Bungeni: Wanne watajwa kuwa 'watovu wa nidhamu'
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iliyopewa kazi ya
kuchunguza mazingira yaliyochangia uvunjifu wa kanuni pamoja na wabunge
waliohusika wiki iliyopita, ilitoa taarifa yake jana bungeni na
kuwataja Wabunge Tundu Lissu (Singida Mashariki, CHADEMA), Joshua Nassari (Arumeru Mashariki, CHADEMA), Pauline Gekul (Viti Maalumu, CHADEMA) na John Mnyika (Ubungo, CHADEMA) kuwa ndiyo watovu wa nidhamu Bungeni.
Akiwasilisha taarifa ya kamati, Mwenyekiti Hassan Ngwilizi alisema kwa
kutumia ushahidi wa picha za video zilizopigwa na TBC na kumbukumbu za
Bunge, ilibaini wabunge waliokuwa wakisimama, kuwasha vipaza sauti na
kujibizana na kiti cha Spika kinyume na kanuni.
Ngwilizi alisema Mnyika alisimama mara kadhaa akiomba utaratibu licha
ya Kiti kutomruhusu, hali iliyodhihirisha utovu wa nidhamu.
Kwa upande wa Lissu, Nassari na Gekul, walibainika kuzungumza kwa jazba
kwamba ‘mnatuburuza’ na kuamsha ari kwa wabunge wengine hali iliyoibua
vurugu.
Ngwilizi alisema Nassari alikishambulia na kujibizana na Kiti cha Spika akimwambia anabaka kanuni.
Wakati miongoni mwa adidu za rejea ni mazingira yaliyochangia vurugu,
Kamati ilibaini kwamba tafsiri ya muda aliotumia Waziri wa Maji,
Profesa Jumanne Maghembe ndicho kilikuwa chanzo cha vurugu.
Hata hivyo Kamati ilisema muda aliotumia Waziri Maghembe wa dakika 30
ulikuwa sahihi kulingana na kanuni, tofauti na Lissu alivyohoji akidai
anapaswa atumie dakika 15. “Hatua ya kuhoji Kiti kuhusu muda haikuwa
sahihi bali kukilazimisha,” alisema.
Kamati ilisisitiza kwamba Naibu Spika, Job Ndugai alikuwa sahihi
kuondoa hoja bila mjadala. Alisema hoja ilifika hatua ya kujadiliwa na
ilikuwapo dhamira isipokuwa mtoa hoja (Mnyika) alifanya fujo.
“Kilichokosekana ni hali ya utulivu na si kukiukwa kanuni,” alisema.
Ingawa Kamati ya Ngwilizi yenye wajumbe 16 ilipewa kazi ya kutoa maoni
na mapendekezo, katika taarifa yake haikufanya hivyo. Hata hivyo Spika
Anne Makinda alisema Kamati haikufanikiwa kukutana na wabunge
waliobainika kuhusika na utovu wa nidhamu.
Alisema katika kuzingatia utawala bora, Kamati itakutana na kila mmoja
kabla ya kuamua hatua za kuchukuliwa dhidi yao. “Kama Kamati ingekutana
nao, tungechukua hatua,” alisema Makinda.
Kanuni ya 74 inataja adhabu zinazoweza kutolewa na Spika kwa ukiukaji
wa kanuni inaweza kushauri ikiwa ni kosa la kwanza, mbunge asihudhurie
vikao vya Bunge visivyozidi 10. Ikiwa ni la pili au zaidi mbunge huyo
hatahudhuria vikao vya Bunge visivyozidi 20. Hata hivyo, bila kujali
ushauri wa Kamati, Bunge linaweza kumchukulia hatua nyingine za
kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kumsimamisha kazi mbunge aliyetenda kosa.
Wabunge hao hata hivyo, wamewekwa kiporo kusubiri Kamati ikutane nao kabla ya kuamua ni adhabu gani wapewe.
No comments:
Post a Comment