TTCL

EQUITY

Wednesday, April 6, 2016

KATIBU MKUU KIONGOZI BALOZI KIJAZI AWAASA WAKUU WA MASHIRIKA NA TAASISI ZA UMMA

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Mhandisi John William Kijazi amewaasa Wakuu wa Mashirika na Taasisi za Umma kuzingatia Maadili ya Viongozi wa Umma katika kutekeleza makujumu yao.
Katibu Mkuu alisema hayo leo jijini Dar es salaam wakati wa akifungua mafunzo ya viongozi hao yalioandaliwa na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili kuhakikisha wanaendana Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Mgufuli.
“Maadili yana umuhimu wake mkubwa katika utawala wa maendeleo ya nchi, kupitia maadili mema wananchi wanajenga imani na viongozi pamoja na Serikali yao kwa ujumla” alisema  Balozi Mhandisi Kijazi.
Ili kuhakikisha mafunzo yanakuwa yenye tija, Balozi Mhandisi Kijazi amewasisitiza viongozi hao kutumia muda vizuri na kujikumbusha na kujifunza maadili hayo kwa manufaa ya mashirika na taasisi zao pamoja na taifa kwa ujumla.
Balozi Mhandisi Kijazi alitaja umuhimu wa maadili katika jamii na kusema kuwa yanasaidia kusimamia rasilimali za umma na kuzitumia kwa maslahi ya wote, kuongeza tija na thamani ya huduma, zinazotolewa na Serikali, kudhibiti mianya ya ukiukwaji wa  maadili na vitendo vya rushwa, kujenga ujasiri wa kusimamia Sheria, Kanuni na Taratibu za utumishi wa umma.
Maadili pia yanasaidia wananchi, viongozi na Watumishi wa Umma kutoa mchango wa haraka katika kutekeleza maendeleo ya nchi, kuepuka utata wa maamuzi ya migongano ya kimaslahi, kuwavutia wawekezaji, kujenga na kudumisha amani na utulivu pamoja na kuondoa na kukomesha ubinafsi kwa viongozi.
Aidha, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi  Kijazi amesema kuwa ukiukwaji wa maadili unaathari hasi kwa taifa ambapo alizitaja baadhi ya athari hizo kuwa ni rasilimali za nchi kunufaisha wachache, wananchi kukosa haki zao za msingi kutokana na rushwa na upendeleo, viongozi wa umma kujilimbikizia mali isivyostahili bila kujali hali za wananchi wanaowaongoza, kupungua kasi ya uwekezaji pamoja na kudhohofika kwa uchumi wa nchi.
Madhara mengine ya kutojali maadili ni wananchi kukosa imani na Serikali yao, kuchochea vurugu pamoja na wananchi kutotii sheria za nchi na hivyo kuhatarisha usalama, amani na utulivu wa nchi.
Kwa upande wake Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Salome Kaganda alipokuwa maelezo mafupi kwa Mgeni Rasmi amesema kuwa misingi ya maadili na maadili yanalenga katika kuzuia mgongano wa maslahi, upendeleo, matumizi mabaya ya rasilimali za umma na taarifa za ofisi na mwenendo usiofaa kwa viongozi wa umma ili kuimarisha na kuendeleza dhana za uadilifu, uwajibikaji na uwazi  ambazo ni sifa muhimu za kiongozi.
Ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi, Jaji Mstaafu Kaganda amesema kuwa ofisi yake inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa watumishi ambapo kuna zaidi ya viongozi 15,000 huku Sekretarieti ina wafanyakazi 200 nchi nzima.
 Mafunzo hayo yamehudhuriwa na washiriki 40 ambapo yalifanyika kwa Mawaziri, Manaibu Waziri, Mkatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Wenza wa Viongozi, Wakuu wa Mikoa.

No comments:

Post a Comment