ORODHA ya wabunge katika Bunge la 11 italifanya liwe tofauti na
lililopita kutokana na idadi ya wabunge wa vyama vya upinzani
kuongezeka, huku vijana nao wakionekana kuwa ni wengi zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliyotolewa
wiki iliyopita, wabunge wenye umri kati ya miaka 21 na 35 wapo 47, wenye
umri kati ya miaka 36 na 50, wapo 112 na walio na umri zaidi ya miaka
51, wapo 91.
Kimsingi vijana ni hazina ya taifa na hivyo wingi wao ndani ya chombo
hicho cha kutunga sheria ni jambo jema, kwa sababu litasaidia kuwaandaa
kushika madaraka makubwa zaidi katika kuongoza nchi yetu siku zijazo.
Kinadharia, vijana huwa na hulka ya kutaka mabadiliko wakati wote
lakini wazee mara nyingi huwa na hofu ya kupokea mabadiliko wakitamani
hali iliyopo iendelee. Wakati wazee wamekuwa muhimu wakati wote kutokana
na uzoefu wao wa kuona mengi, ongezeko la vijana katika Bunge la 11 ni
jambo jema pia kwani watasaidia kuwachangamsha wazee katika kujadili
hoja, mintarafu suala zima la mabadiliko chanya.
Hata hivyo, kwa uzoefu wa Bunge lililopita, vijana wana tatizo la
mihemko ambayo wakati mwingine huwafanya wajisahau na kutumia lugha
zisizo na staha katika kufikisha ujumbe wao.
Kwa utamaduni wa Mwafrika, kijana anatazamiwa kumheshimu mtu
aliyemzidi umri, na hata kama ni kumkosoa au kupingana naye anatakiwa
afanye hivyo kwa kutumia lugha nzuri, isiyoudhi wala kumkosea adabu
mkubwa.
Lakini, kwa bahati mbaya, katika Bunge lililopita tulishuhudia baadhi
ya vijana na wazee wachache wakivuka mipaka kwa kutumia muda adhimu wa
Bunge kurusha vijembe, lugha zenye ukakasi, kuzomea na hata kuzira na
kutoka nje.
Kwa kutumia uzoefu wa Bunge lililopita hofu yetu ni kwamba kuna
uwezekano wa mijadala ndani ya Bunge la 11 kutawaliwa na mihemko ya
vijana hawa kutaka kuonesha umahiri wao katika siasa hata kama
wanachokijadili hakina tija kwa taifa.
Vijana na hata wazee wanaweza pia kuhamashia mchakato wa uchaguzi
ambao umekwisha kwenye Bunge, jambo ambalo litazua malumbano yasiyo na
tija. Wakati tukiamini kwamba semina elekezi zitaandaliwa kwa ajili ya
wabunge wapya kuwafunza kanuni na maadili ya chombo hicho chenye heshima
kubwa kwa Watanzania, ni imani yetu kwamba wabunge vijana
hawatowaangusha waliowachagua kwa maana ya kugeuza chombo hicho kuwa
kijiwe cha lugha zenye ukakasi.
Tunawakumbusha vijana kwamba uwezo watakaouonesha sasa katika kujenga
hoja kwa umakini na busara huku wakilinda heshima yao na ya Bunge, ni
kitu kitakachowajenga zaidi katika maisha ya kisiasa wanayoyaanza.
Umakini, heshima na busara watakazotumia kujenga hoja bila shaka
itakuwa sababu ya kuendelea kuchaguliwa tena katika chaguzi zijazo.
Tunaamini pia kwamba Spika atakayechaguliwa atakuwa madhubuti katika
kusimamia kanuni na kutoa haki kwa wabunge wote bila upendeleo.
Kadhalika tunaamini spika huyo atahakikisha wanaokiuka kanuni za Bunge,
wanachukuliwa hatua bila kujali vyama vyao.
No comments:
Post a Comment