Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Sauti ya Umma (SAU), Issa Mohammed Zonga.
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Sauti ya Umma
(SAU), Issa Mohammed Zonga, amesema Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK)
Zanzibar, haijaundwa kuongozwa na CCM na CUF pekee.
Akizungumza na Nipashe mjini haopa jana, Zonga alisema hata kama
CUF haitashiriki uchaguzi wa marudio, hicho si kigezo au sababu ya
kuvunjika kwa serikali hiyo.
“Nchi hii si ya CCM wala CUF. Wananchi ndio wenye uamuzi wa kutaka
kuendelea na serikali ya umoja wa kitaifa au vinginevyo,” alisema.
Alisema kila chama kilichoamua kuingia katika uchaguzi, lengo na
dhamira ni kushinda na si kusindikiza CCM na CUF kama ilivyojengeka
dhana kwa baadhi ya wanasiasa.
Zonga alisema vyama vyote vya siasa vimeibuka baada ya mfumo wa
vyama vingi kwa kuwa kabla ya hapo, ilikuwapo CCM tu, nayo ilisajiliwa
upya baada ya kuanzishwa kwa vyama vingi.
“Nawashangaa sana wanaodharau vyama vingine. Ukiacha CCM na CUF
hapa Zanzibar kwani sisi hatuwezi kuunda serikali ya umoja wa kitaifa
endapo wananchi wataamua?” alihoji Zonga.
Hata hivyo, alisema chama chake kinashiriki katika uchaguzi wa
marudio unaotarajiwa kufanyika Machi 20, mwaka huu na
kimeshaidhibitishia Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) juu ya ushiriki wao.
Naye mgombea urais wa Chama cha Wakulima Tanzania (AFP), Said Soud,
ameiomba ZEC kuharakisha kuwapatia ulinzi wagombea urais wa Zanzibar
wakati nchi ikijiandaa kwa uchaguzi wa marudio.
Soud ambae pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, alisema ni
wajibu wa ZEC kufanya hivyo ili kuepusha matatizo yanayoweza kujitokeza
ikiwamo mgombea yeyote kupata madhara.
Wagombea hao waliwashauri wananchi wote waliojandikisha katika
daftari la kudumu la wapigakura, kujitokeza kwa wingi kutumia haki yao
hiyo ya kikatiba kuchagua viongozi wanaowataka.
No comments:
Post a Comment