TTCL

EQUITY

Saturday, December 12, 2015

Nyerere aliondoka hajamaliza kazi yake kututoa kwenye utumwa wa fikra

maendeleo3
Ni heri kuchakaza nguo kuliko kuchakaza akili

ALITOKEA bwana mmoja akawakabidhi jamaa watatu mikungu mitatu ya ndizi na bahasha yenye barua ndani yake wampelekee rafiki yake. Njiani watu wale wakajisikia njaa kali. Wakautafuna mkungu mmoja. Walipofika, wakaikabidhi mikungu miwili ya ndizi na barua ile kwa mwenyeji wao.
Mwenyeji aliisoma kwanza barua ile, akawashukuru na kisha akawauliza, “ Je, uko wapi mkungu wa tatu? Watu wale wakashangaa sana yule bwana amejuaje. Walirudi nyumbani wakiamini, kuwa bahasha ile ilikuwa na macho.
Basi ikatokea tena, wakatumwa na bwana yule yule. Waende mji ule ule na kwa rafiki yake yule yule, wapeleke tena mikungu mitatu ya ndizi. Njiani wakajisikia tena njaa kali. Wakaambizana; “tusimame na tule mkungu mmoja tena. Lakini, tuhakikishe, hii bahasha tunaizika kwenye udogo isije kutuona tena.” Wakafanya hivyo.
Lakini walipofika tena, jamaa akawauliza mbona mkungu mmoja siuone? Unaweza kuona utumwa wa fikra unavyotia aibu, ndiyo maana Martin Luther , Jr, akakwambia, “Nothing in the world is more dangerous than sincere ignorance and consciencious stupidity.” Yaani hawa jamaa wanaoneka “malofa” kweli mbele ya jamaa yao.

Ndiyo maana mara baada ya kupata uhuru wa bendera, Nyerere alianza kupigania uhuru wa fikra kwa sababu aliamini kabisa ukombozi wa mtanzania hautakamilika bila kuwa na uhuru wa fikra. Uhuru wa fikra kulingana na Mwl. Nyerere ni hatua ya kumbadilisha mtu kutoka mawazo ya ukoloni yaliyomgandamiza na kumfanya akili yake kudumaa kwa kutokujiamni na kujawa na nidhamu ya woga kwa kutii kila amri za wakoloni pamoja na kwamba zilikuwa zinamdhalilisha.
Silaha pekee aliyoitumia ilikuwa elimu kwa wote na katika hilo alipeleka watanzania kila kona ya dunia kuitafuta elimu kwa gharama yoyote. Kwa bahati mbaya wengi waliokwenda shule wakaenda kupambana na mitihani badala ya utumwa wa fikra na walipoingia madarakani wakawa majambazi wa rasilimazi za watanzania.
Matokeo yake Nyerere ametangulia mbele za haki akituacha katika hatua ya kwanza ya ukombozi: yaani uhuru wa bendera. Kulingana na Nyerere, ukombozi ni mchakato wenye hatua tatu:uhuru wa bendera, uhuru wa fikra na uhuru wa uchumi. Ni uhuru wa fikra ndo huzaa uhuru wa uchumi. Kuwa na uhuru wa bendera ni sawa na kuwa huru huku unanjaa kama anavyosema Lucky Dube, “Unapenda kuwa mtumwa uliyeshiba, ama mtu huru mwenye njaa?”
Leo hii inakuwa vigumu sana kupambana na mkoloni mweusi kwa sababu watanzania wengi tu wabeba mikungu ya ndizi tu, yaani akili zetu zimechakaa. Kuna methali ya Kipare inasema, “Ni heri kuchakaza nguo kuliko kuchakaza akili.”
Haturuhusu bongo zetu kufikiri, badala yake tumekuwa wanyenyekevu kwa majambazi wa jamii kwa kujikomba na kujipendekeza. Kumnyenyekea mtu kakuibia dhahabu, kabinafisisha ardhi yote, kaiba pesa zote na hospitali hazina dawa, duka umefunga kwa sababu ya kodi kubwa, umefukuzwa kazi kwa sababu kiwanda hakizalishi, umefukuzwa kwenye nyumba ya kupanga kwa sababu umeshindwa kulipa kodi, mazao yako yameozea shambani kwa sababu yamekosa soko, umefukuzwa shule kwa sababu umeshindwa kulipa ada, hujaenda kwenu tangu uanze kazi kwa sababu hela yako ya likizo imelipia safari za bosi wao ughaibuni, hapo ulipo umeme umekatika, umeshindwa kufanya kazi ili ulipe mkopo uliochukua benki, mapato ya muziki wako yanazidi kushuka mpaka umechanganyikiwa ni unyenyekevu usio na utaratibu. Yaani ni ukorofi tu.
Lakini pia ile dhana ya Mpende Adui yako imechangia kutudumaza kiakili. Mie siamini kama ni maagizo ya Mungu kama tunavyojidanganya kuendelea kuwachekea mafisadi wa nchi hii badala yake ni ugonjwa wa Stockholm kama anavyosema Robert Mndeme kupitia makala yake ya, Stockholm Syndrome na ufisadi rasilimali aliyoichapisha kwenye gazeti la Raia Mwema, 14 Machi, 2012.
Anasema, “Agosti 23, mwaka 1973 katika mji mkuu wa Sweden, Stockholm, lilitokea tukio lililoishangaza dunia. Majambazi yalivamia benki kwa lengo la kufanya wizi wa kutumia silaha. Katika purukushani, waliwashikilia mateka wafanyakazi wa benki husika. Lakini baada ya jitihada, polisi waliwazidi maarifa majambazi tayari kwa kuwaokoa mateka ambao hadi wakati huo, walikuwa wameshikiliwa kwa takriban siku ya sita.
Kwa mshangao wa dunia nzima, mateka hao mithili ya watu waliokuwa usingizini wakiota, badala ya kuukubali ukombozi ule wa polisi waliupinga na kuwakumbatia majambazi. Pamoja na udhalilishaji, mateso makali na ya hatari waliyokuwa wamekwishafanyiwa, walishindwa kabisa kuwachukulia majambazi katika ukweli wao na badala yake waliwatetea. Juhudi za polisi na misaada mingine ya Serikali ikaonekana ndiyo tatizo mbele ya mateka wale badala ya majambazi na ukatili wao”.
Huu ugonjwa ni kiboko na pengine kwa hapa kwetu Tanzania ndiyo umepelekea majambazi yaendelee kuzishughulikia rasilimali za nchi hii kwa malipo ya matusi. Mliowengi mtakubaliana na mimi kwamba tuna viongozi wengi wametujeruhi sana lakini siku zote wanachaguliwa kwa kishindo kuendelea kututawala. Kiongozi mmoja kawatukana wapiga kura wake kwamba wamelewa viloba lakini cha kushangaza kapita kwa kishindo katika kura za maoni na ni matumaini yangu atachaguliwa tena na lazima atakuwa waziri. Huu ni ugonjwa, siyo bure.

 
Ndiyo maana nasema Nyerere aliondoka hajaimaliza kazi. Lakini kuondoka kwa Nyerere isiwe kigezo cha sisi kushindwa kuutafuta ukombozi wa fikra. Tuendelee kupamba na utumwa huo, vinginevyo Tanzania itapotea kwenye uso wa dunia. Wajina wangu Denis Waitley aliwahi kusema, “life is inherently risky. There is only one big risk you should avoid at all costs, and that is the risk of doing nothing.”
Kumbe kila mtu kwa nafasi yake tuungane kwa pamoja kufanya kazi ya kuutafuta uhuru wa fikra. Kuna methali ya Kipare inasema, “Afadhali kuchakaza nguo kuliko akili”. Maana yake ni kuwa hakuna kitu bora kama akili
. Kuwa uchi kinguo, mtu anaweza kununua zingine. Lakini mtu anapokuwa uchi kiakili, hakuna namna. Kumbe tunakila sababu ya kuvalisha nguo akili zetu ili kuondokana na imani ya kwamba wanasiasa watabadilisha maisha yetu. Kwa kufanya hivyo tutapunguza ushabiki uliopitiliza wa kudeki barabara ili kuruhusu unyonyaji.
Nasema kuruhusu unyonyaji kwa sababu wanasiasa wote bila kujali yuko chama gani wako katika kundi la kufaidika na ujinga wa watumwa wa fikra, ndiyo maana kabla hawajatoa ahadi wanasoma kwanza uzaifu wa watanzania uko wapi. Ngoja ni kuchekeshe, mgombea mmoja kaenda kule Lindi na akasema akiwa rais atabadilisha mtaala wa elimu ujikite katika mambo ya gesi tu kwa watu wa Lindi.

 
Yaani kwa mtu makini, hii haiingii akilini lakini kwa kuwa wengi tu mateka wa utumwa wa fikra tukapayuka kwa vifijo na nderemo. Nyerere alituacha pabaya kwakweli. Jamani wenye fikra finyu tusaidiane kuikomboa jamii yetu.
Hapa nataka tuelewane vizuri, hata kitendo cha kuona uovu na ukashindwa kuukemea kwa njia yoyote ile hata kwa kununa tu basi wewe u mtumwa wa fikra na unahitaji kukombolewa pia. Kumbe , wasiwasi, mashaka, ubinafsi na unafiki wa mtanzania ni silaha ambazo zinamjenga na kumuimarisha jambazi wa jamii yetu. Kuendelea kuishi na silaha hizo ndiyo kifo chetu.
Ni kosa la kijinga na lisilosameheka kukabiliana na adui fisadi kwa kutumia woga, wasiwasi, mashaka, ubinafsi na hisia hasi nyingine zote. Tukumbuke kuwa majambazi ya jamii yanatumia ujinga wetu kuendelea kujinufaisha. Na siku zote, jambazi wa kijamii atatumia kila mbinu kuzalisha woga, wasiwasi na mashaka kwa mateka wake. Kwa mfano, leo hii kuna watu wameishajazwa hofu kwamba ukichagua chama cha upinzani nchi itaingia vitani.
Kwa hila kama hizo hutakuwa kwenye utambuzi halisi wa kinachoendelea kwani utakuwa umepumbazika kiasi cha kutosha. Kama ilivyo kwa uhai wa samaki kwenye maji ndio ilivyo kwa jambazi wa jamii anavyo tegemea ujinga wa mtanzania kuishi. Jamani acheni Nyerere aitwe Baba wa Taifa, maana alikuwa na akili zakuona mbali na siyo mbele.
Nakwambia kichwani pakiwa vizuri hutakuwa na haja ya kukimbizana na samaki bwawani kama unataka kuwatokomeza. Jambo la kufanya liko wazi, ni kuwakaushia maji yote bwawani bila kubakiza hata tone.
Na hapo utawakamata wote kama kumsukuma mlevi. Kwa maneno mengine, ili kumkamata na kumshughulikia jambazi wa jamii ni kuweka woga, mashaka, wasiwasi, na unafiki pembeni . Uhakika na ujasiri huu ni ndiyo ukombozi wa fikra.
Nimalizie kwa kusema hivi kama kweli tunataka heshima kiuchumi, kiafya, kisiasa na ki jamii hatuna budi kuutafuta ukombozi wa fikra. Tunatakiwa kuzalisha taifa huru na lenye watu watetea utu wao, watetea haki zao za ubinadamu na Taifa kwa kujiamini na kwa ukamilifu wote bila woga, unafiki na kujikomba.
Tunahitaji kuvunja mitazamo finyu kama ile ya kwamba, “Umasikini tulionao ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu kama wakoloni na mabeberu wanvyotaka tuamini” Badala yake inatakiwa tuelewe kwamba Mungu ametuumba ametupa rasilimali nyingi ambazo kama zingelitumika kwa faida yetu, zinaweza zikatuinua tukawa matajiri kuliko hao wanaotunyanyasa sasa.
Tunapowaachia watu wengine dhahabu iliyoko Kahama, Geita, Tarime na madini mengine kila kona ya Tanzania bila kuchangia vya kutosha katika maendeleo ya nchi hii ni ujinga wetu wenyewe kwa sababu Mungu aliiweka dhahabu hiyo hapa ili watanzania tuweze kujitajirisha nayo na kutokomeza umasikini wetu. Tim Ferriss anakwambia, fikiri kwa upana usisikilize maneno ya watu wanaokuambia jambo hili haliwezekani. Maisha ni mafupi kufikiri kidogo.

No comments:

Post a Comment