Zanzibar kuelimishwa Polisi Jamii kudumisha amani
KAMATI ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imependekeza
elimu ya Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi iendelee kutolewa visiwani
humo ili wananchi wengi waweze kuifahamu na kuitekeleza kwa vitendo kwa
lengo la kudumisha amani na utulivu.
Kamati hiyo yenye wajumbe tisa inayoongozwa na Mwenyeketi wake, Hamza
Hassan Juma, imetoa mapendekezo hayo katika kikao chake kilichoketi
juzi jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said
Mwema.
Taarifa ya Jeshi la Polisi nchini iliyotolewa na Msemaji wake, Advera
Senso, ilieleza kwamba wajumbe hao wameliomba pia jeshi hilo kutosita
kuwachukulia hatua za kisheria wote wanaochochea vurugu.
Wamemwomba IGP Mwema kuendelea kuboresha makazi ya askari polisi
yaliyopo Zanzibar ili kuwafanya askari hao waishi katika mazingira
mazuri yanayowawezesha kufanya kazi zao bila bughudha.
Wamependekeza pia kuendelea kuboresha masilahi ya watendaji wa jeshi
hilo ili yaweze kuendana na hali halisi ya maisha, kwa kuwa kazi
wanayoifanya ni kubwa na inapaswa kuungwa mkono.
Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Alli Mussa,
amesema wataendelea kuboresha makazi ya askari kwa kutumia rasilimali
zilizopo pamoja na kuwashirikisha wadau wengine wa ndani na nje.
Katika kikao hicho wadau hao wameazimia kukutana mara mbili kwa mwaka
kwa upande wa Zanzibar na mara moja kwa Tanzania Bara kwa lengo la
kuweka mikakati ya kuimarisha usalama nchini pamoja na kufanya semina
za mara kwa mara kwa lengo la kujifunza dhana nzima ya Ulinzi
Shirikishi na Polisi Jamii.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Kamishna wa Polisi, Utawala na
Rasilimali, Kamishna wa Polisi (CP) Clodwig Mtweve, Kaimu Katibu Mkuu
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Agustino Shio, Mkurugenzi Msaidizi
kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano, Lupi Mwaikambo na maofisa
wakuu waandamizi wa Jeshi la Polisi Makao Makuu.
No comments:
Post a Comment