VYOMBO vya habari nchini vimepongezwa kwa kazi kubwa vilivyofanya ya
kutoa taarifa kwa wananchi wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwishoni
mwa mwezi uliopita.
Pongezi hizo zimetolewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, Profesa Elisante ole Gabriel wakati
akizungumza na Menejimenti ya wizara na taasisi zake kwenye kikao cha
kazi kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Profesa Ole Gabriel alisema katika kipindi cha uchaguzi, vyombo vya
habari vilifanya kazi kubwa ya kuwahabarisha wananchi kwa kuzingatia
weledi wa taaluma yao na hivyo kuwawezesha wananchi kujua mambo
mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea nchini.
Katibu Mkuu huyo ambaye hicho kilikuwa ni kikao chake cha kwanza
tangu ateuliwe kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo mwishoni mwa mwezi
uliopita, aliahidi kuwatumikia na kuwaheshimu wafanyakazi wa wizara yake
huku akisimamia majukumu ya kazi kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria
za utumishi wa umma.
“Hiki ni kikao chetu cha kujipanga kwa ajili ya kazi, ni vyema
tukajipanga huku tukijua matarajio ya Mheshimiwa Rais kwetu ni yapi,
wananchi tunaowatumikia wanategemea kupata nini kutoka kwetu na mimi
kama Katibu Mkuu natarajia kupata nini kutoka kwenu,” alisema Profesa
Ole Gabriel.
Akimkaribisha Katibu Mkuu huyo kuzungumza na viongozi hao, Kaimu
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu, Titus Mkapa alisema kikao
hicho ni maalumu kwa ajili ya wizara kujadili utekelezaji wa mipango
yake kwa kasi.
Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti, viongozi hao waliiomba
Serikali iangalie upya bajeti ya wizara hiyo ambayo ni ndogo ili
iongezwe na kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na
Utamaduni Bagamoyo (TasuBa), Michael Kadinde alisema chuo hicho kimekuwa
kikizalisha ajira kwa wanafunzi wanaosoma hapo mara baada ya kumaliza
masomo yao, lakini wanafunzi wengi wanakabiliwa na changamoto ya
kutokuwa na ada.
No comments:
Post a Comment