Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu.
Mwandishi Wetu, Morogoro
WATUHUMIWA wawili Zuberi Thabiti
(30) na Iddy Adamu (32) wanaodaiwa kushirikiana kufanikisha tukio la
kumbaka na kumdhalilisha binti mkulima (jina limehifadhiwa), mkazi wa
Kata ya Dakawa, wilayani Mvomero, mkoani Morogoro, wamekatwa na kohojiwa
na jeshi la polisi mkoani humo.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya tukio
hilo la kinyama usiku wa Mei 4, mwaka huu katika nyumba ya kulala wageni
iitwayo Titii iliyoko Dakawa ambapo Zuberi aambaye ni dereva, mkazi wa
Mbarali Mbeya anadaiwa kumbaka binti huyo huku Iddy ambaye ni mkulima,
mkazi wa Makambako akirekodi picha za video kwa kutumia simu yake ya
mkononi.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, baada
ya kurekodi katika simu yake, baadaye Iddy alizituma picha hizo kwa mtu
aliyefahamika kwa jina la Rajabu Salehe (26), mkazi wa Dakawa ambaye
naye alizisambaza picha hizo katika mitandao mbalimbali ya kijamii kwa
watu mbalimbali.
Taarifa ya polisi imeeleza kuwa, chanzo
cha tukio hilo ni kwamba, binti huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na
Zuberi ambapo siku hiyo mtuhumiwa alimpigia simu binti huyo na
kumwambia aende katika nyumba hiyo ya wageni.
Taarifa hiyo ya polisi imezidi kueleza
kuwa, baada ya kufika katika chumba husika ndipo Iddy alipoingia kisha
kumtaka binti huyo afanye atakachomuelekeza huku akimshikia kisu ili
asipige kelele na baada ya kutekeleza ukatili huo (ubakaji), walimtaka
asitoe siri hiyo vinginevyo atauawa.
Aidha, baada ya tukio hilo kuripotiwa
kituo cha Polisi Dakawa Apliri 5, mwaka huu, polisi walianza uchunguzi
mara moja ambapo walifanikiwa kuwakamata jumla ya watuhumiwa 11 wakiwemo
Zuberi na Iddy pamoja na walioshiriki kuzisambaza picha hizo za
udhalilishaji ambao ni;
Rajabu Salehe (26), Saidi Athumani
(26), Musini Ngai (36), Saidi Mohamedi (24), John Peter (24), Hassani
Ramadhani (27), Ramadhani Ally (26), Lulu Peter (38) na Magreth Njonjome
(30), wote wakazi wa Dakawa ambapo kwa pamoja wamefunguliwa shitaka la
PICHA ZA UTUPU (PONOGRAFIA) chini ya kifungu cha 14 (1) (a) cha sheria
ya makosa ya mtandao.
Taarifa hiyo ya polisi pia imeeleza kuwa
jeshi hilo linaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine huku jeshi hilo
likitoa onyo kwa wananchi wote kuwa makini na matumizi ya mitandao ya
kijamii kwa kutoshiriki makosa ya uhalifu wa kimtandao kwani sheria
itachukua mkondo wake.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu leo alikemea suala
hilo bungeni na kueleza masikitiko yake makubwa kwa watu hao kutekeleza
unyama huo na kusisitiza kuwa watuhumiwa hao wafikishwe mahakamani
haraka.
No comments:
Post a Comment