VIJANA wameshauriwa kuwa wabunifu wa miradi mbalimbali na kufikiri
njia mbadala za kujipatia kipato ili kuweza kujiajiri na kuepukana na
ajira tegemezi.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda aliyasema hayo jana jijini
Dar es Salaama wakati wa kuwaaga na kuwakabidhi bendera ya Taifa
washindi wa tuzo ya Anzisha iliyoanzishwa na Chuo cha Uongozi Afrika
(ALA) cha Afrika Kusini.
“Taifa letu lina changamoto kubwa ya watu kufikiri… na ukipata watu
waliobadilisha fikra zao na kuweka mipango yao kwenye utekelezaji hapo
ndo penye maendeleo,” alisema na kuongeza: “Vijana wengi kwa sasa wana
malalamiko ya ajira na mitaji lakini hata ukitaka kuwapa mitaji hawana
mawazo ya biashara, hivyo tunawapongeza vijana hawa kwa hatua
waliyofikia ya kuwa miongoni mwa vijana 12 waliochaguliwa kwenda kwenye
fainali za tuzo hizo”.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi
Tanzania(TPSF), Godfrey Simbeye alisema tuzo hiyo ilianzishwa kwa lengo
la kuwawezesha wajasiriamali vijana barani Afrika kupanua biashara zao
ili kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi barani Afrika.
Alisema kwa hapa nchini tuzo hiyo inasimamiwa na TPSF ambayo ina
jukumu la kuitangaza na kuwahamasisha vijana wajasiriamali wenye umri wa
miaka 15 hadi 22 kuomba kushiriki katika tuzo hizo.
No comments:
Post a Comment