WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO TAARIFA KWA UMMA TAMKO
LA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KULAANI
TUKIO LA UKATILI WA KINGONO ALILOFANYIWA MWANAMKE NA PICHA ZAKE
KUSAMBAZWA KATIKA MITANDAO.
Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesikitishwa na
tukio la ubakaji na udhalilishwaji lililofanywa na wanaume wawili dhidi
ya mwanamke mmoja, ambaye alishurutishwa kuwa mtupu, kufanya ngono bila
ridhaa yake, kupigwa picha na kusambazwa katika mitandao ya kijamii hapa
nchini.
Wizara
inalaani vikali kitendo hiki cha ukatili na udhalilishaji kilichofanywa
na wanaume wawili, ambao wamekamatwa na Polisi kwa kuhusishwa na
udhalilishaji huo. Mazingira ya ukatili huo yanahuzunisha, kwani
inaelezwa kuwa wanaume hao kwa wakati mmoja walihusika kumwingilia
kimwili pasipo ridhaa yake, ilihali,wakimpiga picha za tukio zima la
ubakaji huo. Kitendo hiki, ni ukatili usio na kifani, maana
kimefedhehesha utu wake binafsi na kudhalilisha familia yake, na
wanawake kwa ujumla. Aidha, kitendo hiki kinaweza kusababisha madhara
makubwa kwa mwanamke huyu kimwili,kisaikolojia, kijamii na kihisia.
Wizara
inaamini kuwa, vitendo hivi vya ubakaji na udhalilishaji havistahili
kuvumiliwa hata kidogo, maana vinaashiria kuwepo kwa matumizi ya nguvu,
vitisho, kulazimishwa kuingiliwa, na kuna uwezekano mkubwa wa mwanawake
huyu kuwa katika hali ya hatari zaidi ambayo inagusa maisha yake
binafsi, jambo ambalo ni haki yake ya msingi.
Naomba
ieleweke kuwa, Wizara haitetei ukosefu wa uaminifu miongoni mwa
wanandoa au watu wenye mahusiano ya kimapenzi, bali tunasisitiza kwamba
mwanawake sawa na binadamu wengine anastahili na ana haki ya kuthamaniwa
utu wake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ikumbukwe kuwa uhuru na haki ya kufanya mapenzi ni hiari na kamwe
hayafanyiki kwa kulazimishwa.
Navipongeza
vyombo vya usalama kwa weledi wa kazi yao ambavyo vimewasaka na na
kufanikisha kupatikana kwa watuhumiwa wa ukatili huo. Serikali
itahakikisha mkondo wa sheria unafuatwa kuhakikisha haki inatendeka.
Natoa
wito kwa wananchi wote kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha vitendo hivi
vinakoma kabisa katika jamii zetu za Kitanzania. Hakika huu sio
utamaduni wetu! ni lazima tuhakikishe tunapambana kukomesha tabia za
udhalilishaji wa wanamke na watoto wa kike kwa nguvu zote. Tujenge tabia
ya kutoa taarifa kwa haraka matukio yote ya ukatili dhidi ya wanawake
yanapotokea katika jamii zetu. Aidha, natoa rai kwa mamlaka zinazohusika
na ulinzi na haki za wanawake zihakikishe zinaelimisha jamii kubadilika
na kuhakikisha wanawake wanalindwa maana hawa ni mama zetu, dada, zetu,
na binti zetu. Pia, natoa wito kwa viongozi mbalimbali katika jamii
kutofumbia macho matukio ya udhalilishaji wa wanawake yanayo kiuka
maadili ya jamii yetu.
Naomba
kutoa rai kwa wawakilishi wa kisiasa, watendaji, na wadau wa haki za
watoto kutumia nafasi zetu katika kuelimisha wananchi kuondokana na
tabia za ukatili dhidi ya wanawake, hususan suala zima la udhalilishaji
wa picha za utupu kupitia mitandao ya kijamii, tabia ambayo imeibuka kwa
kasi kubwa katika siku za hivi karibuni. Kamwe Taifa haliwezi
kuhesabika kuwa limeendelea kama utu wa mwanamke utwezwa na
kudhalilishwa usoni mwa mataifa mengine duniani.
Erasto T. Ching’oro
Mkuu wa Kitengo cha Mawasilino
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
No comments:
Post a Comment