Shirika
la Umeme Nchini (Tanesco) limetakiwa kuandaa mpango madhubuti wa
utitirishaji maji kutoka kwenye bwawa la Nyumba ya Mungu ili kuwepo na
maji ya kutosha kuzalisha umeme kwenye vituo vya Hale na New Pangani.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alitoa agizo hilo
wakati wa ziara yake katika mabwawa ya kuzalishia umeme ya Hale na
Pangani yaliyoko mkoani Tanga na bwawa la Nyumba ya Mungu la mkoani
Kilimanjaro.
Agizo
hilo alilitoa baada ya kujionea namna ambavyo kina cha maji kwenye
mabwawa ya Hale na Pangani kimepungua kutokana na mipango hafifu ya
utiririshaji maji kutoka bwawa la Nyumba ya Mungu ambalo ni chanzo
kikuu cha upelekaji maji katika mabwawa hayo yaliyoko mkoani Tanga.
Profesa Muhongo alisema wananchi wanatarajia umeme usiokatikakatika, umeme wa kutosha na wa bei nafuu.
“Nimeamua
kufanya ziara katika vyanzo vyote vya uzalishaji umeme nchini ili baada
ya hapa tuangalie jinsi tutakavyoboresha hali ya uzalishaji umeme na
wananchi wetu wapate umeme wa uhakika na wa bei nafuu,” alisema Profesa Muhongo.
Meneja
wa Kituo cha kuzalisha umeme wa maji wa Pangani, Mhandisi John Skauk
alisema kuwa mitambo ya Hale ilifungwa mwaka 1964 ikiwa na uwezo wa
kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 21 ambapo kila mtambo (kati ya
mitambo miwili) katika kituo hicho una uwezo kuzalisha umeme wa kiasi
cha megawati 10.5.
Aliongeza
kuwa ukarabati wa kwanza wa mitambo hiyo ulifanyika mwaka 1986 na kuwa
ilipofika mwaka 2008 mtambo mmoja uliharibika na hivyo kusababisha
mtambo mmoja tu kufanya kazi hadi sasa.
Akionekana
kukasirishwa na taarifa hiyo, Profesa Muhongo alihoji ni kwanini
ukarabati wa mtambo huo umechukua muda mrefu na na kuagiza mtambo huo
kufungwa haraka ili uweze kuzalisha nishati ya umeme.
Profesa
Muhongo pia alisisitiza kufanyika kwa ukarabati wa mara kwa mara wa
mitambo ya uzalishaji umeme huku akielezea kuwa kuchelewa kwa ukarabati
wa mitambo hiyo ni sababu mojawapo ya matatizo ya umeme nchini.
Kwa
upande wa kituo cha uzalishaji umeme cha New Pangani ilielezwa kuwa
mitambo iliyopo ina uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 68 hata hivyo
kutokana na upungufu wa maji kwenye bwawa la Pangani mitambo hiyo
inazalisha megawati 17 hadi 50 kwa siku.
"Mitambo
hii ya Pangani iko vizuri haina hitilafu yoyote isipokuwa tu ni suala
la kutopata maji ya kutosha kutoka kwenye chanzo kikuu ambacho ni Nyumba
ya Mungu," alisema Mhandisi Skauk.
Aidha,
akizungumzia Kituo cha Nyumba ya Mungu, Mhandisi Skauk alieleza kuwa
kituo kinao uwezo wa kuzalisha jumla ya Megawati nane hata hivyo kiasi
hicho hakijafikiwa kutokana na utiririshaji mdogo wa maji hivyo kwa sasa
kinazalisha Megawati 3.7.
“Tunashindwa
kutiririsha maji ya kutosha kwa sababu tukifanya hivyo tutasababisha
mafuriko kwenye baadhi ya maeneo ambapo maji hayo yanapita,” alisema.
Akizungumzia
kwa ujumla suala la uzalishaji umeme kwa kutumia maji, Profesa Muhongo
alisema kuwa changamoto ya uzalishaji umeme wa maji nchini inatokana pia
na mabwawa mengi kujengwa kwa kutumia teknolojia ya zamani hivyo
Serikali imedhamimiria kuwa na vyanzo vingi zaidi vya kuzalisha nishati
hiyo ya umeme mbali na maji.
"Lazima
tuwe na vyanzo vingi, umeme upatikane, usikatikekatike. Tunafanya
tathmini ya vyanzo vyote tuone uzalishaji wake, ziara hii ni muhimu
kwani bila kufanya hivi nisingejionea kwamba kuna mtambo haufanyi kazi
tangu mwaka 2008,” alisema Muhongo.
Alisema
alichokiona Kanda ya Kaskazini ni kuwa maji yapo ya kutosha isipokuwa
hakuna mipango madhubuti ya kutiririsha maji kutoka kwenye chanzo kikuu
hadi kufika kwenye mabwawa ya uzalishaji umeme ya Hale na Pangani.
"Habari
ya kuwa mnawaambia wananchi kwamba huku hakuna maji sio sahihi. Maji
yapo isipokuwa hakuna mipango mizuri ya mtiririko wa maji kutoka Nyumba
ya Mungu kwenda Hale na Pangani," alisema.
Alisema
vyanzo vya umeme wa maji nchini vinapaswa kuzalisha Megawati 561 lakini
umeme unaozalishwa kwa njia hiyo kwa sasa si zaidi ya Megawati 110
ambayo ni sawa na asilimia 20.
"Hili
suala la maji linatia aibu; tunataka tutathmini ndani ya siku kumi
tubaini wapi tuongeze nguvu zaidi, Tanesco inapaswa iingie gharama ya
kutengeneza miundombinu ya maji," alisema Profesa Muhongo.
Aliliagiza
Shirika hilo la Umeme kufanya kikao na Bodi ya Bonde la Pangani ili
kuandaa mpangilio mzuri wa kuruhusu maji kutoka bwawa la Nyumba ya Mungu
hadi Hale na Pangani bila kuleta uharibifu kwa kuwa wananchi pia
wanahitaji maji hayo kwa matumizi mbalimbali.
Aliagiza
kikao hicho kifanyike tarehe 15 mwezi huu (Jumanne) asubuhi na
makubaliano ya kikao yapelekwe Wizara ya Nishati na Madini na wakuu wa
wilaya wa maeneo husika ili hatua zichukuliwe haraka.
No comments:
Post a Comment