu" alisema Jerome Munishi ambaye alijitambulisha kuwa ni mkazi wa mbezi mwisho.
Kwa
ujumla wakazi wa kibamba wanamtegemea mbunge wao kuacha kuwa mbunge wa
matukio na vyombo vya habari kwa kutoa matamko kila jambo la kitaifa
linapotokea.
Maelezo
ya wakazi hao wa Kibamba yamejikita katika kile wanachoamini kuwa muda
wa siasa umepita hivi sasa ni bora akaelekeza nguvu zake katika kufanya
kazi kwa kushirikiana na wapiga kura wake.
No comments:
Post a Comment