Bodi
ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa jumla ya Tshs
459/- bilioni kama mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi 122,486
wanasoma katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi katika mwaka wa
masomo 2015/2016.
Hii ni idadi kubwa zaidi
ya wanufaika na fedha kuwahi kutolewa tangu kuanzishwa kwa Bodi mwezi
Julai, 2005 na kwa ujumla, katika historia ya utoaji wa mikopo nchini.
Fedha hizi zimetolewa kati ya mwezi Novemba, 2015 na Januari 10, 2016.
Katika mwaka uliopita wa
masomo, 2014/2015, Serikali kupitia Bodi ilitoa jumla ya Tshs 341/-
bilioni zilizowanufaisha wanafunzi 99,069.
Kati ya fedha
zilizotolewa, jumla ya Tshs 199.7 bilioni zinakwenda kwa wanafunzi
53,537 waliojiunga na masomo kwa mwaka wa kwanza mwezi Novemba, 2015
katika vyuo mbalimbali na Tshs Tshs 259.1 bilioni zinalipwa kwa
wanafunzi 68,916 wanaoendelea na masomo, yaani mwaka wa pili, wa tatu na
kuendelea katika vyuo vya umma na binafsi.
Kwa mujibu wa taarifa ya
Bodi kwa vyombo vya habari iliyotolewa Dar es Salaam leo (Jumatano,
Januari 13, 2016), kundi kubwa katika ya wanafunzi waliopata mikopo ni
wale wanaosoma programu za kipaumbele ambazo zimetajwa katika mwongozo
(Guidelines) uliotolewa na Bodi mwezi Mei mwaka jana, 2015.
Programu hizo ni Udaktari
wa Binadamu, Udaktari wa Meno, Udaktari wa Wanyama, Ufamasia na Uuguzi
na Ualimu wa Masomo ya Sayansi na Hesabu na Uhandisi wa Umwagiliaji.
Wanufaika wengine ni yatima na walemavu.
Katika hatua nyingine,
Bodi ya Mikopo inatoa wito kwa waajiri katika taasisi za umma na binafsi
nchini kuhakikisha wanazingatia matakwa ya sheria iliyoanzisha Bodi
inayowataka kuwatambua waajiriwa wao ambao ni wanufaika wa mikopo
inayotolewa na Bodi; kukata sehemu ya mishahara yao na kuwasilisha kwa
bodi kama marejesho.
Kwa mujibu wa taarifa
hiyo ya Bodi, Kifungu cha 20 (1) (c) cha sheria ya iliyoanzisha Bodi
(Higher Education Students’ Loans Board Act (as amended)), kinawataka
waajiri kuwatambua waajiriwa, kuijulisha Bodi kwa maandishi ndani siku
28 tangu wapate ajira. Aidha, Kifungu cha 20 (2) cha sheria hiyo,
kinawataka waajiri, baada ya Bodi kuthibitisha kuwa muajiriwa ni
mnufaika wa mikopo ya Bodi, (mwajiri) kuitaarifu kuitaarifu Bodi, ndani
ya siku 30 za ajira yake na kukata makato kutoka katika mshahara wa
mwajiriwa na kuyawasilisha Bodi ndani ya siku 15 baada ya kila mwisho wa
mwezi.
Taarifa hiyo imesisitiza
kuwa waajiri wote wanapaswa kutimiza matakwa hayo ya kisheria na kuwa
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameanza kukagua
taaasisi za umma kama zinazingatia matakwa haya ya kisheria.
Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ni Taasisi ya Serikali iliyoanzishwa
kwa mujibu wa Sheria Na. 9 ya mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi
Julai, 2005. Bodi ina majukumu kadhaa, lakini mawili makubwa ni kutoa
mikopo kwa wanafunzi watanzania wahitaji; na kusimamia urejeshaji wa
mikopo kutoka kwa wanufaika wa mikopo
No comments:
Post a Comment