TTCL

EQUITY

Thursday, March 17, 2016

Mkuu wa shule asimamishwa kazi kwa tuhuma za ngono

Mkuu wa wilaya ya Mkalama, Christopher Ngubiagai ameagiza mkuu wa Shule ya Sekondari Chemchem, Tarafa ya Kirumi, Juma Makoro, asimamishwe kazi mara moja, ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma inayomkabili ya kufanya vitendo vya ngono na wanafunzi wake wa kike.
Mkuu huyo wa wilaya, ametoa agizo hilo juzi wakati akizungumza kwenye kikao cha utendaji kilichohudhuriwa na watendaji wa vijiji, kata, tarafa na waratibu elimu kata kilichofanyika kwenye ghala la kijiji cha Nduguti.
Ngubiagai amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mkalama Machi 17 mwaka huu  amwandikie barua ya kumsimamisha kazi mkuu huyo wa shule ili apishe uchunguzi wa tuhuma dhidi yake.
“OCD, (huku akiwa amemwangalia) hakikisha kuanzia sasa mwalimu Makoro anakamatwa na kufanyiwa uchunguzi wa kina juu ya tuhuma ya vitendo vyake ambavyo ni kinyume na maadili ya kazi yake,” alisema Mkuu huyo wa wilaya na kuongeza;
 “Mkuu wa TAKUKURU na wewe kwa nafasi yako, hakikisha unachunguza tuhuma ya mkuu huyo wa Shule ya Sekondari Chemchem. Serikali ya awamu ya tano haina kabisa nafasi na watumishi wa umma wenye tabia mbaya ikiwemo ya kuwaharibia maisha wanafunzi wa kike”
Akifafanua alisema kwa muda mrefu mwalimu Makoro amekuwa akituhumiwa kufanya mapenzi na wanafunzi wa kike ambao ni sawa na watoto wake wa kuzaa.
“Inadaiwa mwalimu Makoro amekuwa akiagiza mwanafunzi wa kike ampelekee madaftari ofisini kwake na mwanafunzi akikabidhi  madaftari hayo anamlazimisha ampige busu hii ni aibu kubwa sana,” alisema kwa masikitiko makubwa.
Katika hatua nyingine, Ngubiagai ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Iramba, alisema kwamba amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Iramba, kutoa maelezo ya kueleweka ni kwanini ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kike Shule ya Sekondari Kinyangiri haujakamilika toka ujenzi wake uanze Septemba, 2011.
“Mkuu wa Shule ya Sekondari Kinyangiri kwa ubunifu wake, aliandika andiko la kuomba ufadhili kwa kutoka ubalozi wa Japan kujengewa bweni la wanafunzi wa kike, andiko hilo lilizaa matunda Septemba 6, 2011 kwa ubalozi huo kutoa hundi ya shilingi 118,686,817,” alisema.
Alisema kwa sababu zisizojulikana hundi hiyo iliyopokelewa na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji kwa wakati huo na kukaa nayo miezi minne bila kuipeleka benki. 
“Baada ya miezi hiyo minne ya kukaa na hundi hiyo kwenye droo ya meza ya ofisi ya mkurugenzi mtendaji, aliipeleka benki na baada ya kuingiza kwenye akaunti, pia akakaa nayo kimya kwa zaidi ya miezi minne mingine, ndipo akampa mkandarasi kazi imechukua zaidi ya miaka minne  hadi sasa na haijakamilika,” alisema Ngubiagai.
Alisema ubalozi wa Japan ulitoa masharti kwamba wenyewe utajenga bweni, halmashauri inunue vitanda 80 na mashuka 80 na wananchi wachangie  kuleta maji, kokoto na mchanga na halmashauri hadi sasa haijatimiza wajibu wake.
Wakati huo huo, alisema kuwa kwenye fedha za ufadhili kutoka Japan kuna dalili kubwa ya ubadhirifu ambao kwa sasa anaufanyia kazi.
Kwa mujibu wa DC Ngubiagai, Mkuu huyo wa Shule ya Sekondari ya Kinyangiri, alifikia uamuzi wa kuandika andiko la kuomba ufadhili wa kujengewa bweni hilo baada ya wanafunzi wa kike waliokuwa wamepanga kwenye nyumba za watu binafsi, wengi kujazwa mimba na kupelekea kuacha Shule.

No comments:

Post a Comment