KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndg. Nape Nnauye |
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amesema vyama vya upinzani vitaendelea kuwa wasindikizaji wa CCM katika chaguzi mbalimbali zitakaofanyika nchini kutokana na wananchi wengi kuendelea kukiamini chama hicho.
Aidha amesisitiza kuwa Katiba Inayopendekezwa itapita kwa kishindo wakati wa Kura ya Maoni itakayofanyika Aprili 30, mwaka huu, pamoja na kelele na shinikizo la vyama vya upinzani kutaka wananchi kususia upigaji kura wa Katiba hiyo.
Nape aliyasema hayo katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Chamwino, wakati Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alipofanya ziara wilayani humo katika mwendelezo wa ziara yake ya kuutembelea Mkoa wa Dodoma.
Akizungumzia ushindi wa chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao wa udiwani, ubunge na urais, Nape alisema hakuna siri kuwa vyama vya upinzani vitaendelea kuisindikiza CCM ili kushinda viti vingi vya udiwani, ubunge na kushinda kwa kishindo kwenye uchaguzi wa urais.
“Ndugu zangu nataka niwaeleze wazi kwamba vyama vya upinzani ni kama mpambe wa Bwana Harusi, ambaye pamoja na kufanya shughuli zote za usaidizi na upambe kwa Bwana Harusi lakini safari yake huishia sebule maharusi wanapofika nyumbani” alisema Nape.
Alisema tayari ishara ya ushindi wa CCM imeonekana katika uchaguzi wa serikali za mitaa, ambapo CCM imeshinda kwa kishindo kwa kunyakua viti vingi kwenye vitongoji, mitaa na vijiji, huku vyama vya upinzani vikiambulia ushindi katika baadhi ya maeneo.
“Nataka niwaambie wazi, wananchi wa nchi hii bado wana imani kubwa na CCM, ukiona kuna mtu anakipenda chama cha upinzani ujue anasumbuliwa na ushamba tu na si kitu kingine. Sisi tumezunguka nchi nzima na tumegundua wakati CCM inazidi kuimarika na kupanda juu, vyama vya upinzani vinazorota na kushuka chini, wenye macho na walione hili” alisena Nape
No comments:
Post a Comment