MOJA ya habari kubwa katika vyombo vya habari nchini juu
ya ziara za kushtukiza za Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli,
ikiwemo ziara ya Wizara ya Fedha.
Akiwa katika ofisi za wizara hiyo iliyo mdomoni kabisa kwa Ikulu ya
Magogoni, Dar es Salaam, Rais huyo aliyeanza kazi rasmi Alhamisi ya wiki
iliyopita mara baada ya kuapishwa, alikagua ofisi moja baada ya
nyingine, huku akishuhudia baadhi ya viti vikiwa vitupu, bila ya
wahusika kuwapo katika ofisi zao.
Alidiriki kuhoji, na kujibiwa baadhi yao wako nje ya ofisi ama kwa
kazi maalumu au kupata kifungua kinywa. Kwa ujumla, ziara hiyo iligeuka
kuwa gumzo, ikielezwa ameanza kufuatilia kwa vitendo utendaji kazi wa
watumishi wa umma na hivyo uamuzi wake kwenda sambamba na kaulimbiu
maarufu aliyoibuka nayo wakati wa kampeni zake za kuwania urais kwa
tiketi ya CCM, `Hapa Kazi Tu’.
Wapo waliompongeza kwa uthubutu wake wa kutaka kujionea utendaji kazi
katika idara, taasisi za serikali na mashirika ya umma kwa ujumla, huku
wengine wakibeza, kwa madai kuwa ni `nguvu ya soda’.
Sisi wa HabariLeo Jumapili, tunaungana na waliompongeza Dk Magufuli,
kiongozi mwenye historia ya uchapakazi na uadilifu, kwa kuonesha kwa
vitendo jinsi anavyokerwa na watumishi wa umma wanaofanya kazi kwa
mazoea, wakitumia muda mwingi kufanya mambo yao binafsi badala ya
kutimiza majukumu yaliyowaweka ofisini.
Pamoja na pongezi, ni vyema watumishi wa umma na Watanzania kwa
ujumla, kila mmoja akajitathmini na kuona ni jinsi gani atatoa mchango
wake katika kustawisha maendeleo ya nchi.
Haya anayoyafanya Dk Magufuli kamwe si majukumu yake, bali
anachofanya ni kujaribu tu kuwakumbusha watumishi kuwa, kila mmoja
atimize majukumu yake kulingana na mahali au ofisi alipo.
Rais ana majukumu mengi mno, hivyo itashangaza kuona watumishi
wakilala au kwenda ofisini kusaini daftari la mahudhurio na kisha
kuingia mtaani kufanya ujasiriamali na mwisho wanapokea fedha za
mshahara bila hata kuifanyia nchi kitu chochote cha maana.
Je, tukimsubiri Rais apite kila sehemu, hata kwenye kuzibua mitaro
mitaani kwetu ambako pia kuna mamlaka husika za kusimamia majukumu kama
hayo, mwisho tutamlaumu Rais kuwa hajafanya chochote katika kukuza
maendeleo na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Ifike mahali kila Mtanzania atimize wajibu wake, aliye kwenye
utumishi wa umma atimize wajibu wake ili kupunguza kero na foleni na
urasimu usio na maana katika ofisi za umma.
Tukifanikiwa kuyafanya haya, kwa maana ya kila mmoja kutimiza wajibu
wake, hakika haitatuchukua muda mrefu kabla ya kuona mabadiliko makubwa
ya ustawi wa nchi na maendeleo kuanzia hatua ya familia, kata wilaya,
mkoa na hata taifa kwa ujumla.
Na hicho ndicho wanachotaka kukiona Watanzania, mabadiliko hasa ya
kiuchumi, na si kubadili sura au rangi za bendera za vyama pekee. Ili
kulifikia lengo hilo, tuanze kwa kumuunga mkono Dk Magufuli kwa kuchapa
kazi kwa vitendo, badala ya kuleta ujanja ujanja na mwisho tuishie
kuilaumu serikali kuwa haijafanya lolote.
Kamwe huo hauwezi kuwa uzalendo, bali unafiki na uhaini wa uchumi wa
taifa hili. Ahsante Dk Magufuli kwa mwanzo mzuri katika kuwaamsha
watumishi, nao sasa wapige kazi bila kuvizia ziara za viongozi ili
waonekane ni watu makini katika maeneo ya kazi.
No comments:
Post a Comment