NAIBU Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Luhanga
Mpina amewapa siku saba viongozi wa kiwanda cha kutengeneza vyandarua
cha A to Z cha hapa kulipa faini ya Sh milioni 70 kilichopigwa na Baraza
la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) kwa uharibifu wa mazingira.
Nemc ilitoa adhabu hiyo Septemba mwaka jana baada ya uongozi wa
kiwanda kukutwa na makosa hayo kutokana na uharibifu wa mazingira.
Inadaiwa kimekaidi kulipa faini hiyo kwa miezi mitano. Mpina alitoa
maagizo hayo baada ya kuzungumza na menejimenti ya kiwanda hicho juzi.
Alisema serikali haiwezi kukubali ukaidi unaofanywa na mwekezaji
yeyote kwa sababu yoyote na kwamba wakishindwa kulipa faini hiyo ndani
ya siku hizo, kiwanda hicho kitafungwa.
“Hii ni dharau ya hali ya juu na kamwe serikali ya awamu ya tano
haiwezi kukubali dharau ya namna hii. Hivyo kwa kuwa mmekiri wenyewe
kukiuka sheria kama mlivyoelekezwa na NEMC, hakuna kisingizio chochote
ambacho serikali itakubaliana nacho katika hili,” alisema naibu waziri.
Aliendelea kuwaambia, “Kama kweli mna nia njema, badala ya kuendelea
kuandika barua za visingizio mngeomba hata kupunguziwa hiyo faini au
hata kulipa kwa awamu lakini inaelekea mmeamua makusudi kukaidi maagizo
halali ya serikali. Sasa nawapa siku saba mlipe vinginevyo tutakifungia
kiwanda.”
Awali, Mkurugenzi Uendeshaji wa Kiwanda hicho, Binesh Haria
alijitetea kwamba wameshindwa kulipa faini hiyo kutokana na mawasiliano
yanayoendelea kati yao na NEMC kuhusu masharti mbalimbali waliyopewa na
baraza hilo katika kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama.
Hoja hiyo ilipingwa na Mratibu wa NEMC, Kanda ya Kaskazini, Dk Menan
Jangu aliyesema tangu kiwanda hicho kilipopigwa faini kimekuwa
kikijaribu kukwepa faini hiyo kwa kuandika barua zenye visingizio
mbalimbali.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Mpina alitembelea mfumo wa hifadhi ya
maji machafu yanayotumika kiwandani na kuagiza maofisa wa NEMC kufanya
ukaguzi wa mara kwa mara kuhakikisha maji hayo yenye sumu hayasababishi
madhara kwa wananchi wa maeneo yanayozunguka kiwanda hicho.
No comments:
Post a Comment