“Nchi yetu ni kama
nyumba mpya. Nchi change sawa sawa na nyumba mpya. Mmeijenga vizuri
mmetayarisha msingi, mkaijenga mkaimaliza. Mnafurahi. Ndipo mnaridhika
nyumba imara, inapendeza. Lakini haijasukumwa. Haijatikiswa. Mara
unatokea mtikisiko, ile nyumba inatikiswa.
“ Ule mtikisiko
utawaonyesheni sehemu mbovu za nyumba ile. Ilikuwa kwanza mnaiona yote
ni nzuri, inapendeza. Lakini, kama unakuja msukumo wa mtikisiko wa
kutosha kabisa, sasa ndipo mtakapoanza kuona maeneo mabovu ya nyumba ile
na kutokea nyufa. Nyingine ndogo katika paa, kama ilikuwa ni nyumba
imara, nyufa nyingine ndogo zaidi katika paa, nyingine katika dari,
hata linta lililokuwako huenda likaanguka chini.
“Lakini, kama
mtikisiko ulikuwa mkubwa, mnaweza kukuta nyufa hata katika msingi: hata
msingi wenyewe nao umepata nyufa! Sasa, mtakachotaka baada ya hapo,
baada ya kuona hivyo, mambo mawili yanaweza kutokea. La kwanza ni kwamba
ule mtikisiko utakwisha: hautakuwapo.
“ Sasa baada ya hapo
mtafanya nini? Mtaziba zile nyufa: mtaziba. Mtaziona sehemu mbovu:
mtaziba vizuri sana. Kama zilikuwapo katika paa mtaziba kwenye dari,
mtaziba mtatengeneza vizuri. Eh! Zilizoharibika haribika, hizo
mtazitengeneza vizuri; zilikuwapo nyufa katika msingi, mtatengeneza
sana, hasa zile katika msingi. Maana zile ndizo muhimu sana.
“Na
nyumba baada ya hapo itakuwa imara sana. Ilikuwa haijapata mtikisiko
ninyi mlidhani ni imara, lakini ilikuwa haijapata mtikisiko. Sasa
imepata mtikisiko mmeziona zile nyufa zake. Zile sehemu mbovu mbovu zake
mmeziona, sasa; mkizitengeneza, nyumba itakuwa imara. Ikiwa mtikisiko
umekwisha, mtapata nafasi ya kutengeneza.
“Linaloweza kutokea
jingine ni kwamba mtikisiko ule utaendelea. Ukiendelea, itabomoka. Hata
ingekuwa imara kiasi gani, itawabomokeeni madhali imekwisha kuonyesha,
hata katika msingi, kuna nyufa. Kama tikisiko lile likiendelea,
itabomoka. Ndivyo ilivyofanyika Kobe juzi juzi Ujapani. Lile
halikumalizika. Kama lingepita mara moja tu, ‘vupu’ Kobe isingalikwisha.
Lakini liliendelea, yakaanguka majumba mengi sana .
Mwalimu J.K. Nyerere; Nyufa (1995)
|
No comments:
Post a Comment