Namna ya kupangilia Nguo
Mara nyingi unaweza kukuta mtu ana kabati limejaa nguo hadi zinakosekana pa kuwekwea na katika hali halisi anajiona hana nguo za kuvaa. Hali  hii inatokana na kukosa mpangilio wa nguo kwenye kabati na pia kuweka nguo ambazo hazihitajiki tena. Nguo zisipokuwa na mpangilio maalumu ni ngumu sana kutafuta nguo gani uivae na ipi maana hujui ipo upande gani wa kabati. Pia pale unapohifadhi nguo ambazo unajua hutazivaa tena inasababisha kabati kujaa bila sababu. Njia hizi zitakusaidia katika kupanga kabati lako:

organized-closet1. Tafuta siku ambayo unamuda wa kutosha na toa nguo zako zote kabatini kisha tenga zile ambazo unahitaji kuzivaa na zile ambazo unaona hutazivaa tena ( iwe zimekubana, zimechakaa, hauzitaki tena n.k).

2. Tafuta mfuko safi uweke nguo zote ambazo hutazivaa tena ambazo upo tayari kugawa kwa wenye uhitaji. Ni vyema ukianzia nyumbani mwako, kama una dada wa kazi unaweza mpa zile ambazo zitamfaa na kisha nyingine ukapelekea wengine wenye mahitaji unaowafahamu kama ni kanisani au mahali popote pale. Ila jihadhari usimpe mtu nguo iliyochakaa sana, haipendezi.


3. Nguo ambazo unazihitaji zitenge katika makundi (blauzi, sketi, magauni, n.k) na kisha uzikunje vizuri na kuzipanga kabatini kila kundi sehemu yake. Hii itakusaidia ukiwa unatafuta gauni unajua uangalie sehemu gani.  Nguo zinazoendana pamoja kama suti au vitenge ni vyema zikawekwa pamoja sketi na blauzi yake. Kama kabati lina nafasi kubwa makoti ya suti yakiwekwa kwenye henga yanapendeza zaidi.
4. Vitu kama mikanda, skafu, mitandio n.k viwekwe mahali pake ili iwe rahisi kupatikana pale vinapohitajika.
Jitahidi uwe na tabia ya kupanga nguo zako kila unapozifua. Ilikuepuka kutafuta nguo asubuhi na hatimaye kuharibu mpangilio wa kabati lako ni vyema kama utakuwa na utaratibu wa kunyoosha nguo za wiki zima kila mwisho wa wiki, hii itaokoa muda na ‘stress’ za kutafuta nguo ya kuvaa kila asubuhi.