TTCL

EQUITY

Saturday, December 6, 2014

UBABE WA CCM UMEKARIBIA MWISHO

Chama Cha Mapinduzi hakikosi kulalama (kutoa maelezo yenye hisia ya kutoridhishwa na jambo) kwenye mikutano ya hadhara baada ya kuona mambo yake kutokwenda kama kilivyotarajia. Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana anafanya ziara ya mara kwa mara vijijini na kuona hali ya mambo yalivyoharibika. Wakati wenziye wakikazania kukisakama Chadema, yeye anaeleza jinsi watendaji wa serikali wanavyokula fedha za wananchi na kushindwa kutekeleza ahadi za miradi mbalimbali ya maendeleo. Anakiri kuwa watendaji wa chama chake na serikali hawana ari ya utendaji, nidhamu wala ubunifu ila kukaa ofisini tu. 
Yaliyofichuliwa na kukemewa na Chadema huku CCM kikifanya kazi ya ziada kukanusha, sasa yameshikiwa bango na Kinana! Alipokuwa Bagamoyo aliitaka serikali ishughulikie malipo ya wananchi wanaotakiwa kupisha uwekezaji katika eneo la Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZ) na wakati huohuo kuwaelimisha kuhusu mradi huo ili kuwaondoa kwenye utata unaowafanya washindwe kushughulikia maendeleo yao. “Si haki kuwaweka wananchi kwa muda mrefu mpaka wanashindwa kufanya mambo yao ya msingi. Serikali yapaswa  kumaliza tatizo hili na kuwaondoa wananchi katika hali ya kutofahamu kinachoendelea”, alisema.
  Akiwa ziarani Mafia, Kinana aliuambia mkutano wa hadhara kwamba ameambiwa viongozi wengi wa huko, hasa wenzake wanaovaa mashati ya kijani (wana-CCM), waliojikita zaidi katika fitina na kugombea vyeo lakini wamekuwa wakijisifia kuwa nambari wani. “Kwa mtindo huu hamuwezi kuwa hivyo ila mtakuwa namba kumi. Viongozi wanaoeneza fitina dhidi ya wenzao waache na kama wanataka uongozi wasubiri mwakani,” alisema.
Kinana amesikika mara kadhaa akiwakemea watendaji wa serikali kwa umangimeza (wanaoongoza kwa kukaa ofisini tu) huku miradi ya maendeleo ya wananchi ikisuasua, kukamilishwa chini ya viwango au kutokamilishwa kabisa, wanaofisidi fedha za umma na wanaokumbatia rushwa. Hakuna eneo lolote analokwenda Kinana asikose kusikia malalamiko ya wananchi kuhusu ahadi zilizotolewa na chama chake lakini hazijatekelezwa.
Kwa mfano alipokuwa Kibaha, alielezwa kuhusu ukosefu wa vifaa-tiba mbalimbali kwenye hospitali hiyo ya rufaa mkoa wa Pwani. Kwamba serikali iliahidi kuikabili hali hiyo lakini imepita miaka kadhaa bila ahadi hiyo kutekelezwa. Akiwa Mkata katika wilaya ya Handeni aliilaumu Benki ya Dunia akisema imekuwa kikwazo kwa maendeleo ya nchi masikini duniani ikiwemo Tanzania. Akasema mradi wa maji huko Mkata ulibuniwa miaka takriban kumi iliyopita na ulitazamiwa kukamilishwa mwaka 2008 lakini mpaka sasa haujakamilika.
Mambo kama haya hufanyika wakati watendaji wa serikali ya CCM wakiangalia tu bila kuchukua hatua. Kwa miaka sita walikuwa wapi bila kufuatilia hata sasa wailaumu Benki ya Dunia kwa kutokamilisha mradi huo? Ikumbukwe tu kwamba Benki hiyo ina wataalamu wake wanaofuatilia kuona jinsi fedha zake zinavyotumika. Ikibainika fedha kutumiwa n-nje ya mkataba, utoaji mwingine wa fedha husitishwa na hapana shaka ndivyo ilivyo kwa miradi mingi nchini inayolegalega kutokana na wafadhili kutoridhishwa na jinsi fedha zao zinavyotumiwa.
Methali yatwambia: “Ulivyoligema (tembo) utalinywa vivyo.” Ulivyoigema pombe yako utainywa hivyo hivyo. Ni methali inayotukumbusha kwamba tutakapo kufanikiwa katika jambo lazima tulianze vizuri. Msingi mzuri wa jambo ni muhimu. Yaweza kutumiwa kwa mtu aliyetenda jambo lililomletea matatizo kumkumbusha lazima apambane nayo. CCM yapaswa kupambana na hali iliyoko nchini kwani ndicho chama kilicho madarakani na uduni wa maisha umesababishwa nacho. Sasa chatapatapa na kukiandama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa madai kuwa kinawapotosha wananchi kwa kuwashawishi kufanya maandamano na mikutano yake ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C).
CCM kinawazuga (kitendo cha kuwafanya wafuate mambo wanayoelekezwa bila ya kujijua) wananchi kwamba wasisikilize ‘porojo’ za Chadema zinazohatarisha amani ya nchi! Ili kukabiliana na wafuasi wake, Jeshi la Polisi limewatawanya askari kila pembe ya nchi kuzuia maandamano na mikutano yao ya hadhara. Kuthibitisha kuwa Jeshi hilo linafanya kazi si kwa kufuata kanuni bali maelekezo ya CCM, soma alivyosema Kamanda wake mkoani Mbeya, Ahmed Msangi:
“Watu wenye akili timamu za kuchanganua mambo wamepeleka kesi mahakamani kupinga mchakato wa Katiba. Kwa nini Chadema waingie barabarani kama si kutaka kuleta fujo? Chadema wanatuchokoza na nasema wakithubutu kuandamana, bora nifukuzwe kazi lakini kitu nitakachowafanyia hawatanisahau maishani mwao.” Wahenga wasema “Maneno ni kama fumo, yakitoka mdomoni hayarudi.” Maana yake neno analolitamka mtu ni kama mkuki (fumo), likitoka halirudi na huweza kuleta madhara. Yatunasihi tuwe na tabia ya kuyatafakari maneno tuyasemayo kabla. Ni vizuri kulipima neno kabla ya kulisema na kujiletea majuto baadaye. 
Maneno ya Kamanda Msangi yaonesha mambo manne muhimu: kwanza hajui wajibu wake wa kuwa mlinzi wa usalama wa raia na mali zao. Pili kajitambulisha kuwa ni mkereketwa (shabiki mkubwa) wa CCM na kwamba anafanya kazi kwa lengo la kukitetea hicho kwa hali yoyote hata ikibidi kuwadhuru wafuasi wa Chadema! Kwamba yu tayari hata kufukuzwa kazi kwa atakachowafanyia wafuasi wa Chadema! Tatu anaonekana kuwa na kisasi dhidi ya Chadema na nne kutoa vitisho kwa maneno, kosa linaloweza kumfikisha mahakamani. Anajiamini nini hata atoe vitisho hivyo?
‘Maandamano’ ni matembezi ya watu kwa lengo maalumu kama vile kuadhimisha au kushinikiza jambo. Hufanyika nchi zote duniani. Mwaka 1982 nilikwenda Marekani kufanya mafunzo ya vitendo kwenye jarida la Maryknoll katika mji wa Ossining Kusini Mashariki mwa jiji la New York. Siku Rais Ronald Regan  alipokwenda kulihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, nilikuwa miongoni mwa waandishi waliokuwepo kule. 
Ninachotaka kueleza ni maandamano makubwa ya watu waliopinga utawala wake. Wengine walikaa kwa utulivu n-nje ya jumba la Umoja wa Mataifa wakiwa na mabango ya kumpinga Regan na mengine yakimwita dikteta na muuaji. Waliangaliwa tu na askari na Regan akapitishwa barabara nyingine na kuingilia mlango mwingine pia. Askari waliokuwepo hawakuwasukuma wala kuwatolea vitisho.  Nilipokuwa Washington DC kutembelea jumba la White House, nilishangazwa kuona mamia ya watu wakiwa wamekaa pembezoni mwa jengo lile, pia wakiwa na mabango yenye maandishi tofauti ya kumlaani Rais Regan na serikali yake. Hawakubughudhiwa na askari. Nikavuta hisia ingekuwaje mambo hayo yafanyike pale Magogoni, si kando ya Ikulu bali barabara inayoelekea huko! 
Ndivyo ilivyo katika nchi zinazojali demokrasia na uhuru wa wananchi wake. Huandamana wakiongozwa na askari na magari ya wagonjwa (ambulance) kwa tahadhari ya watakaohitaji huduma ya matibabu ya haraka. Niliona pia maandamano ya mashoga (wanaume wanaoingiliwa na wenzao) nikaachama kwa mshangao! Hawakukatazwa wala kumwagiwa maji ya washawasha au mabomu ya machozi. Ingawa hapa kwetu maandamano hayahitaji kibali cha Polisi bali taarifa tu kuwa siku fulani kutakuwa na maandamano yatakayoanzia mahali fulani mpaka sehemu iliyokusudiwa ili kutoa dukuduku lao huwa vigumu kuyakubali, hasa yale ya wapinzani. Maandamano ni njia ya wanyonge kueleza matatizo yao kwa watawala ingawa Tanzania ni ‘kosa’ linalodaiwa kuhatarisha amani ya nchi! Watawala hawajifunzi kwa wenzao walioondoshwa madarakani kwa njia ya maandamano?