Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli amekutana na makundi mbalimbali yaliyoshiriki katika
kampeni za uchaguzi mkuu 2015 wakiwemo wasanii.
Rais
Magufuli akiambatana na makamu wa Rais Mh. Samia Suluhu Hassani, Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, Mwenyekiti wa Jumuia ya wazazi Abdalah Bulembo
pamoja na mawaziri kadhaa wa serikali yake amekutana na makundi hayo
ikulu jijini Dar es salaam kwa nia ya kuwashukuru na kutoa agizo la
katazo la utoaji wa vibali vya kuagiza sukari kutoka nje ya nchi.
Aidha Dkt Magufuli ameiagiza mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) kufanya
operesheni maalum ya kukamata kazi zote za wasanii zisizo na alama
maalum ya mamlaka ya mapato nchini kufuatia malalamiko ya wasanii
kushindwa kumudu ushindani katika soko kutokana na kazi nyingi
kuingizwa nchini bila ya kulipia ushuru.
Pia amemtaka Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa Na Michezo Mh. Nape
Nnauye kuangalia utaratibu wa chama cha haki miliki Tanzania (COSOTA)
kuwa chini ya wizara yake tofauti na ilivyo sasa ambapo chama hicho kiko
chini ya wizara ya viwanda na biashara.
Kwa upande wake makamu wa Rais Mh. Samia Suluhu hassani amewashukuru
wasanii hao kwa mchango wao uliokiwezesha Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kuwataka kuendelea kushirikiana
na serikali katika masuala mbalimbali ya kuhamasisha maendeleo huku
waziri mkuu Mh Kassim Majaliwa akiwaahidi kusimamia kwa vitendo maagizo
yote yaliyotolewa na Rais.
Kwa upande wasanii hao wamemshukuru Rais kwa uamuzi wake wa kuwaita
na kuzungumza nao ikiwa ni jitihada za kutambua mchango wao katika
uchumi na maendeleo ya nchi na miongoni mwa makundi yaliyofanikisha
chama cha mapinduzi kushinda katika uchaguzi mkuu wa 2015..
No comments:
Post a Comment