Haki ya kukata rufaa ni ya kila mshtakiwa
MARA baada ya kusikiliza ushahidi au maelezo yalitolewa na pande
mbili zinazopingana mahakamani, mahakama huandaa hukumu ili kuhitimisha
mgogoro uliopo mbele yake kwa kubainisha upande upi wenye haki juu ya
madai.
Hukumu ya kesi ya madai ni sharti iwe na mambo muhimu na ya msingi
kama maelezo mafupi na fasaha kuhusiana na shauri husika, masuala au
mambo yaliyokuwa yakibishaniwa na pande mbili katika mgogoro ulioko
mahakamani - ambayo mahakama imeombwa kuyatolea uamuzi, uamuzi juu ya
masuala au mambo yaliyopo mbele ya mahakama, na sababu ambazo
zimeisababisha mahakama kutoa uamuzi huo.
Mara baada ya hukumu kuandaliwa na hakimu au jaji aliyesikiliza
shauri husika, ni sharti isomwe kwenye mahakama ya wazi, ambapo mtu
yeyote anaweza kufika na kusikiliza ikisomwa.
Lakini katika baadhi ya mashauri, hasa yale yanayohusisha watoto
wadogo, mahakama yaweza kuyasikiliza na kusoma hukumu katika mahakama
isiyokuwa ya wazi, au chemba kama wengi walivyozoea kuita.
Amri ya mahakama
Amri ni maelezo rasmi ya mahakama yenye kutoa uamuzi wa mwisho
kuhusu haki ambayo pande mbili zinazopingana mahakamani zinadaiana.
Amri ya mahakama ni muhtasari wa hukumu ya mahakama kuhusiana na shauri
husika, na inapaswa kuwa na jina la mahakama iliyotoa hukumu hiyo,
namba ya shauri lililofikishwa mahakamani, majina na maelezo ya
mdai/mdaiwa katika shauri husika, maelezo ya madai na nafuu inayooombwa
katika shauri husika, gharama halisi zilizotumiwa katika shauri
husika, na tarehe, sahihi ya jaji au hakimu aliyeitoa, na mhuri wa
mahakama iliyotoa amri hiyo.
Ziko aina mbalimbali za amri ya mahakama, ikiwa ni pamoja na kukaza
hukumu/amri kwa kurejeshewa fedha anazodai mdai, kiasi cha fedha
kilichoonyeshwa na mdai katika hati ya madai ndicho kitakachorudishwa
kwa mdai; kukaza hukumu/amri kwa kurejeshewa mali inayohamishika, kama
magari au thamani za maofisini au nyumbani; na kukaza hukumu/amri kwa
kulipwa fidia ya pesa badala ya kurejeshewa mali iisyohamishika.
Nyingine ni kukaza hukumu/amri kwa kumilikishwa mali isiyohamishika na
kulipwa fidia ya kodi, kama mali hiyo ilikuwa inazalisha faida.
Kwa mfano nyumba ya kupangisha - mdai anapewa uwezo wa kukusanya kodi
ya nyumba au kodi ya aina yoyote ile toka kwenye mali ya mdaiwa hadi
atakapokuwa amemaliza dai lake.
Mfano anaweza kuchukua kodi ya nyumba hadi hata miaka miwili kutegemea aina ya deni na nyumba anayoipangisha.
Hukumu/amri nyingine ya mahakama ni inayotolewa kwa kuvunja
makubaliano ya ubia. Kama ni biashara iliyokuwa inaendeshwa kwa ubia
mahakama itatoa amri kuivunja na wakati mwingine hata kutoa amri ya
kugawana au kuuza mali.
Kwa kawaida, hukumu/amri ya mahakama hukazwa na mahakama
iliyoitoa. Tuseme kama ni mahakama ya wilaya ndiyo ilisikiliza kesi
hadi ikatoa hukumu basi ndiyo itakayotoa amri ya kukaza hukumu.
Hata hivyo, mahakama nyingine yaweza kupokea maombi ya kukaza hukumu
iliyotolewa na mahakama nyingine na ikasimamia kukazwa kwa hukumu/amri
hiyo, kutegemea na mazingira ya shauri moja hadi jingine, na pia
kutegemea mali za mdaiwa ziko katika mamlaka ya mahakama ipi.
Utaratibu wa kuhamisha ukazaji wa hukumu/amri kutoka mahakama
iliyoitoa hadi mahakama nyingine ni kwamba mdai ataomba mahakama
iliyoitoa hukumu/amri hiyo iihamishie katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
katika mahali ambapo anaomba hukumu/amri ikazwe.
Nayo Mahakama ya Hakimu Mkazi ambapo hukumu/amri hiyo imehamishiwa
yaweza kusimamia kukaza hukumu hiyo yenyewe au kuihamishia katika
Mahakama ya Wilaya ambako mali za mdaiwa zimo.
Kwa kawaida, ni wajibu wa upande ulioshinda mahakamani kuomba mahakama ikaze hukumu.
Mahakama yaweza kukaza hukumu kwa mdaiwa kulipa deni; madai
aliyoamuriwa na mahakama kulipa au kwa kukamata mali au akaunti ya
benki, au mshahara wa mdaiwa, kama hatalipa yeye mwenyewe kwa hiari.
Kukata rufaa
Kukatata rufaa ni haki ya kila mtu ambaye atakuwa hajaridhika na
uamuzi uliotolewa na mahakama. Haki ni ya msingi sana, hivyo basi ni
vema hakimu anayetoa hukumu katika mahakama yoyote ile akamsaidia na
kumwelewesha mshitakiwa juu ya haki hii.
Haki hii inaenda sambamba na kupatiwa nyaraka muhimu kama vile nakala
ya hukumu pamoja na mwenendo mzima wa mahakama, tokea siku ya kutajwa
kwa shauri husika.
Mahakama nyingi zimekuwa na tabia ya kuchelewesha nakala ya hukumu
kwa kisingizio kwamba haijaandikwa sawa, kwani ilisomwa tu. Inawezekana
ukachelewa kuiandaa, lakini sio kwa muda mrefu kiasi hicho kwani
utakuta mkata rufaa hadi miezi miwili inapita yeye anazunguka na barua
huku na huku akiomba nakala ya hukumu yake.
Kama haki imetendeka basi apewe nakala yake ndani ya muda wa kawaida
ili aweze kujiridhisha hata kama hana mpango wa kukata rufaa.
Msomaji mara nyingi ni kawaida kuona mmoja kati ya pande, wakati
mwingine pande zote, zinazopingana kutoridhika na uamuzi wa mahakama
baada ya hukumu kusomwa.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatoa haki
ya kukata rufaa kwenye mahakama ya juu zaidi ya ile iliyotoa hukumu au
uamuzi huo kwa upande wowote ambao unadhani kwamba haukutendewa haki na
mahakama hiyo.
No comments:
Post a Comment