Ludovick
Utouh, aliyekuwa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG),
ametaja mambo matatu ambayo yalimkera wakati akiongoza ofisi hiyo,
ukiwamo ubinafsishwaji wa Shirika la Usafiri la Dar es Salaam (UDA)
ambao kesi yake iliondolewa mahakamani bila ya sababu za msingi.
CAG Utouh alisema hayo jana katika mahojiano na Mwananchi kuhusu hali ilivyokuwa kwenye ofisi hiyo nyeti wakati akiiongoza.
Utouh,
ambaye alistaafu mwaka 2014, alitaja mambo mengine kuwa ni uamuzi wa
kusimamisha mita za mafuta kwenye Bandari ya Dar es Salaam na Tanga na
badala yake kutumia upimaji wa kijita, na suala la wafanyakazi hewa.
Akizungumzia
suala la ubinafsishwaji wa Uda, ambao umekuwa ukipigiwa kelele na
wabunge kiasi cha kurushiwa maneno ya kashfa, Utouh alisema hajui sababu
za suala hilo kutoshughulikiwa ipasavyo wakati kila kitu kiliwekwa
bayana.
Alisema
katika ukaguzi huo, kila kitu kilikuwa dhahiri na kesi ikafunguliwa
mahakamani, lakini baadaye ikaondolewa na suala hilo likakoma.
“Ukweli
ukiniambia kwa nini kesi ilitolewa mahakamani sijui. Utekelezaji (wa
mapendekezo ya CAG) ulifanywa nusu, lakini naamini ni jambo ambalo
serikali italifanyia kazi,” alisema.
“Na
pengine ukweli wa mambo utafahamika,” alisema Utouh lakini alipoulizwa
ukweli ni upi, alisema taarifa zote aliziweka kwenye ripoti yake ya
ukaguzi.
Katika
ripoti ya mwaka 2013, CAG anabainisha kuwa tathmini ya hisa na mali za
shirika wakati wa kulibinafsisha mwaka 2009 haukufanywa kikamilifu.
“Ripoti
ya tathmini ya hisa iliyoandaliwa Oktoba 30, 2009 na Novemba 15, 2010
inahusisha uthaminishaji upya wa mali, karakana na vifaa uliofanywa
Agosti 2009, lakini haukuzingatia ukokotoaji wa mali halisi; mali ambazo
jumla yake ni Sh473,241,498 ambazo ziliripotiwa kuwa zilichukuliwa na
Msajili wa Hazina,” inasema ripoti hiyo.
Pia ripoti hiyo inazungumzia uthibitisho wa fedha zilizolipwa na mnunuzi ambaye ni kampuni ya Simon Group.
“Mkataba
wa mgawanyo wa hisa wa Februari 11, 2011 unaeleza kuwa mwekezaji
(mnunuzi) alitakiwa alipe jumla ya Sh1,142,643,935 kwa kuzingatia
ununuzi wa hisa ambazo hazikutengwa za Uda; ingawa mkataba haukubainisha
namba ya akaunti ya benki ambayo malipo hayo yalitakiwa yafanyike,”
inaeleza ripoti hiyo.
“Mwekezaji alilipa jumla ya Sh285 milioni kwenye akaunti namba 01J1021393700 ya CRDB inayomilikiwa na Uda.
“Hakukuwapo
na malipo zaidi yaliyofanywa na mwekezaji kwa ajili ya ununuzi wa hisa
za Uda. Malipo haya ni sawa na asilimia 24.9 ya bei iliyokubaliwa.
Mwekezaji anadai alimlipa mwenyekiti wa Bodi ya Uda jumla ya Sh320
milioni kama ada ya ahadi yake mwishoni mwa mwaka 2009.”
Ripoti
hiyo inasema kuwa mwenyekiti huyo alikiri kupokea fedha hizo, akidai ni
malipo ya ada ya ushauri kutokana na huduma aliyompa mwekezaji, jambo
ambalo ni mgongano mkubwa wa kimaslahi.
Suala
la Uda bado ni gumzo kwenye vikao vya wabunge na wiki iliyopita suala
hilo liliahirishwa kwenye kikao cha kamati ya Bunge inayoshughulika na
serikali za mitaa kutokana na kutokuwapo kwa mwenyekiti.
Wakati fulani wabunge wa Dar es Salaam walipohoji sakata hilo, walijibiwa kuwa “wanafikiri kwa kutumia makalio”.
Utouh
pia alitaja jambo la pili lililomkera kuwa ni mishahara ya wafanyakazi
hewa, akisema alilipigia kelele wakati akiwa CAG na hata CAG wa sasa,
Musa Asad amelipigia kelele lakini halikufanyiwa kazi ipasavyo.
CAG
Utouh alirejea taarifa ya hivi karibuni ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angela Kairuki iliyoeleza kuwa katika
kipindi cha miezi mitatu, wafanyakazi hewa 7,795 wamebainika na
wangesababisha upotevu wa Sh7.5 bilioni.
“Ukiangalia
ukubwa wa pesa zinazopotea na mahitaji ya wananchi, kama kweli mtu ni
mzalendo unaumia rohoni, unaumia rohoni,” alisema.
Kadhalika
CAG Utouh alilitaja jambo la tatu ambalo lilimuudhi kwa kuwa
halikufanyiwa kazi katika uongozi wake kuwa ni ripoti yake ya matumizi
ya ‘flow meter’ za bandarini ambayo aliitoa 2012 na kubaini upimaji
mbovu wa mafuta kwa kutumia mfumo huo.
“Madhara
yake ni makubwa kwa sababu unapotumia mfumo wa kijiti kupima mafuta, ni
subjective (dhahania). Nchi inapoteza fedha nyingi za kodi kwa sababu
ni underdeclaration. Vitu hivi vilionekana na viliripotiwa, lakini
havikufanyiwa kazi,” alisema.
Suala
la wafanyakazi hewa ni moja ya mambo ambayo Utouh alisema yanaisumbua
sana Serikali na ambayo yamelifikisha Taifa katika “utumbuaji majipu”.
Alisema
suala la ufuatiliaji matatizo makuu ya ufuatiliaji wa mapendekezo ya
ripoti za CAG, Utouh alisema chanzo cha mapendekezo hayo kutofanyiwa
kazi ni kukosekana kwa msukumo wa nguvu ya asili na kupuuza.
“Kutekelezwa
au kutokutekelezwa kunasababishwa na vitu viwili. Pasikupokuwa na
msukumo wa nguvu ya asili, mara nyingi hulka ya mwanadamu ni kupuuza.
Sasa mimi nasema, of course kulikuwa na mambo yaliyotekelezwa na ambayo
hayakutekelezwa,” alisema.
“Ni vizuri Serikali kusema kuwa hili halijatekelezwa kwa sababu gani, na kulifanyia kazi,” alisema.
Alisema
taasisi za serikali zinategemeana katika kufanya kazi, kwa hiyo ripoti
ya CAG inapotolewa, Bunge hufanya kazi yake, mapendekezo huweza
kupelekwa Takukuru, kwa Mkurugenzi wa Mashtaka, (DPP) na mahakamani kwa
ajili ya kufanyiwa kazi.
Alisema
ingawa yapo mapendekezo yaliyotekelezwa, baadhi hayakufanyiwa kazi hata
hivyo anaamini yatafanyiwa kazi na Serikali ya Awamu ya Tano.
Maeneo yenye matatizo makubwa
Katika
mahojiano hayo, CAG Utouh alisema halmashauri ndizo zina matatizo
makubwa na kubainisha matatizo hayo kuwa ni malipo ya wafanyakazi hewa,
usimamizi mbovu, mifumo mibovu ya udhibiti wa ndani na udhaifu wa
ukusanyaji wa mapato wa Serikali.
Alisema mambo hayo ndiyo yanayoitingisha Serikali hadi kufikia hatua ya kutumbua majipu.
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii
Akizungumzia
suala la mifuko ya hifadhi ya jamii kukopesha fedha nyingi taasisi za
Serikali ambayo pia hailipi kwa wakati, CAG Utouh alisema ni kweli
aliandika hayo katika ripoti yake.
“Nilipoandika
kwa wakati ule nilikuwa sahihi, lakini kwa sababu sipo sijui maboresho
yaliyotokea. Kwa wakati ule nilichoandika nilikuwa sahihi na hakuna
aliye ni challenge (aliyekosoa),” alisema.
‘Kazi ya CAG ni mbaya’
Utouh pia alisema kazi ya ukaguzi na udhibiti ni ngumu na anashukuru amemaliza salama.
“Kwanza
niseme kazi ya CAG ni kazi moja mbaya, si nzuri, ni kazi ambayo
haifurahishi watu, ni kama hii ya utumbuaji majipu. Baadhi wanaumia,
wengi wanafurahia,” alisema.
Alisema
kazi ya CAG ni kazi ambayo unachokonoa vitu ambavyo watu walitaka
vizikwe kwenye makaburi yaliyojengewa na hivyo suala hilo humuweka
mkaguzi katika wakati mgumu.
“Kwa
hiyo unapoibua unasababisha vitu vingi. Unaleta uhasama na chuki. Kuna
kazi nyingine majaribu kama hayo na vitisho ni lazima vinakuwepo,”
alisema.
Kuhusu
kutishiwa maisha alisema yote hayo ni mambo ya kawaida ya kibinadamu,
kwani wakati mwingine unaona kabisa mtu anakufuata ana dalili ya
kukuhonga lakini unatafuta namna ya kumtoa.
“Namshukuru
Mungu kusurvive (kuwapo) mpaka leo tunazungumza hapa,” alisema na
kufafanua kuwa hawezi kuzungumza kwa undani kwa sababu ya kiapo.
“Kwa
kweli kiapo nilichoapa bado kinanitesa na kitaendelea kunitesa mpaka
naingia kaburini,” alisema akimaanisha kuwa kuna mambo hayawezi
kuyasema.
CHANZO: MWANANCHI.
CHANZO: MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment