Jeshi
la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limeshitushwa na kusikitishwa kwa
taarifa zinazo lituhumu JWTZ kuhusu unyanyasaji wa kijinsia unaodaiwa
kufanywa na Wanajeshi wetu kwa Wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo.
JWTZ
chini ya Umoja wa Mataifa (MUNUSCO) limekuwa likitekeleza majukumu ya
Ulinzi wa amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo takribani miaka
mitatu sasa.Katika muda ambao JWTZ limekuwa nchini Congo hapakuwepo na
tuhuma kama hizo.
Aidha,
JWTZ limetekeleza na limeendelea kutekeleza majukumu kama hayo katika
nchi mbalimbali duniani kama vile Msumbiji, Liberia, Visiwa vya Comoro
(Anjouan), Lebanon, Sudan katika jimbo la Darfur na sehemu nyingi kama
hizo.Katika kutekeleza majukumu hayo JWTZ limeyatekeleza kwa nidhamu na
weledi wa hali ya juu.JWTZ limekuwa moja ya majeshi mengi yanayofanya
vizuri na kutoa mchango mkubwa katika Ulinzi wa amani katika nchi ambazo
limetekeleza majukumu hayo.
Hivi
karibuni kumezuka tuhuma nchini Congo kuhusu Wanajeshi wa JWTZ
kuwanyayasa kijinsia wananchi wa Congo. Kimsingi JWTZ haliwezi kupuuzia
taarifa hizo, hivyo limeanza kuchukuwa hatua za kiuchunguzi ili kubaini
ukweli wa tuhuma hizo ingawa rekodi za majukumu ya ulinzi wa amani
zilizokwisha fanywa na JWTZ sehemu mbalimbali zinaonesha kuwa hakukuwa
na tuhuma kama hizo.
Kufuatia
tuhuma hizo, JWTZ kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa unafanya
uchunguzi wa kina ili kujiridhisha na ukweli wake. JWTZ halitasita
kuchukua hatua kali kwa watakaobainika katika tuhuma hizo. JWTZ bado
lipo imara na linaendelea kutekeleza majukumu yake nchini Congo kwa
kufuata sheria na taratibu za Umoja wa Mataifa.
Imetolewa na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano
Makao Makuu ya Jeshi, Upanga
S.L.P 9203, Simu: 0784-477638/0756-716085
Email:ulinzimagazine@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment