TTCL

EQUITY

Saturday, December 6, 2014

HAYA NDIO MAMBO YA KUZINGATIA ILI NDOA IWE HALALI


NDOA nyingi zimekuwa na migogoro  ya mara kwa mara ambayo hupelekea ndoa hizo kutodumu. Tafiti zinaonyesha wanandoa wengi ambao wanaishi katika ndoa zao sio kwa kuwa wanapendana, bali ni kwa kuwa wana watoto au makusudi mengine, ni dhahiri kuwa yale wanandoa wanayoyategemea kwenye ndoa hayapo kwa sababu hakuna upendo baina ya wanandoa.
Ndio maana unaweza kushuhudia migogoro mingi dhidi ya wanandoa kwa wasuluhishi au hata mahakamani mara kwa mara. Kwa lugha nyepesi ndoa ni muungano kati ya mwanaume na mwanamke ambao wanakubaliana kuishi kwa pamoja kama mke na mume siku zote za maisha yao.
Lakini kufuatana na sheria ya ndoa ya mwaka 1971, Ndoa ni muungano wa hiari kati ya mwanaume na mwanamke unaokusudiwa kudumu kwa muda wa maisha yao.
Kabla ya kuangalia azma ya makala haya ya leo hebu tuzijue aina mbili za ndoa ambazo zinakubalika kisheria,
i) Ndoa ya mke mmoja, hii ni ndoa ambapo mwanaume ana mke mmoja tu. Kwa mfano ndoa zinazofungwa kwa mujibu dini ya kikristo.

ii] Ndoa ya wake wengi, hii ni ndoa ambayo mwanaume ana wake zaidi ya mmoja. Mfano wa ndoa za namna hii ni zile ndoa zinazofungwa kwa mujibu wa dini za Kiislamu au zile ndoa zinazofungwa kwa taratibu za kimila. Ili ndoa yoyote ile ikubalike kisheria basi ni lazima iwe imekidhi matakwa ya kisheria kama navyoelezea hapa chini:
 (a) Ni lazima muungano uwe wa hiari:
Mume na mke wawe wameamua kuishi pamoja kwa ridhaa yao wenyewe. Hii inamaanisha kusiwe na kulazimishwa, kuhadaiwa kwa aina yoyote, kwani muungano kama huo utakuwa batili kisheria.
Ni kosa la jinai kushiriki katika shughuli ya ndoa ambayo mmoja wapo au wote wamelazimishwa kufunga ndoa. Kwa upande mwingine ndoa kati ya mtoto na mtu mzima haiwezi semekana kuwa ni ya hiari kati ya wawili hao.
Mfano wa ndoa batili ambazo hata msomaji wangu umewahi kushuhudia  ni ndoa itokanayo na msukumo wa mzazi au wazazi.  wazazi wanalazimisha, ili binti  aweze kuolewa na mwanaume Fulani, ili waweze kupata kipato tu, wakati binti mwenyewe hayupo tayari kuolewa na mwanaume husika au kwa kuwa ni mtoto anakubali bila kujua matokeo ya baadaye.
Wakati mwingine maneno  yakutisha au yakumkana mtoto kwa mfano: utasikia mama akisema kama wewe ni mwanangu lazima uolewe na mtu fulani au usiniite mama au baba endapo hutaolewa na mtu fulani. Kwa kweli haya ni mabavu na endapo binti huyo ataolewa basi ndoa hiyo ni batili kwa kuwa hakuwa haiajikidhi sharti la hiari.
 (b) Muungano uwe ni kati ya mwanamke na mwanamume:
Muungano wa watu wa jinsia moja hata kama ni wa hiari muungano huo hautambuliki  kamwe kisheria. Pia dini zote zinakataza. Hivyo basi kwa mujibu wa sheria mtu huhesabika mwanamke au mwanaume kutokana na sehemu za siri alizozaliwa nazo na siyo alizozipata baadaye.
Jamii inachukulia kuwa ndoa ni njia pekee ya kujipanua. Upanukaji huo ni kwa kuzaa watoto. Kwa hali hiyo, ili kupata watoto ni lazima ndoa iwe kati ya mwanaume na mwanamke.
Nazungumzia hivyo kwa kuwa kutokana na kuendelea kwa dunia ya utandawazi siku hizi kuna mbinu za kubadilisha maumbile aidha kutoka kuwa mwanaume na kuwa mwanamke na mwanamke kuwa na hulika za kiume, hii haitamaanisha kuwa ni mwanaume, cha msingi hapa kigezo ni sehemu zake za siri alizozaliwa nazo.
(c) Muungano huo uwe unakusudiwa kuwa wa kudumu:
Pamoja na kuwa mwanamke na mwanaume wameamua kuishi pamoja kwa hiari yao lakini siyo kwa kudumu muungano huo hautambuliki kisheria kama ndoa.
Muungano ni lazima uwe wa kudumu maisha yote au kama mmoja wao amefariki au kama ndoa imekumbwa na matatizo na mahakama ikaona ni bora kutoa talaka kwa yeyote aliyefika kulalamika.
(d) Wafunga ndoa wasiwe maharimu:
Maharimu ni watu walio na mahusiano ya karibu ya damu au kindugu.
Wawili wanaoamua kufunga ndoa wasiwe na uhusiano wa karibu kindugu. Inakatazwa katika kifungu cha 14 cha Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 mtu kuoa au kuolewa na mzazi wake, mtoto au mjukuu wake, kama ni dada yake, mama au shangazi au baba wa mjomba wake, baba au mama wa kambo na mwanaye aliyemfanya kuwa mtoto wake (adopted child).
Ikumbukwe pia kitendo cha kufanya mahusiano na ndugu ni makosa ya jinai kwa mujibu wa sheria zetu za Tanzania, kama ilivyoainishwa katika Kanuni za Adhabu Sura ya 16.

No comments:

Post a Comment