CHADEMA yalisulubu Bunge
WANASHERIA wameunga mkono msimamo wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) na wale wa NCCR- Mageuzi kupinga hatua ya Ofisi ya
Bunge kuliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata wabunge wake ili wakahojiwe.
Wakizungumza na Tanzania Daima, mwanasheria mashuhuri hapa nchini na
wakili wa kujitegemea, Mathew Kakamba, alisema ni kinyume cha sheria na
ni matumizi mabaya ya madaraka kwa Ofisi ya Bunge kutumia polisi
kuwakamata wabunge katika masuala yanayolihusu Bunge.
Wanasheria hao walitoa maoni yao kuhusiana na mvutano mkubwa wa
kisheria uliozuka baina ya CHADEMA na Ofisi ya Bunge ambayo imeagiza
kukamatwa kwa wabunge kadhaa wa upinzani ili wakahojiwe na Kamati ya
Haki, Kinga na Maadili ya Bunge, ambayo CHADEMA wanadai kuwa haipo.
Wakili Kakamba katika maoni yake alisema ni makosa kisheria kutumia
nguvu za mhimili mwingine katika kuendesha masuala yanayohusu mhimili
wa pili.
“Kuna mgogoro unaojulikana kwa Watanzania karibu wote kuhusiana na
vurugu zilizotokea katika mkutano wa Bunge lililokwisha, na kuvunjwa
kwa kamati za kudumu za Bunge.
“Pamoja na kuvunjwa kwa kamati hizo, bado kama sikosei, wajumbe wake
hawajateuliwa na kwa maana hiyo, kisheria utendaji wake haujaanza. Kwa
lugha nyingine, haziwezi kuitwa kamati rasmi kwa sababu hazina
wajumbe,” alisema Wakili Kakamba.
Kauli ya Wakili Kakamba imeungwa mkono na wakili mwingine, Aloyce
Komba, ambaye amekiita kitendo cha Ofisi ya Bunge kutumia polisi
kuwakamata wabunge wao wa upinzani kuwa ni udhalilishaji mkubwa na
uvunjaji wa haki za binadamu.
Komba anayetoka Kampuni ya Uwakili ya Haki Kwanza, alisema Bunge ni
chombo kinachojitegemea na linazo sheria na kanuni zinazopaswa kutumika
kumlazimisha mbunge kutimiza agizo la wito.
“Masuala yote ya Bunge yanatakiwa kuendeshwa kibunge bila kutegemea
vyombo vingine vya nje, labda tu ikiwa kuna mwingiliano kutoka katika
mhimili mwingine.
“Si sahihi kwa spika kutumia polisi kuwakamata wabunge wakati wanazo
kanuni na taratibu nzuri tu, na sidhani kama ni utaratibu mzuri na
unaolenga kudumisha demokrasia.
“Mbunge akishindwa kufika, kwani hakuna sheria nyingine hata za
kuzuiwa kuhudhuria vikao kadhaa vya Bunge, hadi leo wanataka kutumia
polisi kuwakamata?” alihoji Komba.
Akizungumzia uhalali wa kamati hizo, Komba ambaye ni mtaalamu wa
sheria katika mambo ya utawala, alisema kimsingi hazipo, kwa sababu
tangu kuvunjwa kwake na kuundwa nyingine, bado spika hajateua wajumbe wa
kamati mpya.
“Hajateua wajumbe wa kamati hizo, na ni sawa kabisa kuwa hazipo. Sasa
wanaitwa kuhojiwa na kamati gani? Mtazamo wa kisheria ni kwamba
hazipo.
Alikwenda mbali zaidi na kuilaumu Ofisi ya Bunge kwa madai ya kuvunja
haki za msingi kwa sababu aliyetendewa kosa ni spika (kiti),
anayelalamika ni spika, mteuzi wa kamati ni spika na ushahidi mwingi
utatoka kwa spika, hivyo kupingana kabisa na haki za sheria ambazo
mlalamikaji hapaswi tena kuwa mwendesha mashitaka.
Hata hivyo, mawakili hao walikubaliana na kuwataka wabunge wote
waliopata barua za wito kutoka Ofisi ya Bunge kuitikia na si kukaidi.
“Pamoja na kasoro hizo, kama wameitwa na Ofisi ya Bunge, wanatakiwa
kwenda na si kugoma. Huko ndiko mahali pekee wanakotakiwa kuwakosoa hao
wakubwa, na hata wanao uwezo wa kukataa kuzungumza hata kama kamati
yenyewe ingekuwa hai kisheria,” walisema wanasheria hao.
CHADEMA wagoma
Juzi Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa alimwagiza Mnadhimu
wa Kambi ya Upinzani Bungeni kuiandikia barua Ofisi ya Bunge ya
kukataa wabunge wake kukamatwa na polisi ama kuhojiwa na kamati
waliyodai ni hewa, kwa kuwa zilizokuwapo zilivunjwa na Spika Anne
Makinda katika kikao kilichoisha mwezi uliopita.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Dk. Slaa alisema kisheria,
kanuni na taratibu za Bunge, kamati ambazo zimeshavunjwa haziwezi
kufanya kazi yoyote kwa kuwa ni batili mpaka hapo zitakapoundwa kamati
nyingine.
Alilitaka Bunge kurejea kanuni za kudumu za Bunge namba 113 (7),
inayozungumzia ukomo wa uhai wa kamati za Bunge, uhai wake unaishia
Mkutano wa Kumi wa Bunge ambapo inakuwa ni nusu ya kwanza ya uhai wa
Bunge lenyewe.
Dk. Slaa alisema kutokana na kifungu hicho, inaonesha dhahiri kwamba
Spika Anne Makinda na wasaidizi wake wana matumizi mabaya ya sheria,
kutoifahamu vizuri ama kulewa madaraka, hali ambayo CHADEMA
haitakubaliana nao.
Hivyo alisema Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge ambayo
ilikuwa chini ya Mbunge wa Mlalo, Brigedia mstaafu Hassan Ngwilizi
(CCM), haitawahoji wabunge wake kwa kuwa imekwisha kumaliza kazi yake
tangu Februari 8, mwaka huu.
Msimamo wa CHADEMA unakuja zikiwa ni siku mbili tangu Ofisi ya Bunge
kupitia Katibu Mkuu, Dk. Thomas Kashililah, itumie Jeshi la Polisi
kuwataarifu baadhi ya wabunge wa chama hicho kuwa wanahitajika jijini
Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano na kamati hiyo.
Katibu Mkuu huyo alisema kama wabunge wa CHADEMA wanaitiwa kuhusu
vurugu zilizotokea bungeni Februari 4, mwaka huu, tayari zimeshatolewa
hukumu yake kwa kuwataja wahusika kuwa ni Tundu Lissu (Singida
Mashariki), John Mnyika (Ubungo), Paulina Gekul (Viti Maalumu) na
Joshua Nassari ( Arumeru Mashariki).
Alisema katika hukumu hiyo ambayo ilisomwa na Spika Makinda ilikuwa
ya upande mmoja wa kamati yenyewe iliyokaliwa na wabunge wa CCM ambao
waliwaona wabunge wa CHADEMA pekee ndio waliofanya vurugu huku
ikishindwa kuwaita wahusika kwa mahojiano.
Aidha, alisema hata kama kamati ya Brigedia Ngwilizi ingekuwa hai,
wabunge wake wasingeitii, kwa kuwa tayari imekwisha kuwahukumu.
Hata hivyo Dk. Slaa alitumia nafasi hiyo kumtaka Spika Makinda kwenda
kozi kwa ajili ya kujifunza sheria za kuongoza Bunge kutokana na
kushindwa kwake katika kipindi chote alichokalia kiti hicho.
“Nasikia Spika Makinda huwa anasema kuwa niwafundishe wabunge wangu
sheria, kanuni na taratibu za Bunge kwa kuwa nazifahamu vizuri, kwani
yeye na wanasheria wake wanafanya nini? Kupoka kwake sheria na
taratibu za bungeni ndizo zinazosababisha vurugu?” alihoji Dk. Slaa na
kuongeza:
“Nataka nimwambie kwamba wakati nipo bungeni, maspika waliokuwa
wakiongoza Bunge akiwamo Samuel Sitta walikuwa wakijua kuongoza, kwa
kufuata sheria na kanuni zake na ndiyo maana hakuna vurugu zilizokuwa
zikitokea na si yeye.”
Aidha, alisema maspika hao walikuwa wanajua kwamba mabunge yote ya
Afrika na yale ambayo Tanzania inaiga kutoka kwao yana sheria na
taratibu zinazowaruhusu kushangilia hata kuzomea kwa kutaja chama chao
na si hivi ambavyo Spika Makinda anavyofanya.
Lissu anena
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Lissu alisema kwa mujibu wa sheria
na kanuni za Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge, zinamtaka
Katibu Mkuu wa Bunge Dk. Kashililah kuandika barua hizo kwa niaba ya
Spika Makinda lakini hakufanya hivyo.
Lakini pia Lissua alisema hata barua ya polisi (police message)
waliyopewa si taarifa tosha ya kujipeleka wao kuhojiwa bali walipaswa
kupelekewa taarifa ya kuitwa kwa ajili ya mahojiano na Bunge.
Kutokana na maelezo hayo Lissu alisema hakuna jambo lililofuatwa
kisheria, hivyo hakuna watakayemwona, na alidai kuwa tayari hukumu yao
ilishatolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Brigedia Ngwilizi Februari
8, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment