Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe
(pichani), amesema serikali itayafanyia kazi malalamiko yote ya wananchi
yanayojitokeza kwenye huduma ya utoaji haki, yakiwamo ya upepelezi wa
kesi unaochukua muda mrefu na ucheleweshaji wa nakala za hukumu usio na
tija.
Dk. Mwakyembe aliyasema hayo wakati akijibu malalamiko ya wananchi
yaliyojitokeza wakati wa mikutano yake ya kampeni katika ziara yake ya
kutembelea wananchi kusikiliza kero zao wilayani Kyela.
Alisema mambo mengine ambayo yatafanyiwa kazi na wizara yake ni
tatizo la na ubambikizwaji wa makosa kwa wananchi wasio na hatia.
Dk. Mwakyembe alisema wizara yake na ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
zimedhamiria kwa pamoja kumaliza changamoto hizo ndani ya muda mfupi
ujao ili haki itendeke na wananchi kujenga imani kubwa na vyombo
vinavyotoa haki.
Mapema akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika mji mdogo wa
Ipinda, Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Kyela, Dk. Hunter
Mwakifuna, aliitaka serikali ikomeshe vitendo vya rushwa, ucheleweshaji
kesi na kuwabambikizia kesi watu wasio na hatia, upungufu ambao waziri
alithibitisha kuwapo.
"Tumetumia muda mrefu kuisoma hali halisi kwenye vyombo vyote vya
utoaji haki. Upungufu huo upo na dawa yake iko jikoni inatokota,"
alisema.
Alieleza changamoto nyingine kubwa katika utoaji haki nchini ni
uhaba mkubwa wa mahakama za mwanzo ambao tayari Serikali inaufanyia
kazi.
"Uamuzi wa Mheshimiwa Rais hivi majuzi kuipatia Mahakama fedha
zake zote za maendeleo kwa mwaka huu wa fedha, yaani Sh. bilioni 12.3,
ulilenga kuiwezesha mahakama kujenga mahakama za mwanzo zaidi mwaka huu
ili kupunguza adha iliyokuwapo," alisema.
No comments:
Post a Comment